Cerca

Vatican News
Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo ni dira na mwongozo wa maisha ya Mkrisro! Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo ni dira na mwongozo wa maisha ya Mkristo!  (AFP or licensors)

Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo ni dira na mwongozo wa maisha ya Mkristo!

Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu ni dira na mwongozo wa maisha ya Mkristo na kwamba inajengwa katika mahusiano na mafungamano kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake. Tasaufi kimsingi inapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kanisa, Liturujia, Mafundisho, Ushuhuda na katika Sakramenti za Kanisa.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. - Vatican.

Ndugu msikilizaji nakukaribisha katika tafakari ya tasaufi ya Damu Takatifu. Tuko katika mwezi wa saba, mwezi ambao Mama Kanisa ameutenga maalumu kwa ajili ya kutafakari na kuitukuza kwa namna ya pekee Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu, Damu ya ukombozi na upatanisho. Katika tafakari iliyopita tulisema kuwa tasaufi ni ujumla wa mambo yanayohuisha na kuongoza maisha ya mtu au kikundi cha watu; ni mambo yahusuyo imani, mitazamo na matendo maalumu. Katika mazingira ya Kikristu tunaweza kusema kwamba tasaufi ni mtindo wa maisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Katika Kanisa kuna tasaufi mbalimbali ambazo ni zawadi zitokazo kwa Roho Mtakatifu. Ikumbukwe daima kuwa kiini cha tasaufi yeyote ya Kikristo ni Yesu mwenyewe: yaani mafundisho na mfano halisi wa maisha yake. Kila tasaufi hujaribu kuyaishi mafundisho ya Yesu katika matendo na maisha ya kila siku. Tasaufi huongoza maisha ya mtu au kikundi cha watu katika mahusiano na Mungu, mahusiano na watu wengine, na ulimwengu kwa jumla.

Tasaufi yeyote haiwezi kuwa tasaufi ya kweli kama haina uhusiano na maisha halisi. Ikijengwa katika misingi ya Neno la Mungu, Mapokeo ya Kanisa, Mang’amuzi na mafundisho ya watakatifu mbalimbali katika historia ya Kanisa, Liturjia na hasa Ekaristi Takatifu, tasaufi ya Damu Takatifu inatusaidia kuishi katika imani thabiti ya Kikristu na inatujenga katika mitazamo sahihi ya Kikristu kadiri ya mafundisho ya Yesu mwenyewe. Leo hii tutaongelea tunu au fadhila tatu zitokanazo na tafakari ya mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote. Tunu hizi ni muhimu kwa Mkristu anayeongozwa na tasaufi ya Damu Takatifu kama njia ya kumuiga Kristu na kufanana naye

Huruma: Katika mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote tunapata kutambua Huruma ya Mungu kwa wakosefu. Hiki ndicho anachotuambia Mtakatifu Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Timoteo sura ya pili aya ya nne akisema kwamba Mungu anataka watu wote waokolewe na wapate kujua yaliyo kweli. Naye nabii Ezekieli katika Agano la Kale anatudhihirishia juu ya mpango na nia hiyo hiyo ya Mungu pale anaposema kwamba Mungu hafurahii kifo cha mtu mwovu bali aiache njia yake mbaya ili apate kuishi. (Rejea Ezekieli 18: 21, 23, 32).

Ndugu yangu kadiri tunapotafakari kwa kina Huruma na Upendo wa Mungu kwa wakosefu na wenye dhambi ndivyo tunavyogundua haja ya kubadili mitazamo yetu ya kibinadamu juu ya wengine na hasa wakosefu na wenye dhambi. Siku moja nilipata kuongea na mama mmoja ambaye ni Mkristo mzuri lakini alipata shida kidogo kuuelewa msimamo wa Baba Mtakatifu Francisko pale ambapo aliposita kuwahukumu moja kwa moja watu wanaojihusisha na mahusiano ya jinsia moja. Si mama huyu peke yake bali ni wengi ambao kwa msimamo huu wa Baba Mtakatifu wanajisikia kukwazwa naye. Wengi wanajiuliza ni kwa kwanini anawakaribisha Vatican, makao makuu ya Kanisa Katoliki, “waovu” hasa viongozi wa nchi mbalimbali ambao maisha yao hayatoi mfano mzuri kwa jamii. Hata hivyo, ukweli ni kwamba Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote mambo yote yanayoenda kinyume na maadili ya Injili na mafundisho ya Kanisa. Ni changamoto hii hii aliyoipata Bwana wetu Yesu Kristu katika maisha na utume wake hapa duniani. Mwinjili Matayo katika Injili yake sura ya tisa, aya ya kumi hadi ya 13, anatusimulia jinsi Yesu mwenyewe alivyolaumiwa kwa kuwapokea wenye dhambi, kukubali kukaa na kula pamoja nao.

Ndugu yangu, bila kuufahamu Moyo wa Mungu uliojaa huruma na Mapendo kwa wote hasa wenye dhambi, hatuwezi kumwelewa Yesu katika mafundisho na maisha yake kwa jumla. Kadharika hatuwezi kumwelewa Baba Mtakatifu anayesita kuwahukumu wenye dhambi japo hakubaliani kabisa na matendo yao yasiyofaa. Bwana wetu Yesu Kristu anatualika kuwa na mtazamo wa kutowahukumu wengine anaposema, “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa, msilaumu, nanyi hamtalaumiwa, achilieni nanyi mtaachiliwa.” (Luka 6:37).

Ndugu yangu, pengine wewe na mimi tumekuwa na tabia ya kuwahukumu wengine bila hata kujali mwaliko huu wa Yesu. Japokuwa tumesoma mara nyingi Biblia Takatifu bado hatujaitambua vema Huruma ya Mungu. Ili kutusaidia kuielewa Huruma ya Mungu, katika maisha na utume wake hapa duniani, Yesu hakupenda kuhukumu. Mfano mmojawapo ni pale ambapo Mafarisayo na Wanafiki walipotaka kumuua kwa kumpiga mawe yule mwanamke aliyekutwa na hatia ya kuzini. Baada ya kuongea na dhamira zao, wahuni hao walitoweka kwa kukimbia, mmoja baada ya mwingine. Alipobaki yeye pamoja na yule Dada, akamwambia, hata mimi sikuhukumu, nenda lakini kuanzia sasa usitende dhambi tena. (Rejea Yoh 8:10-11).

Hatuwezi kutenganisha tasaufi ya Damu Takatifu na Huruma ya Mungu. Ndiyo maana moja ya litania za Damu Azizi ya Kristu inasema, “Damu ya Kristo Mto wa Rehema...”. Miaka miwili iliyopita tulikuwa tukisherehekea Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Picha halisi iliyokuwa ikitusindikiza katika tafakari ya mwaka huo wa Jubilei ni ule mfano wa Mwana mpotevu akiwa amebebwa mabegani na Baba. Alipokuwa akiufunga Mwaka wa Jubilei wa Huruma ya Mungu, tarehe 20 Novemba, 2016, Baba Mtakatifu Fransisko alisema kuwa japo Mlango Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu ulikuwa ukifungwa, mlango halisi wa Huruma, ambao ni mlango wa Moyo wa Yesu unabaki wazi.

Tunapokubali kuongozwa na tasaufi ya Damu ya Kristo, lazima tukubali kufanana na Mungu katika Huruma yake. Ndiyo maana Yesu hachoki kutualika akisema, “Basi iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.” (Lk 6: 36). Basi wewe na mimi leo tujiulize ni namna gani tunaitikia wito huu wa kuwa na huruma katika familiya zetu, jumuiya zetu na katika Kanisa na katika jamii kwa jumla. Kristu mwenyewe anatra tufanane naye kwa kuwasaidia wengine hasa wanaotukosea kukutana na Huruma ya Mungu ili waweze kubadili maisha na mitazamo yao.

Basi ninakualika ndugu yangu tuchukue nafasi ili kuitafiti mioyo yetu na kuona kama kweli tasaufi hii ya Damu Takatifu inaongoza maisha yetu, mahusiano yetu, mitazamo yetu na katika mambo tunayoyachagua. Tasaufi ya Damu Takatifu ni tasaufi inayopaswa kuongoza maisha ya kila Mkristo, awe mtawa, padre, au mlei maana tasaufi hii imejengwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuishi fadhila zitokanazo na tasaufi hii ili iwe njia kwetu ya kushuhudia imani yetu kwa maneno na matendo.

Sikiliza

 

21 July 2018, 16:15