Tafuta

Vatican News
Mtakatifu Oscar Romero alikuwa mchungaji mwema, nabii na shuhuda wa huruma ya Mungu Mtakatifu Oscar Romero alikuwa mchungaji mwema, nabii na shuhuda wa huruma ya Mungu 

Mtakatifu Oscar Romero alikuwa mchungaji mwema, nabii na shuhuda wa huruma ya Mungu.

Mtakatifu Oscar Armulfo Romero sasa atangazwe kuwa ni “Mwalimu wa Kanisa” kutokana na ushuhuda wake kama mchungaji mwema na nabii, aliyejitahidi katika maisha na utume wake kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umefika wakati kwa Mama Kanisa kumtangaza Mtakatifu Oscar Armulfo Romero kuwa ni “Mwalimu wa Kanisa” kutokana na ushuhuda wake kama mchungaji mwema na nabii, aliyejitahidi katika maisha na utume wake kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni wakati pia kwa Kanisa mahalia kuanza mchakato wa kumtangaza Padre Rutilio Grande, Myesuit aliyeuwawa kunako mwaka 1977 huko El Salvador kutangazwa mtumishi wa Mungu, Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu kadiri ya mpango na huruma ya Mungu kwa waja wake.

Kama kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, familia ya Mungu kutoka El Salvador, imemwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchi yao kama njia ya kumuenzi Mtakatifu Oscar Romero kwa vitendo zaidi! Huu ni ushuhuda uliotolewa, Jumatatu, tarehe 15 Oktoba 2018 na Askofu mkuu Josè Luis Escobar Alas wa Jimbo kuu la Sal Salvador wakati alipokuwa anatoa hotuba ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na familia ya Mungu kutoka El Salvador.

Amesema, Askofu mkuu Oscar Romero aliuwawa kikatili na Kikosi cha mauaji nchini El Salvador, lakini katika maisha na utume wake, akajikita katika ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Mtakatifu Oscar Romero ni mwanga wa matumaini kwa wale wote wanaotembea katika uvuli wa giza na mauti; watu wanaotangatanga pasi na imani thabiti; na kwa wale ambao wametopea katika nyanyaso na ukosefu wa haki msingi za binadamu katika maisha yao. Hawa ndio wale ambao utu na heshima yao kama binadamu vinawekwa rehani.

Askofu mkuu Josè Luis Escobar Alas amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kanisa nchini El Salvador bado linaendelea kupambana na misukosuko mbali mbali, lakini daima limeendelea kuwa aminifu kwa Kristo Yesu na kwamba, linaendelea kusali kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa aendelee kutekeleza dhamana na utume wake kwa familia ya Mungu. Katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, Mababa wa Sinodi wamebahatika kuangalia ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa vijana wa El Salvador, waliokuwa wamekusanyika nchini mwao kwa ajili ya mkesha wa  Askofu mkuu Oscar Romero kutangazwa kuwa Mtakatifu.

Askofu mkuu San Salvador
16 October 2018, 14:51