Tafuta

Vatican News
Wema, huruma, upendo na ukuu wa Mungu unamwilishwa katika matendo ya huruma kwa jirani! Wema, huruma, upendo na ukuu wa Mungu unamwilishwa katika matendo ya huruma kwa jirani!  (AFP or licensors)

Wema, ukuu na ukarimu wa Mungu unavyomwilishwa katika matendo ya huruma kwa jirani!

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tunaongozwa na dhamiri kuu: ukarimu, ukuu na wema wa Mungu katika maisha ya binadamu kwa sababu ombi la Mungu kwetu limefumbata ndani yake wema wake mkuu na ukarimu wake mkubwa ajabu.

Na Padre William Bahitwa. - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News popote pale ulipo, tunapotafakari kwa pamoja Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, huku tukiongozwa na dhamiri kuu: ukarimu, ukuu na wema wa Mungu katika maisha ya binadamu kwa sababu ombi la Mungu kwetu limefumbata ndani yake wema wake mkuu na ukarimu wake mkubwa ajabu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (1 Waf. 17:10-16) Ni simulizi la namna mtumishi wa Mungu Nabii Eliya alivyopata kulishwa katika kipindi cha njaa, nchi ilipokosa mvua. Mungu anamtuma kwa mama, mjane wa mji ulioitwa Serepta. Huu ni mojawapo ya miji ambamo wakazi wake hawakuwa wanamwabudu Mungu, walikuwa wanaabudu miungu baali, na inawezekana pia mama huyu alikuwa ni mmojawapo wa wale waliokuwa waabudu miungu baali. Mama huyu alikuwa ni mjane. Mara nyingi katika Agano la Kale, mjane alihusishwa na watu wenye shida. Wajane, wazee na watoto wanatajwa daima kuwa wahitaji, masikini, watu wenye shida (Rej. Ayubu 24:3-4). Na zaidi ya hapo mama huyu mjane alikuwa amebakiza chakula cha siku moja tu. Cha ajabu ndiye aliyemhifadhi Eliya na kumpa chakula hadi hapo njaa ilipoisha. Kwani kadiri ya Neno la Bwana “pipa la unga halitapunguka wala chupa ya mafuta haitaisha”.

Somo hili lenye mafundisho mengi linatuonesha kwanza ukuu wa Mungu. Mungu ni mkuu kuliko miungu mingine yote na ana nguvu hata nje ya mipaka ya Israeli hivi kwamba hata katika himaya ya miungu hiyo anawashushia baa la njaa. Na katika uwezo wake hakuna kisichowezekana. Mungu anaweza kumtumia yoyote kukamilisha kazi na mipango yake duniani. Anamtumia mwanamke mjane, nje ya Israeli na ambaye hata huenda alikuwa anaabudu miungu wengine awe ndio mtekelezaji wa mipango yake, kumpa chakula mtumishi wake Eliya. Somo hili pia linalokazia fadhila ya ukarimu. Ndiyo fadhila aliyokuwa nayo mama huyo mjane na ndiyo fadhila Mungu aliyoiona kwake akamtumia.

Somo la pili (Ebr. 9: 24-28) kutoka waraka kwa waebrania linaendeleza dhamira ya ukuhani wa Kristo, dhamira iliyoanza dominika zilizopita. katika somo la leo Kristo anaelezwa kuwa ni kuhani ambaye alijitoa sadaka yeye mwenyewe. Makuhani wa ukuhani wa Haruni, somo linatueleza, walizoea kuingia kila mwaka patakatifu pa patakatifu kutolea sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu. Walipoingia huko patakatifu pa patakatifu walitolea sadaka wanyama waliokuwa wanaandaliwa. Kristo yeye kama kuhani mkuu, kwanza aliingia patakatifu pa patakatifu halisi yaani mbinguni na sadaka aliyoitoa sio ya wanyama bali alijitoa mwenyewe sadaka. Alitoa sadaka moja na iliyokamilika isiyohitaji kurudiwa kila mara kama walivyofanya makuhani wa ukuhani wa Haruni. Sadaka ya Kristo, moja tu inatosha kwa nyakati zote hata atakaporudi kwa wokovu wa hao wamtazamiao, yaani wanaomwamini, wanaomkiri na wanaomuishi katika maisha yao.

Sadaka moja tu ya Kristo inayozungumzwa hapa ndiyo ile ya kifo chake msalabani kwa kumwaga damu yake azizi. Ndiyo sadaka ile ile ambayo kanisa linaendelea kuiadhimisha katika Misa Takatifu mpaka atakaporudi. Misa zinaadhimishwa mara nyingi na katika mahali pote dunia nzima lakini katika Misa zote hizo sadaka inayotolewa ni ile ile ya Kristo msalabani, sadaka inayotolewa bila kumwaga damu altareni. Naye ni Kristo yule yule anayejitoa sadaka. Padre mwadhimishaji wa Misa anaadhimisha katika nafsi ya huyo huyo Kristo, na ni Kristo asemaye “twaeni mle wote, huu ndio mwili wangu... twaeni mnywe nyote hii ndiyo damu yangu”. Hili ni somo linalotupa kiini, na fundisho linalotuambia Misa tunayoadhimisha na kuishiriki ni nini hasa.

Injili (Mk 12:38-44) Injili ya leo inaweka mbele yetu makundi mawili ya watu yanayotupatia picha mbili tofauti. Inatupatia katika upande mmoja waandishi na katika upande mwingine ya mama mjane. Waandishi walikuwa ni wale waliokuwa wamesomea Maandiko Matakatifu na ndio waliokuwa wakiyatafasiri na kuwafundisha waisraeli. Walikuwa na nafasi katika sinagogi. Mjane yeye hakuwa na nafasi yoyote isipokuwa ile ya mshiriki wa kawaida wa ibada.

Tena waandishi wanaelezewa kwa sifa nyingi: walikuwa na mavazi marefu, walikuwa wanasalimiwa masokoni, walikaa mbele katika masinagogi, walikuwa katika nyumba za wajane na walisali sala ndefu kwa unafiki. Mama mjane kwa upande wake anaelezwa kwa sifa moja tu: alikuwa masikini. Na katika umasikini wake anatoa sentii mbili kama sadaka katika mfuko wa hazina. Hapo Yesu anasema mjane huyu ametoa kuliko wote, sio tu kuliko waandishi walioelezwa kwa sifa nyingi bali ametoa hata kuliko matajiri ambao wao walitoa sehemu ya mali iliyowazidi bali yeye alitoa yote aliyokuwa nayo.

Katika mafundisho haya ya Yesu, tunaona utofauti unaoweza kuwapo kati ya nafasi ambayo mtu anaipata mbele ya watu na anayoipata mbele ya Mungu. Heshima na kusalimiwa na umati kama waliyokuwa nayo waandishi; mavazi marefu yaani cheo au nguvu ya madaraka, elimu na mali havimpi mtu tiketi ya moja kwa moja ya kukubalika pia mbele ya Mungu. Kinachompa mtu tiketi hiyo ni kiu yake ya ndani, kiu ya kutamani kujaza moyo wake na uwepo wa Mungu,  ndiyo umaskini wa roho kama wa yule mama mjane. Vitu kama heshima, vyeo, elimu, mali nk, mtu awe navyo au asiwenavyo, anapaswa kupalilia bado mahusiano ya ukaribu na Mungu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika jumapili ya leo tunaalikwa kutafakari juu ya kumwitikia Mungu kwa ukarimu. Mwenyezi Mungu daima hupenda kututumia sisi ili kukamilisha kazi yake na mipango yake kwetu, kwa wenzetu na kwa ulimwengu mzima. Na ni ajabu kabisa kwamba Mungu kwa uwezo na ukuu wake anahitaji bado utayari wetu.  Na mara nyingi tunaona kana kwamba Mungu anatudai mambo makumbwa sana tusiyoyaweza au yanayoweza kuturudisha nyuma au kutupa ugumu fulani katika maisha yetu.

Maandiko ya leo yanatupa picha tofauti kabisa: tukijitoa kwa Mungu kwa ukarimu kile tunachokiona kidogo kitafanya mambo makubwa kwetu na kwa wenzetu.  Hii ni kwa sababu ombi la Mungu kwetu limefumbata ndani yake wema wake mkuu na ukarimu wake mkubwa ajabu. Tumwitikie basi Mungu kwa ukarimu katika yale aliyotujalia na katika utume mbalimbali anaoutuitia.

Liturujia 32

 

10 November 2018, 06:38