Cerca

Vatican News
Kipindi cha Majilio: Toba na wongofu wa ndani ni chachu ya matumaini ya Kikristo! Kipindi cha Majilio: Toba na wongofu wa ndani ni chachu ya matumaini ya Kikristo!  (ANSA)

MAJILIO: Toba na wongofu ni chachu ya matumaini ya Kikristo!

Toba na wongofu wa ndani ni kati ya matendo makuu ya Kipindi cha Majilio. Huu ndio mwaliko wa kutubu anaoutoa Yohane Mbatizaji akisema: “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake”. Kila mmoja wetu anaalikwa kujitafakari namna ya jangwa lililomo katika moyo wake.

Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.

Habari ya Yohane Mbatizaji ni simulizi mahususi wakati wa kipindi cha Majilio. Dominika ya Pili ya Majilio hujikita katika kuuelezea unabii wake. Yeye anajitambulisha kama “Sauti ya mtu aliaye nyikani”. Anaelezewa kama mtangulizi wa Bwana na ambaye anamtambulisha Kristo katika jamii ya watu. Katika masimulizi ya Injili Yohane anaelezewa kuwa na unasaba na Kristo kwani mama yake Yohane Elizabeti alikuwa ni binamu ya Bikira Maria, Mama yake Kristo (Lk 1:36). Pamoja na udugu huu, masimulizi ya Injili hayaoneshi unasaba uliokuwa juu yao wakati wa utume wao. Yohane Mbatizaji anatambulishwa kama mtangulizi na anayemwandalia Kristo njia. Aliutambua ukuu wake ndiyo maana hata wakati wa ubatizo wake alisita kumbatiza Kristo. Huyu ndiye Yohane Mbatizaji ambaye ni sauti iliayo nyikani akisema: “itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake”. Hii ndiyo dhamira ya Dominika ya pili ya Majilio, yaani kufanya toba na kumwandalia Mungu mahali ili akae nafsini mwetu.

Utume wa Yohane Mbatizaji unafanyika nyikani ama jangwani. Ni maeneo ambayo hayavutii, makavu, pengine huwa na vitisho na hayaoneshi uhai wa namna yoyote. Lakini katika lugha ya kiimani kwa jamii ya kiyahudi jangwa lilieleweka kama mahali pa kukutana na Mungu na kuunganika naye. Hapa ni mahali ambapo Mungu alipata fursa ya kukutana na watu wake katika muunganiko wa kiroho na anajiweka kwao kama mchungaji. Katika hali hiyo ya upweke wa jangwani Yeye anakuwa kimbilio pekee na ishara ya matumaini. Mungu wa Israeli ni mwaminifu kwa dhamana yake na anaweka ahadi zake za wokovu. Anawaita tena watu wake jangwani, kutangaza kwao kuwasili kwa Masiha. Lakini Mungu daima anatarajia ushirikiano kutoka kwa mwanadamu na atataka kutoka kwake ubatizo wa uongofu, utakaso wa dhambi zake, na jitihada za kushinda vikwazo vinavyomzuia kuyaona mapambazuko ya wokovu.

Hapa inaonekana tabia mojawapo ya kipindi cha Majilio, tendo la toba. Huu ni mwaliko wa kutubu anaoutoa Yohane Mbatizaji akisema: “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake”. Kila mmoja wetu anaalikwa kujitafakari namna ya jangwa lililomo katika moyo wake. Hizi ni nyakati zenye kutatisha tamaa mmoja anazozipitia; haya ni matendo yanayokatisha tamaa kutokana na dhuluma kati ya wanadamu; ugomvi na husuda; ni matendo maovu yanayotutenga na Mungu na hata ndugu zetu. Hali hii wakati mwingine hutudanganya kwa kitambo kuwa tupo sawa lakini mara nyingi hutuingiza katika msongo wa mawazo na kumkimbilia Mungu. Katika jangwa hili Mungu anakuwa pamoja nasi; anadhihirisha uwepo wake uliojaa upendo katika hali zote na anakuita akitaka uitengeneze njia ya moyo wako kusudi Masiha au Mkombozi wako apate mahali pa kupita na kukaa pamoja na wewe.

Nabii Baruku anaielezea vema njia hiyo ya toba inayofikisha katika matumaini mapya. Anawaalika wana wa Israeli kuvua mavazi ya toba ili waokolewe kutoka uhamishoni na kuifanya Yerusalemu ing’ae ulimwenguni kote kwa mkono wa Mungu. Ulikuwa ni mwaliko wa kuinua macho yao na kuutazama ukuu wa wokovu wa Mungu. Baruku alikuwa ni mwandishi wa Nabii Yeremia. Yeye mwenyewe anauandika unabii wake huu wakati Israeli ikiwa utumwani Babeli. Katika mazingira haya anawapatia habari ya matumaini kwamba waondoe huzuni yao na kujivika mavazi ya utukufu. Mungu anawarudia tena na ananuia kuwafanya kuwa taifa kubwa na lenye nguvu ambalo kwalo watu wa mataifa yote watakusanyika: “Ondoka Ee Yerusalemu, utazame wanao wanavyokujia”. Hali yao ya utumwani itakoma na wataingia katika utukufu kwa kuwa Mungu wao anawaletea wokovu. “Bwana atamletea Israeli furaha”.

Mwaliko tunaoupata katika Dominika hii ni kuangalia yaliyo mabonde na kuyajaza, kuangalia milima na kuisawazisha na palipoparuzwa kupasawazisha. Mabonde hayo ni upungufu katika maisha yetu ya kiroho. Ni wakati wa kutafakari nini ambacho kinatufanya kuwa dhahifu na kuonesha upungufu. Pengine ni uvivu wangu katika sala, kutokushiriki vema masakramenti, kutojishibisha na Neno la Mungu n.k. Milima ndani mwangu inaweza kuelezewa na kiburi changu na kujikweza mbele ya watu. Kiburi hiki kinaweza kuchagizwa na uwezo wa kidunia iwe ni akili nyingi au mali nyingi kiasi cha kutokuiona nafasi ya Mungu na umuhimu wake katika maisha yangu. Mikwaruzo katika maisha yangu huenda ni zile hali ambazo zinanikosesha amani na raha. Mahusiano yasiyo sawa na jirani zangu na magomvi ya mara kwa mara. Haya pamoja na mengine ndiyo ambayo Mungu anatuambia kupitia kinywa cha Nabii Baruku kuwa amekuja kuyaangusha chini na kujazia palipopungua “ili Israeli aende kwa bidii kwa heshima ya Mungu”.

Hali hiyo mpya tumekwishaipokea kwa njia ya Ubatizo wetu, yaani pale tulipofanywa kuwa wana wa Mungu. Tuliipokea hadhi iliyotutoa katika vazi la kale, vazi la huzuni na mahangaiko, vazi la utumwa na kuvikwa vazi jipya na kukombolewa na Kristo. Mtume Paulo anatukumbusha umuhimu wa kuitunza hali hiyo. Na hapa anatupeleka katika maandalizi mengine ya juu zaidi ya kuingojea siku ya ujio wa pili wa Kristo. Yeye anasema: “Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo”. Hili ni himizo linalotutaka kubaki waaminifu katika wokovu tulioupokea hadi ujio wa pili wa Kristo. Hivyo kipindi hiki cha Majilio kinatuandaa katika ujio huo pale ambapo tutang’aa kama nyota kwa sababu ya matendo yetu mema na kujiunga naye katia furaha za ufalme wa mbinguni.

Hii inatutaka sisi kuwa vyombo vya kuieneza furaha ya Injili ambayo tumeipokea kwa maneno yetu na kwa mfano wa maisha yetu. Furaha ya Injili hujidhihirisha katika matendo ya upendo kwa Mungu na jirani. Hatari inayotunyemelea mara nyingi sisi tulio wafuasi wa Kristo ni kuwa na bidii ya kulihubiri neno lake bila kulitenda. Mafundisho ya Kristo katika maisha yake yote ya hadharani yalijikita katika kujifunua kwa ndugu yako aliye karibu yako. Hata mifano mbalimbali ya Watakatifu inatuthibitishia dhahiri kuchanua kwa furaha ya Injili ndani yake Yeye aliyempokea Kristo.

Hivyo tunapaswa kuifanya hai daima furaha yetu kwa kuwa sababu ya furaha kwa wengine. Wajibu anaokuwa nao Yohane Mbatizaji, wajibu wa kuifanya mioyo ya watu kutulia unabisha hodi katika nafsi yangu na yako na hivyo kwa njia ya mfano wa maisha yaliyojaa upendo tunakuwa watangulizi wa Kristo na wakati huo huo tunaindaa mioyo yetu ili atakapokuja tena atukute tupo imara katika imani, tunamngojea kwa matumaini na tumeshamiri katika upendo wetu kwa Mungu na kwa jirani zetu.

Majilio J2
06 December 2018, 10:54