Tafuta

Vatican News
Zimbabwe uchaguzi umepota, sasa ni mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Zimbabwe uchaguzi umepita, sasa ni mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.  (AFP or licensors)

Zimbabwe uchaguzi umepita, sasa ni upatanisho wa kitaifa!

Baraza la Makanisa Zimbabwe, ZCC., Hakuna sababu ya kuanzisha vita, vurugu na mipasuko ya kijamii, kwani tayari wananchi wa Zimbabwe wameteseka kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa demokrasia na utawala wa sheria; umaskini, magonjwa na hali ngumu ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makanisa nchini Zimbabwe, ZCC katika tamko lake, ambalo linaungwa mkono na Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, linaitaka familia ya Mungu nchini Zimbabwe kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa, sanjari na kujielekeza zaidi katika mchakato wa upatanisho kama nyenzo msingi ya kudumisha amani baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini humo. Hakuna sababu ya kuanzisha vita, vurugu na mipasuko ya kijamii, kwani tayari wananchi wa Zimbabwe wameteseka kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa demokrasia na utawala wa sheria; umaskini, magonjwa na hali ngumu ya maisha.

Pale ambapo wagombea uchaguzi wataona kwamba, haki haikutendeka, basi wafuate sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka badala ya kuwatumbukiza watu katika maafa makubwa ya vita isiyokuwa na kichwa wala miguu! Baraza la Makanisa nchini Zimbabwe linaipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kufanikisha uchaguzi huru jambo ambalo limeweka historia ya Zimbabwe katika kipindi cha miaka 37 ya utawala wa Rais Robert Mugabe. Rais Emmerson Mnangagwa wa Chama tawala cha ZANU-PF aliyeibuka kidedea katika uchaguzi huu dhidi ya mpinzani wake wa karibu Bwana Nelson Chamisa wa Chama cha Muungano wa MDC, wametakiwa kumaliza tofauti zao kwa njia ya sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Baraza la Makanisa nchini Zimbabwe limevitaka vyombo vya sheria kuwajibika barabara katika ulinzi wa raia na mali zao na kamwe visitumie nguvu kupita kiasi. Baada ya uchaguzi mkuu, wananchi wa Zimbabwe wanapaswa kusahau tofauti zao za kisiasa zilizowatenganisha na kuanza kuchuchumilia mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa, tayari kusonga mbele kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wachunguzi wa mambo wanasema, kwa sasa Zimbabwe imegawanyika kati ya wananchi wanaoishi vijijini na mijini; kuna pengo kubwa kati ya maskini na matajiri; changamoto zinazzohitaji majibu ya kinabii, ili kuweza kufikia muafaka, haki, amani na maridhiano nchini Zimbabwe.

 

06 August 2018, 14:30