Cerca

Vatican News
Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu: Urithi wa Uinjilishaji ni: Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Bikira Maria Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu: Urithi wa Uinjilishaji ni: Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Bikira Maria 

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji: Urithi: Neno la Mungu, Ekaristi & Bikira Maria

Wamisionari wa kwanza waliona hatari kubwa iliyokuwa inawakabili mbele yao, lakini kwa nguvu ya Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu, tunza na ulinzi wa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, wakathubutu kujitosa kimasomaso, leo hii imani kwa Kristo Yesu imeenea ndani na nje ya Tanzania!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania, Jumamosi, tarehe 3 Novemba 2018, Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha aliwasha moto wa Injili, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika mahubiri ambayo yalijaa hisia kali za moyo wa shukrani kwa zawadi ya imani; unyenyekevu, toba na msamaha kutokana na mapungufu ya kibinadamu yaliyojikita katika: majivuno, kiburi na kujikweza na hata wakati mwingine, baadhi ya watu wa familia ya Mungu nchini Tanzania wakajihesabia haki kutokana na huduma na kusahau kwamba, cheo ni dhamana!

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, familia ya Mungu nchini Tanzania inapaswa kuomba msamaha, neema na baraka, tayari kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota angavu ya uinjilishaji mpya, mfano na kielelezo cha utii na unyenyekevu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, kiasi kwamba, akabahatika kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa! Askofu mkuu mstaafu Lebulu, amewakumbusha waamini waliofika Bagamoyo Mlango wa Imani mahali yalipo makaburi ya wamisionari wa kwanza, waliolala katika usingizi wa amani wakiwa na matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele!

Hawa ni wamisionari waliothubutu kupiga moyo konde hata katika umri wa ujana wao kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; wengi wao wamefariki dunia wakiwa na umri kati ya miaka 25, 34 na 40! Wamisionari hawa waliona hatari kubwa iliyokuwa inawakabili mbele yao, lakini kwa nguvu ya Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu, tunza na ulinzi wa Bikira Maria, wakathubutu kujitosa kimasomaso, leo hii imani kwa Kristo Yesu imeenea ndani na nje ya Tanzania! Kwa ari na moyo mkuu, Askofu mkuu mstaafu Lebulu anasema, katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko, Kristo Yesu, ameliachia Kanisa zawadi kuu tatu, kama kielelezo cha uwepo wake endelevu katika maisha na utume wa Kanisa!

Askofu mkuu mstaafu Lebulu anasema, zawadi ya kwanza ni “Neno la Mungu”. Amekumbusha kwamba, Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake! Katika maisha na utume wake, akawatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, iliyokita mizizi katika akili na nyoyo za Mitume wake, wakawa tayari kuitangaza na kuishuhudia sehemu mbali mbali za dunia, kama kumbu kumbu endelevu ya uwepo wa Kristo kati yao!

Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu akaweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, inayofumbatwa katika huduma ya upendo, kama kielelezo cha uwepo wake endelevu katika Maumbo ya Mkate na Divai, chakula cha njiani kinachozima njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele! Hii ndiyo zawadi ya pili ambayo Kristo Yesu, ameliachia Kanisa lake. Kila mara, Kanisa linapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, linafanya ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, muhtasari wa imani iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume pamoja na waandamizi wao, hadi kuifikia familia ya Mungu nchini Tanzania. Waamini wanapofanya kumbu kumbu hii ya uwepo endelevu wa Kristo kati yao, wanapaswa kuiadhimisha kwa moyo wa ibada na uchaji wa Mungu na kamwe wasiadhimishe Mafumbo ya Kanisa kwa mazoea!

Bikira Maria ni nyota angavu ya uinjilishaji, aliyekubali kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake; akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Bikira Maria akaambatana na Mwanaye mpendwa katika maisha na utume wake, kiasi hata cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia upanga mkali ukipenya moyoni mwake kwa kumwona Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu, akiwa ametundikwa Msalabani, pale Mlimani Kalvari! Akiwa Msalabani, Yesu, akawakabidhi wafuasi wake wote na kwa namna ya pekee waliokuwa mjini Bagamoyo chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, nyota ya uinjilishaji mpya! Tangu wakati huo, Bikira Maria amekuwa ni Mama wa Mungu na wa Kanisa! Zawadi ya tatu, ambayo Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake!

Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha alizaliwa kunako tarehe 13 Juni 1943 huko Kisangara, Jimbo Katoliki la Same, Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikuhani, tarehe 11 Desemba 1968 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 12 Februari 1979 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Same na kuwekwa wakfu tarehe 24 Mei 1979. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Arusha kunako tarehe 28 Novemba 1998 na tarehe 16 Machi 1999 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha.

Katika maisha na utume wake kama: Padre amelitumikia Kanisa kwa miaka 50 na kama Askofu takribani miaka 40. Tarehe 27 Desemba 2017, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani. Hiki ni kipindi kirefu chenye changamoto na madai makubwa. Ni kipindi ambacho Askofu mkuu Josaphat Louis Lebulu amekiishi kwa ukarimu na uthubutu mkubwa, alikuhudumia kwanza kam Padre wa Jimbo Katoliki Same,  Askofu wa Jimbo Katoliki la Same na baadaye kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha.

Lebulu 50 Yrs
07 November 2018, 10:14