Tafuta

Vatican News
Kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Toba, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Bikira Maria, Utakatifu na elimu makini Kilele cha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Toba, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Bikira Maria, Utakatifu na elimu makini 

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Yaliyojiri!

Askofu Mkude amewahimiza waamini nchini Tanzania, kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo na Kanisa lake. Amewataka waamini kutambua uwepo na madhara ya dhambi katika maisha yao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu utakaowaimarisha zaidi katika imani inayomwilishwa katika ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Telesphory Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, mwenyeji wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania, tarehe Mosi, Novemba, 2018 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, ufunguzi wa Jubilei hii, sanjari na kuwakumbuka pamoja na kuwaombea Wamisionari marehemu waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, amewahimiza waamini nchini Tanzania, kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kupyaisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo na Kanisa lake. Amewataka waamini kutambua uwepo na madhara ya dhambi katika maisha yao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu utakaowaimarisha zaidi katika imani inayomwilishwa katika ushuhuda na matendo!

Askofu Mkude amewataka waamini kuendelea kuimarisha utume wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani, AMECEA!  Amewasihi waamini kudumisha Ibada ya Rozari kwa Bikira Maria, muhtasari wa historia ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa Rozari Takatifu, amebarikiwa kuliko wanawake wote, ni sura ya Kanisa iliyovishwa mwanga wa Pasaka; Yeye ni heshima ya watu wa Mungu; mshindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo!

Bikira Maria ni shuhuda wa unabii wa upendo wa huruma ya Mungu; mwalimu mahiri wa Habari Njema ya Mwana wa Mungu, alama ya moto wa Roho Mtakatifu. Huku bondeni kwenye furaha na machozi, Bikira Maria awafundishe watoto wake ukweli wa milele, ambao Baba wa milele, anapenda kuwafunulia wadogo. Bikira Maria awaoneshe ulinzi na tunza ya mkono wake wenye nguvu! Moyo wake usiokuwa na doa uwe ni kimbilio la wadhambi, njia inayowaelekeza kwa Mwenyezi Mungu.

Mada kuhusu “Mlei Mkatoliki katika Kuyatakatifuza Malimwengu” imetolewa na Padre Raymond Saba, kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma, ambaye amewahi kuwa pia Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Anasema,  kwa njia ya utakatifu wa maisha, Kanisa nchini Tanzania linaweza kupyaisha ari ya maisha ya kiroho na utume wake. Mafuta ya utakatifu yanaweza kulisaidia Kanisa kuganga na kutibu majeraha ya watoto wake na walimwengu katika ujumla wao, kwa kuonesha utimilifu wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Hivi ndivyo anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kuchuchumilia furaha ya kweli katika maisha na kuondokana na tabia ya kutaka kuyakumbatia malimwengu na raha zake! Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuchuchumilia neema ya utakaso waliyoipokea wakati wa Ubatizo na hivyo waendelee kupyaisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na kuendelea kutekeleza mapenzi ya Mungu hapa duniani, ili hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele!

Elimu Katoliki kwa ajili ya malezi fungamano katika kipindi cha miaka 150 ya uinjilishaji imedadavuliwa na Padre Charles Kitima, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye amesema kwamba, elimu na mchakato wa uinjilishaji ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa na kamwe haviwezi kutenganishwa. Familia ya Mungu nchini Tanzania haina budi kumshukuru Mungu kwa mchango mkubwa uliotolewa na Kanisa katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii katika kipindi cha miaka 150 iliyopita.

Huu ni wakati wa kusimamia na kuendeleza matunda ya uinjilishaji katika sekta ya elimu, kwa Kanisa kuendelea kuwekeza katika elimu bora zaidi, itakayowasaidia watanzania kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili kweli Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Huu ni wakati muafaka kwa Kanisa na Serikali kushikamana kwa dhati ili kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi katika sekta ya elimu kwani Kanisa ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini Tanzania!

Kuna uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki pamoja na dhamana ya Uinjilishaji wa kina inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Uinjilishaji nchini Tanzania. Ili kutambua umuhimu huu, kuna haja kwanza kwa walimu, walezi na wanafunzi wenyewe kufahamu changamoto inayoletwa na Kanisa kwa wakati huu! Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya vijana: kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa, ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho nchini Tanzania.

Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vimekuwa ni vituo vya majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kurithisha imani, maadili na utu wema. Kutokana na dhamana hii, vijana wanapaswa kuwa kweli ni wadau wa uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili. Jambo msingi kwa walimu, wazazi na walezi ni kutambua dhamana na utume wa shule za kikatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwajengea watoto na vijana msingi wa imani, maadili na utu wema.

Hapa ni mahali pa kujenga na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani, ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule za Kikristo waweze kuwa kweli ni wadau katika kuyatakatifuza malimwengu. Dunia inawahitaji vijana watakaotoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, shule na taasisi hizi ni vyombo makini vya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho!

Askofu Mkude
06 November 2018, 07:24