Tafuta

Vatican News
Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya umoja, udugu, upendo na mshikamano wa dhati. Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya umoja, udugu, upendo na mshikamano wa dhati.  (Vatican Media)

Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya umoja, udugu na mshikamano

Mosi, Tasaufi ya Damu Takatifu inatusisitizia juu ya thamani kubwa ya uhai wa mwanadamu na heshima aliyonayo. Pili, Tasaufi hii inatusaidia kuishi kiini cha Ekaristi Takatifu yaani undugu, umoja na ushirika tunu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. - Vatican.

Ndugu msikilizaji, ninakukaribisha tena katika mwendelezo wa tafakari yetu juu ya tasaufi ya Damu Takatifu ya Kristo. Tasaufi ya Damu Takatifu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo ni msingi wa ukombozi wetu na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote. Pia tasaufi hii ina msingi wake katika na Neno la Mungu na katika Ekaristi Takatifu ambayo ndiyo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa na maisha ya Mkristo kwa jumla. (Rej Kifungu namba 1324 cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki). Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa imani yetu na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. (Rejea kifungu namba 1327 cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki).

Katika tafakari yetu iliyopita tuliangalia jinsi ambavyo tasaufi ya Damu Takatifu inavyoweza kutuongoza na kutujenga katika kuishi tunu mbalimbali za imani yetu kadiri ya mafundisho ya Injili. Tuliona na jinsi gani tasaufi hii inatusaidia kutambua ukuu wa huruma ya Mungu kwa wanadamu na jinsi gani twaweza kuitikia mwaliko wa Yesu wa kututaka tuwe wenye huruma kama jinsi Baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma.

Pia tuliona kuwa tasaufi hii inatupa changamoto ya kuwa na upendo usiobagua kama jinsi Mungu anavyowapenda wote bila ubaguzi na kama jinsi ambavyo Yesu mwenyewe alivyouishi upendo huo hapa duniani. Hatimaye tuliona kwamba tasaufi hii inatusaidia kumuiga Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa na mshikamano na wale wenye shida kama namna mojawapo ya kuliishi fumbo la umwilisho tukimuiga Yesu mwenyewe aliyekubali kujinyenyekeza akawa mwanadamu na akatutumikia.

Kutokana na upana na utajiri wa tasaufi hii, si rahisi kuziongelea tunu zote. Kila mmoja wetu anaalikwa kuendelea kutafakari zaidi juu ya Damu Takatifu ya Yesu ili kugundua tunu nyingine za kikristo zitokanazo na tasaufi hii. Leo tungependa kwa kifupi kuona ni jinsi gani tasaufi ya Damu Takatifu inavyotusaidia na kutujenga katika mitazamo sahihi kuhusu Mungu, maisha, wenzetu, na ulimwengu kwa jumla.

Mosi, Tasaufi ya Damu Takatifu inatusisitizia juu ya thamani kubwa ya uhai wa mwanadamu na heshima aliyonayo. Pili, Tasaufi hii inatusaidia kuishi kiini cha Ekaristi Takatifu yaani undugu, umoja na ushirika.

Ushirika, umoja na udugu ni tunu muhimu za Kanisa. Kwa namna ya pekee, sifa hizo ni muhimu kwa Kanisa letu la Afrika linalojitambulisha na kujitangaza kama, “Familia ya Mungu”.  Ili kuweza kuishi kama Familiya ya Mungu basi Kanisa zima la Afrika katika ngazi zake zote lazima liweze kuziishi tunu hizo muhimu. Kati ya matunda muhimu ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani ni kule kutambua kwamba Kanisa ni Ushirika au komunio. Hati zote za Mtaguso huu wa pili wa Vatican zina sifa hii kubwa kama wazo muhimu na mwelekeo wa maisha ya Kanisa. Ushirika au umoja ambao waumini wanaitwa kuuishi una kiini na chanzo chake katika maisha ya Utatu Mtakatifu wa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. (Rejea katika Hati ya Mtaguso wa Pili wa Vatican, Lumen Gentium au Mwanga wa Mataifa kifungu cha nne). Katika sala yake ya mwisho ya kikuhani, Yesu alituombea sote akisema, “wawe na umoja kama Sisi tulivyo wamoja” (Yoh 17:21).

Neno la Kiingereza, “communion” au kwa Kiswahili, “komunio” linatokana na neno la Kilatini “communio” lenye kumaanisha kuishi kwa ushirika na kushirikishana kwa pamoja. Neno hilohilo kwa lugha ya Kigiriki ni “koinonia” ambalo lina maana ya ushirika. Hii ilikuwa ni sifa mojawapo muhimu sana katika Kanisa la Mwanzo. Maandiko matakatifu yanatuambia kuwa jamii ya waamini wa kwanzawalikuwa mahali pamoja na kuwa na vitu vyote shirika. (Rejea Matendo 2: 44). Wale wanaomwamini Yesu Kristo wanapaswa waishi pamoja katika mshikamano, upendo na imani na wakiwa wameunganika katika lengo moja. Kila mmoja lazima ajitolee kwa ajili ya wengine, wanapaswa kuheshimiana, kupokeana na kutumikiana kwa upendo. (Rejea Matendo 2:42; Wafilipi 2: 1-2; Warumi 5: 13; 12: 16; 15: 7; 1 Petro 3:8). Zaidi ya hayo, Neno la Mungu linatuambia kuwa Wakristu wanapaswa kuwa wema, wenye huruma, wakarimu na wenye kushauriana na kupeana moyo. (Rejea Waefeso 4: 32; Wakolosai 3: 16; 1 Petro 4:9; 1 Watesalonike 5:11; Waebrania 3:13).

Ndugu mpendwa tukitaka kuyaishi hayo yote lazima tujifunze katika shule ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo maana Ekaristi huitwa “Komunio Takatifu”, inayowaunganisha wale wote wanaoshiriki Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ndiyo maana Mtakatifu Paulo anapowaandikia Wakorinto anawafundisha jambo hili akisema, “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je si ushirika katika Damu ya Kristo? Na Mkate tuumegao, je si ushirika katika Mwili wa Kristo?” (1 Wakorinto 10: 16).

Msingi wa umoja wa waamini hauko katika wao kama wao kukusanyika pamoja katika kuadhimisha ibada bali upo katika Yesu mwenyewe aliyesulibiwa na ambaye anawaita wote kuishi katika umoja wa wana wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kujenga jumuiya moja na familiya moja ya Mungu. (Rejea Yohana 11: 51-52). Kumbe tunaposema kwamba Kanisa ni Familiya ya Mungu, msingi wake ndiyo huo kwamba sisi sote mbali na tofauti zetu za rangi, utamaduni na utaifa ni wa familiya moja. Hiyo ndiyo imani yetu na hicho ndicho ambacho Neno la Mungu linatualika kuishi. Hati ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano Lumen Gentium, kifungu namba 7, inatusisitizia juu ya ushirika na umoja wa waamini wote wanaoshiriki Mwili na Damu ya Kristo katika Ekaristi ikisema kwamba Kanisa katika Kristo ni sacramenti ya muungano na Mungu na muungano na watu wengine wa makabila na utaifa tofauti.

Katika kuthibitisha hilo Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kutoa Damu yake ili kutuunganisha sote katika Ekaristi ili tuwe ndugu wa Familiya moja ya Mungu. Ni Damu ya Kristo ndiyo yenye kuvunja kuta zote za utengano baina yetu na kuwafanya watu wote kuwa wamoja. (Rejea Waefeso 2: 14). Ndiyo maana Baba Mtakatifu Mstaafu Benedicto XVI anasisitiza juu ya jambo hili akisema kuwa katika kushiriki Ekaristi Takatifu, waamini wanaingia katika mahusiano ya damu na wanakuwa ndugu kweli zaidi ya undugu wao wa asili. (Rejea Africae Munus, 152).

Katika tamaduni na mila zetu tumezoea kusema kwamba, “damu ni nzito kuliko maji.” Msemo huu una lengo la kudhihirisha kwamba undugu wa asili wa kuzaliwa ni muhimu zaidi kuliko mahusiano mengine yeyote. Madhara ya msemo huu kwa Kanisa letu la Afrika yamekuwa ni mengi. Wakati mwingine kumekuwa na mvutano katika jimbo fulani katika kuishi mchanganyiko wa waumini watokao katika makabila mbalimbali. Waumini na hata viongozi wa Kanisa wameshawishika kutoa upendeleo fulani au kwa ndungu wa familia moja, ukoo au kwa watu wa kabila lao. Inasikitisha pia kuona kwamba sehemu nyingine wamewakataa waziwazi baadhi ya viongozi wanaoteuliwa kuongoza makanisa mahalia mbali na sehemu zao za asili. Hii ni fedha kubwa kwa Kanisa, ni kinyume cha kile Bwana wetu Yesu Kristo anachotufundisha na kinyume cha kile ambacho Ekaristi Takatifu inatufundisha.

Msingi wa undugu wetu katika Kristo haukujengwa katika maji tu, yaani katika ubatizo, bali umejengwa katika Maji na katika Damu. Ili kuhakikisha kwamba Yesu alikuwa amekufa, askari mmojawapo alimchoma ubavuni kwa mkuki na mara ikatoka Damu na Maji. Mababa wa Kanisa wanatufundisha kwamba hapo ndipo zilipotoka Sakramenti za Ubatizo na Ekaristi Takatifu, maji kama ishara ya ubatizo na damu kama ishara ya Ekaristi Takatifu. Huu ndiyo hasa msingi unaomfanya Mkristo wa kweli na yule anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu kuwaona wote kuwa ndugu. Hayati Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuwa kweli shuhuda wa imani hii kimatendo na ndiyo maana alipinga kwa nguvu zote ubaguzi wa aina yeyote uwe wa ma kabila, dini au rangi. Kwa Mkristo wa kweli fundisho hili lazima likae moyoni mwake na kumwongoza katika mahusiano na watu wengine. Wewe na mimi basi tunaalikwa kuishuhudia imani yetu tukiongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu.

Kumbe basi, tasaufi ya Damu Takatifu ni msaada wa kutuongoza na kutukumbusha juu ya mitazamo yetu sahihi kama wakristu na juu ya wajibu wetu kwa wenzetu na kwa kwa dunia nzima. Ninakualika basi ili nawe uweze kuchota kutoka tasaufi hii nguvu ya kumtumikia Mungu na kuwatumikia wengine kwa kutoa ushuhuda wa imani kwa maneno na kwa matendo.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

07 August 2018, 11:25