Tafuta

Vatican News
Furaha ya kweli katika maisha inafumbatwa katika hekima ya Mungu! Furaha ya kweli katika maisha inafumbatwa katika hekima ya Mungu! 

Tafakari: hekima, hadhari ya mali na furaha ya kweli katika maisha.

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXVIII ni mwaliko kwa waamini kujichimbia katika Amri za Mungu, ili ziweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao. Kristo anaihamasisha familia ya Mungu kujibandua kutoka kwenye malimwengu, kama njia ya ushuhuda na ufuasi makini, tayari kutumia mali na utajiri kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Hek. 7:7-11) Somo letu la kwanza leo linaeleza sala ya mfalme Sulemani aliyomwomba Mungu na akasikilizwa.  Yeye kama mfalme wa Israeli hakujilinganisha na wafalme wa mataifa mengine waliokuwapo katika wakati wake, wafalme ambao mara nyingi walijifananisha na miungu au kujiita wana wa miungu. Yeye, tunaona katika sura nzima ya 7 ya kitabu cha Hekima, pamoja na kuwa ni mfalme anakiri kuwa ni mwanadamu sawa na watu wengine wote. Ni katika ubinadamu huo alisali akimwomba Mungu ajaliwe Hekima. Aliomba Hekima badala ya vito vya thamani, badala ya mali na utajiri, badala ya mamlaka makubwa na kuogopwa. Aliiomba kama nuru itakayomwangazia katika njia zake zote, na akiisha kuipata hiyo kwanza, alijaliwa mema yote ya jamii pamoja na mali.

Somo hili linaeleza umuhimu wa Hekima katika maisha ya mwanadamu. Linaonesha pia ukaribu na uhusiano kati ya Hekima na Mungu. Hekima kama elimu, ufahamu, maarifa na kadhalika kimsingi ni tunu ya kimungu. Inatoka kwa Mungu na inamsaidia mtu kuwa na mahusiano mazuri na Mungu na pia kuwa na mwono sahihi kuhusu maisha. Kwa maneno mengine elimu, ufahamu au maarifa yanayomweka kando Mungu si Hekima.

Somo la pili (Ebr. 4:12-13) Somo letu la pili kwa mistari michache tu linaeleza mambo mengi kuhusu Neno la Mungu: nguvu zake, sifa zake na kazi zake. Neno la Mungu ndilo Neno lililoumba na hivyo lina uwezo pia wa kuhukumu lilichokiumba (rej. Zab 51:6, Amos 1:2). Neno la Mungu ni kama jicho la Mungu. Linaona yote yaliyo moyoni mwa mtu.

Tunaona pia kuwa lugha iliyotumika kulipambanua Neno la Mungu hapa ni ile ile ambayo ilikuwa inatumiwa na Wayahudi kupambanua Hekima na Torati. Hekima kwa mfano, katika Hek. 7:24 inaelezwa pia kuwa ni nyepesi na huenda upesi kila upande. Kumbe kwa namna fulani Waraka kwa Waebrania, kama ilivyo pia katika sehemu kubwa ya Agano Jipya, Neno wa Mungu ambaye ni Kristo, anadokezwa kuwa ndiye anayewakilisha Hekima na pia Torati. Vyote viwili yaani Hekima na Torati vinanafsishwa kwa Kristo. Na kwa haki kabisa Kristo anatajwa kuwa ndiye Hekima yetu (1Kor. 1:30) na kuwa ndiyo ukamilifu wa Torati (Mt. 5:17-20).

Neno la Mungu linapambanuliwa hivi ili kutoa mwaliko wa kuliishi. Mwandishi wa waraka kwa Waebrania anawaalika watu kulipokea Neno la Mungu. Kanisa nalo katika liturujia linaendeleza mwaliko huo. Kila wakati Neno linapotangazwa mwisho hutolewa mwaliko wa kuliitikia kwa “Amina” kuonesha utayari wa kuliishi

Injili (Mk 10:17-30) Katika injili ya leo Yesu anakutana na kijana tajiri anayemuuliza “mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?” Yesu anamwambia azishike amri. Naye anajibu kuwa zote hizo amezishika tangu utoto. Yesu anamwangalia na anampenda. Ndiyo kusema kuwa hatilii shaka kile anachokisema kijana huyo na kuwa ni kweli amezishika amri hizo. Ndipo anamwambia kuwa amepungukiwa jambo moja, si mfuasi wa Yesu na ili kuwa mfuasi inabidi auze alivyonavyo, awape maskini na hapo atakuwa na hazina mbinguni. Kijana akaenda zake kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Ni jambo linaloweza kutushangaza kidogo. Iweje mtu anayezishika amri za Mungu ashindwe kupokea wito wa Mungu? Iweje mtu anayezishika amri za Mungu ashindwe kuwa mfuasi wa Yesu? Jibu analitoa Yesu mwenyewe juu ya kikwazo cha mali nyingi. Na anasema kuwa ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, swali linalofungua tafakari yetu ya leo ni hili: Je, utajiri ni dhambi? Utajiri haufai? Utajiri ni mbaya? Katika mwanga wa masomo yetu ya leo tunaona kuwa mahangaiko ya mwanadamu kwa vizazi na vizazi ni kutafuta furaha katika maisha, ni kutafuta kuepuka matatizo au uchungu maishani ili kuishi maisha mazuri na kuishi vizuri. Na kwa kweli mwanadamu ametafuta njia nyingi, vitu vingi na namna nyingi za kuifikia furaha katika maisha yake.

Kwa Wayahudi, pamoja na falsafa na fikra nyingi za mataifa yaliyowazunguka, wao waliona njia pekee ya kufikia furaha maishani ni kujifunza Hekima. Na wao hawakuona Hekima kuwa kama elimu au ufahamu tu bali waliiona kuwa hasa ni maadili, ni namna nzima ya kuishi kwa mwanadamu. Hekima ilionekana kama tunda au kilele cha matamanio ya kweli ya mtu. Vitu vingine vyote kama vile mali na elimu vinapaswa kumsaidia mtu kuifikia Hekima. Mtu asiye na hekima, asiye na maadili mema hawezi kuifikia furaha maishani hata kama ana elimu kubwa kiasi gani na hata kama ana mali nyingi kiasi gani. Na kwa imani yao, chanzo cha Hekima hiyo ni Mungu pekee na Hekima hiyo hukua katika mahusiano ya mtu na Mungu.

Kristo anathibitisha mafundisho hayo mema ya Wayahudi katika Agano la Kale na daima anaonya dhidi ya kishawishi kinachoambatana na mali. Mali ni pamoja na vitu vingine vizuri ambavyo Mungu alimkabidhi mwanadamu ili avitawale na ili vimsaidie mwanadamu kuishi kadiri ya mpango aliokusudia Mungu mwenyewe Muumba. Lakini katika mzunguko mzima wa mali: utafutaji, matumizi na umiliki mwanadamu amegeuka mtumwa wa mali na hata kufika hatua ya kuweka mali katika nafasi ya Mungu.

Katika kutafuta, utafutaji wa mali kumekuwapo na kishawishi cha kuitafuta kwa “gharama yoyote ile na kwa namna yoyote ile”. Kuanzia udanganyifu, ukandamizaji wa wengine na bila kujali kuhatarisha imani, wito na ubinadamu kwa ujumla. Katika matumizi mali imeambatana na kishawishi cha ufujaji; kukosa ukarimu kwa wasio nacho, matumizi mabaya ya vitu na kukosa kiasi. Katika kumiliki, mali imeambatana na kishawishi cha kusimama mbele ya nafsi ya mtu, kumjaza moyo wake si na utu bali na mali na kufikia hatua ya kuona  thamani ya utu kuwa ni kile alichonacho badala ya kuwa vile alivyo. Yesu anatambua hatari hii kubwa inayozunguka utajiri na mali. Hasemi kuwa mwenye utajiri hataingia mbinguni bali anasisitiza ugumu alionao ili kutualika kuwa macho daima katika mahusiano yetu na mali, kuwa na roho ya ufukara kila tunapotafuta, tunapotumia na kumiliki mali. Ni roho ya ufukara inayotusaidia kuweka uhusiano sahihi na tena ule anaoukusudia Mungu mwenyewe.

Tofauti na kijana tajiri aliyeondoka kwa huzuni alipoambiwa auze vyote alivyonavyo, Kanisa huwapokea vijana wengi hata leo ambao katika maisha ya utawa na upadre hujichukulia ahadi na nadhiri za kuishi kifukara kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Mwaliko wa Kristo leo uzidi kusaidia kueneza roho hii katika ulimwengu mzima wa leo. Na zaidi sana katika kundi hili maalumu roho hii izidi kujidhirisha katika maisha ili mitindo ya kiulimwengu ya utafutaji, matumizi na umiliki wa mali isififishe sura njema ya ahadi na nadhiri zao za ufukara bali wawe daima mwanga wa matumaini ya kuiishi furaha maishani bila kusongwa na utumwa wa mali.

Liturujia ya Neno la Mungu J 28 ya Mwaka B wa Kanisa

 

13 October 2018, 06:41