Tafuta

Vatican News
Waraka wa Maaskofu Katoliki Kenya: Utu na heshima ya wananchi wa Kenya vipewe kipaumbele cha kwanza! Waraka wa Maaskofu Katoliki Kenya: Utu na heshima ya wananchi wa Kenya vipewe kipaumbele cha kwanza! 

Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, 2018

Waraka wa Maaskofu Katoliki Kenya: Mkazo: ulinzi na tunza ya watoto kimaadili, changamoto na hatima ya wakulima wadogo wadogo nchini Kenya; umuhimu wa kukuza na kudumisha siasa fungamani na katika kanuni maadili; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; mfumo wa kodi na wajibu wa Serikali katika maboresho ya maisha kwa maskini nchini Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mapadre wa Kenya waliouwawa Kusini mwa Sudan na Cameroon; ulinzi na tunza ya watoto kimaadili, changamoto na hatima ya wakulima wadogo wadogo nchini Kenya; umuhimu wa kukuza na kudumisha siasa fungamani inayojikita katika kanuni maadili; mapambano dhidi ya saratani ya rushwa na ufisadi; mfumo wa kodi na wajibu wa Serikali katika maboresho ya maisha kwa maskini; madini na maliasili ya Kenya kwa ustawi na maendeleo ya wengi; mfumo wa usafiri salama na makini; kura ya maoni na Mabadiliko ya Katiba ni kati ya mambo tete yaliyomo kwenye Waraka wa Kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Kenya!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Waraka wake kichungaji linasema, limesikitishwa sana na mauaji ya kikatili waliyofanyiwa Padre Victor Luke Odhiambo huko Sudan ya Kusini pamoja na Padre Cosmas Omboto Ondari aliyeuwawa nchini Cameroon. Maaskofu wanapenda kutoa salam za rambi rambi kwa familia ya Mungu nchini Kenya. Wanaziombea roho za marehemu Mapadre hawa waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, ziweze kupumzika katika usingizi wa amani, kwa matumaini ya ufufuko na maisha ya uzima wa milele!

Maaskofu wanawataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wana wapatia watoto wao malezi bora na makini yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, kimaadili na kiutu, ili kupambana na mmong’onyoko wa kimaadili ambao umeanza kuonesha makucha yake katika masuala yafutayo: kumekuwepo na tuhuma za unyanyasaji wa watoto kijinsia; ongezeko la mimba za utotoni pamoja na kuendelea kushamiri kwa utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba nchini Kenya. Nyanyaso na ukatili wa kijinsia ni dalili za jamii inayoendelea kukengeuka na kutopea katika maadili na utu wema. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linataka kutekeleza kwa dhati sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo.

Kumekuwepo na ongezeko la mimba za utotoni, hali inayokwamisha juhudi za kuwainua wasichana kwa njia ya elimu makini, endelevu na fungamani. Maaskofu wanaitaka Serikali kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika wote, ili sheria iweze kushika mkondo wake na wawe ni fundisho kwa wengine. Wazazi wahakikishe kwamba, wanatekeleza vyema wajibu wao mintarafu malezi na makuzi ya watoto wao kadiri ya Mafundisho ya Kanisa na utu wema! Utamaduni wa kifo unaendelea kushika kasi nchini Kenya kiasi cha kutishia: uhuru, usalama na Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo! Huu ni wakati wa kurejea tena kwenye misingi ya maadili na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kulinda, kuheshimu, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai.

Kuhusu changamoto na hatima ya wakulima wadogo wadogo nchini Kenya, Maaskofu wanasikitika kuona kwamba, wakulima hawa wanakosa soko la mazao yao na wakati huo huo serikali inaendelea kuagiza mazao yanayopatikana kwa wingi na kwa bei nafuu nchini humo. Kuna maelfu ya wakulima ambao hawajalipwa fedha zao, dalili za rushwa na ufisadi wa mali ya umma, changamoto kwa Serikali kuhakikisha kwamba, wakulima wanatendewa haki nchini Kenya, kwa kulinda mazao yao dhidi ya ushindani usiokuwa na tija wala faida kwa wakulima wa Kenya. Wakulima walipwe vizuri na kwa wakati na serikali iwakingie kifua pale inapobidi na wahujumu uchumi washughulikiwe kikamilifu!

Wanasiasa wanapaswa kudumisha siasa fungamani inayofumbatwa katika kanuni maadili; kwa kulinda na kutetea usalama wa raia na mali zao; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa dhidi ya ukabila na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto. Uongozi unapaswa kueleweka kuwa ni huduma ya kutukuka kwa wananchi! Kumbe, viongozi wanapaswa kujielekeza katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, kwa kuboresha maisha ya wananchi yanayofumbatwa katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani. Rushwa na ufisadi bado ni saratani inayosigina utawala wa sheria na demokrasia fungamani. Wahusika wanapaswa kushughulikiwa kikamilifu, ili kujenga na kudumisha utawala bora na dhamiri nyofu. Hapa utashi wa kisiasa ni muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Mfumo wa kodi na wajibu wa Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi wa Kenya ni mambo ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limejadili kwa kina na mapana!

Kodi na mapato ya serikali yachangie maboresho ya maisha na ustawi wa wananchi wa Kenya, vinginevyo, watu watahisi kwamba, kodi ni mzigo mzito usiobebeka katika maisha yao! Sera na umakini wa ukusanyaji kodi; ukweli na uwazi wa matumizi ya kodi ya wananchi pamoja na maboresho ya maisha ya wananchi ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika masuala ya kodi nchini Kenya. Katika sera hizi, utu na heshima ya wananchi wa Kenya inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Ugunduzi wa maliasili na madini sehemu mbali mbali za Kenya usiwe ni mwanzo wa vita na mipasuko ya kijamii! Wananchi walipwe stahiki zao; walindwe na kushirikishwa kikamilifu kabla ya miradi kuanza kutekelezwa. Wananchi wanataka kuona utawala wa sheria; ukweli na uwazi vinafuatwa kikamilifu katika matumizi ya rasilimali za nchi na kama sehemu ya mapambano dhidi ya umaskini nchini Kenya. Utajiri wa madini na maliasili visiwe ni kwa ajili ya mafao ya wajanja wachache ndani ya jamii, bali kielelezo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, sheria za usalama barabarani zinafuatwa kikamilifu ili kupunguza ajali barabarani zinazoendelea kupukutisha nguvu kazi. Wavunja sheria hasa katika usafiri wa umma washughulikiwe bila kupepesa pepesa macho! Hata hivyo raia wa Kenya wanakumbushwa kwamba, wao pia ni wadau wa ulinzi na usalama wa maisha na mali zao, kumbe, wanapaswa kuwajibika barabara. Mwishoni Maaskofu wanasema, kuna haja kwa Kura ya Maoni na mabadiliko ya Katiba kuendelea kujadiliwa na wananchi ili waweze kufahamu undani wake, tayari kujenga madaraja ya watu kukutana na kujadiliana ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wananchi wajiandae kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, badala ya kuwaachia wanasiasa kumezwa na ubinafsi. Mabadiliko ya Katiba yaendelee kujadiliwa na wananchi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; daima: haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa vikipewa kipaumbele cha kwanza!

Waraka: Maaskofu Kenya

 

 

06 December 2018, 11:28