Tafuta

Vatican News
Bagamoyo ni mlango wa imani, matumaini na mshikamano katika mchakato mzima wa uinjilishaji Afrika Mashariki! Bagamoyo ni mlango wa imani, matumaini na mshikamano katika mchakato mzima wa uinjilishaji Afrika Mashariki!  (AFP or licensors)

Kardinali Pengo: Nguvu ya Msalaba, tunza na ulinzi wa B. Maria nyenzo msingi za uinjilishaji Tanzania

Kardinali Pengo amegusia historia ya chimbuko la Ukristo Tanzania Bara; umuhimu wa kuendelea kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na mazingira kwa njia ya elimu makini; mchakato wa kudumisha amani inayofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru na maendeleo endelevu na fungamani bila kusahau majadiliano ya kidini, kiekumene, kisiasa na kitamaduni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bagamoyo ni chemchemi ya imani na unaendelea kubaki kuwa ni Mlango wa Imani kwa Kanisa Katoliki Afrika  Mashariki. Hapa ni mahali ambapo Wamisionari wa kwanza walitua nanga ya: imani, matumaini na mapendo na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo Afrika Mashariki. Bagamoyo ni alama ya ukombozi, mahali ambapo mwanadamu amepata tena fursa ya kuinua moyo wake kwa imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu baada ya kukombolewa kutoka utumwani, kashfa ambayo inaendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam hivi karibuni alipata nafasi ya kuzungumzia kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara yanayoongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Furaha ya Injili. Amegusia historia ya chimbuko la Ukristo Tanzania Bara; umuhimu wa kuendelea kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na mazingira kwa njia ya elimu makini; mchakato wa kudumisha amani inayofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru na maendeleo endelevu na fungamani bila kusahau majadiliano ya kidini, kiekumene, kisiasa na kitamaduni, ili kweli Tanzania iendelee kuwa ni kisiwa cha amani kwa watu wake na jirani wanaowazunguka, kama sehemu ya matunda ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Kardinali Pengo anasema, “Dar es Salaam” maana yake ni “Dari – Salama” yaani “Nyumba salama” mahali ambapo Sultani wa Zanzibar alipenda kujipatia mapumziko baada ya shughuli zake kule Visiwani Zanzibar. Nyumba aliyoitimia kwa mapumziko hadi sasa iko kwenye Makao makuu ya Shirika la Wamisionari wa Afrika, “White Fathers” eneo la Posta ya zamani, Jijini Dar Esalaam. Ufafanuzi huu ni tofauti kidogo na kama ilivyozoeleka na wengi kwamba, Dar Es Salaam maana yake “Bandari Salama”.

Kardinali Pengo anakaza kusema, uhusiano kati ya Bara na Visiwani, ulisimikwa katika biashara ya utumwa na kwamba, Bagamoyo kilikuwa ni kituo cha mwisho kabla ya watumwa kusafirishwa kwenda sehemu mbali mbali. Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu “Spiritans” ambao pia wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uwepo wao nchini Tanzania waliamua kujiingiza katika biashara ya utumwa kwa kununua watumwa kutoka kwa Waarabu na hatimaye, kuwaweka huru. Watu waliokombolewa walirejeshewa utu na heshima yao kama binadamu; wakajengewa uwezo kwa njia ya elimu na ufundi; huduma ya afya na ustawi. Watumwa hawa wakamwongokea Mungu na kujaliwa kupata zawadi ya imani.

Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu waliendeleza mji wa Bagamoyo na hatimaye, kuitwa “Mji wa Mariam” maana yake mji wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa Wamisionari hawa wakashuhudia nguvu ya Msalaba waliousimika kwenye Pwani ya Bagamoyo! Kardinali Pengo anasema, Wamisionari hawa waliamini na kuthamini sana: nguvu, ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Bagamoyo ukawa Mlango wa Imani Afrika Mashariki. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 yaendelee kukoleza furaha ya Injili kwa familia ya Mungu nchini Tanzania!

Bagamoyo 150
20 October 2018, 13:51