Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anatarajiwa kutoka Daraja takatifu ya Upadre kwa Shemasi Richard Joseph Masanja, tarehe 26 Julai 2018 Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Richard Joseph Masanja, tarehe 26 Julai 2018  (Vatican Media)

Askofu mkuu Paul Ruzoka kutoa Daraja ya Upadre kwa Shemasi Richard Joseph Masanja

Wakleri wana dhamana na utume wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hii ni changamoto ya kuendelea kutoa ushuhuda wenye mvuto katika maisha na utume wa Kanisa. Wito, maisha na utume wa Kipadre upewe kipaumbele cha kwanza: kwa kujipyaisha kwa Neno la Mungu, maisha ya Sala, kufunga na matendo ya huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Mwenyeheri Paulo VI, katika Waraka wake kwa Mapadre, miaka 50 iliyopita anasema, anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na Wakleri wote, waliokabidhiwa dhamana na utume wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hii ni changamoto ya kuendelea kutoa ushuhuda wenye mvuto katika maisha na utume wa Kanisa. Wito, maisha na utume wa Kipadre upewe kipaumbele cha kwanza. Huu ni wosia wa kibaba unaotolewa kwa moyo mnyofu, katika ukweli na uwazi na kwamba, hii ni changamoto kwa Wakleri kuweza kuupokea wosia huu na kuufanyia kazi katika maisha na utume wao!

Waamini wanathamini maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu na hatimaye, kumwilishwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Neno la Mungu linafafanua na kukazia zaidi kwamba, Mwenyezi Mungu anafahamu fika mambo yao yote, anajua bidii yao, uvumilivu kwa watu waovu na watenda dhambi na kwamba, wamewapima wale wanaojidai kuwa mitume na kumbe si mali kitu!

Mwenyeheri Paulo VI anawashukuru na kuwapongeza wakleri wenye saburi, wenye uwezo wa kuvumilia taabu na mateso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake pasi na kuvunjika moyo! Lakini, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Wakleri wanapyaisha kila siku ya maisha yao ule upendo waliokuwa nao siku ile ya kwanza, walipoitwa na kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao! Wakleri watambue kwamba, wao ni watumishi wa Kristo, waliokabidhiwa siri za Mungu na kwamba, wanatakiwa kuwa waaminifu na watu wenye dhamiri nyofu bila mawaa mbele ya Mungu na jirani zao.

Wakleri ni waalimu wa mambo matakatifu, wagawaji wa mafumbo ya Mungu na marafiki wa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu. Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, wasaidiane, wataabikiane na kushikamana, ili kuweza kuyapatia matatizo na changamoto hizi ufumbuzi wa kudumu katika mwanga wa Injili. Mwenyeheri Paulo VI anasema, alitaka kuwashirikisha haya mambo mazito yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake, ili wakleri watambue kwamba, Kanisa linawathamini na kujali mchango wao katika mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Mapadre wajitahidi kadiri wanavyoweza kuwa na umoja na mshikamano kamili na Maaskofu wao, ili waweze kupata amani, utulivu wa ndani na nguvu ya kutangaza na kushudia furaha ya Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.

Huu ndio ushauri ambao Vatican News inapenda kuwapatia Mapadre wapya waliowekwa wakfu nchini Tanzania kama matunda ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki, Tanzania Bara na kwa sasa kilele chake ni Mwezi Novemba 2018 badala ya Mwezi Oktoba kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali. Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, tarehe 26 Julai 2018 anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Richard Joseph Masanja, IC. Kutoka katika Shirika la Mapendo, maarufu kama Warosminiani. Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Yosefu, Parokia ya Ndala, Jimbo kuu la Tabora. Tarehe 27 Julai 2018 Padre Richard Joseph Masanja anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa ya Shukrani, kwenye Kigango cha Igoko, Parokia ya Ndala, Jimbo kuu la Tabora.

Ifuatayo ni historia fupi ya maisha na wito wake: Mimi naitwa Frt.  Richard Joseph Masanja wa Shirika la Mapendo (Institute of Charity I.C au Rosminians).  Ni mzaliwa wa Kigango cha Igoko, Parokia ya Ndala Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, nchini Tanzania. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto sita. Msichana mmoja na wavulana watano. Nilisoma katika Shule ya Msingi Igoko baadaye nikaenda Shule ya Sekondari Kazima iliyopo katika Manispaa ya Tabora. Baada ya masomo ya kidato cha nne nilikwenda kufanya kozi ya ualimu kwa ngazi ya Astashahda katika Chuo cha Ualimu Mpwapwa na kidato cha Sita. Baadaye nilijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora kwa ngazi ya Stashahda ya Elimu katika masomo ya Jiografia na Kiswahili. Baada ya kufanya kazi kidogo nilijiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino tawi la Mwanza (SAUT) kwa ngazi ya Shahada katika masomo ya Jiografia na Kiswahili.

Nikiwa Chuoni Mwanza nilivutiwa sana na wahadhiri wangu hasa Mapadre wa Shirika la Yesu (Jesuit Fathers) walivyokuwa wana Niliipenda sana kazi ya ualimu tangu nikiwa mtoto mdogo. Kwa hiyo nilipokutana na Mapadre hawa hamasa yangu iliongezeka zaidi ya kutaka kuwa Padre na Mhadhiri wa Chuo Kikuu.  Hivyo nikiwa SAUT, nikaamua kuulizia taratibu za mimi kujiunga na Shirika hilo la Yesu (Jesuits Fathers). Nilipewa kitabu kidogo kilichokuwa na anwani mbalimbali za wakurugenzi wa miito katika mashirika mbalimbali ya kitawa na kazi za kitume. Mojawapo lilikuwa ni Shirika la Mapendo (Rosminians) na Shirika la Yesu(Jesuit Fathers). Niliandika barua mbili moja kwa Rosminians na nyingine kwa Shirika la Yesu. Nilipata barua kutoka Shirika la Mapendo wakati niko mwaka wa pili naelekea kuingia mwaka wa tatu, Chuo Kikuu cha SAUT.

Baada ya kupata barua hiyo sikuwa na mpango tena wa kujiunga na Shirika la Yesu. Hivyo nilipomaliza masomo yangu ya Shahada mwaka 2010 nikawasiliana na Mkurugenzi wa Miito wa Shirika la Mapendo na kuniambia kuwa nijiandae kuanza malezi ya awali. Niliwaeleza wazazi wangu wote wawili nia yangu ya kujiunga na maisha ya utawa. Namshukuru Mungu wazazi wote walikubali ombi langu kwa kauli moja. Na hiyo ndiyo ikawa mwanzo wa safari yangu ya wito katika Shirika hili la Mapendo. Nilianza taratibu za malezi ya awali kwa ngazi ya Upostulanti mwishoni mwa mwaka 2011 kwa miezi michache, kisha  mnamo mwaka 2012 nikapokelewa kuanza rasmi hatua ya Unovisi.

Unovisi ni kipindi cha miaka miwili. Hivyo nilimaliza na kufunga nadhiri zangu za kwanza mnamo mwaka 2014. Mara baada ya nadhiri za kwanza nilitumwa kuja Roma katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Beda (Pontifico Beda College) kilichopo karibu na Kanisa la Mtakatifu Paulo. Nilifunga nadhiri zangu za daima mwishoni mwa mwaka 2017. Kwa neema na uwezo wa Mwenyezi Mungu nikapewa  Daraja la Ushemasi wa Mpito, hapo tarehe 27 Januari 2018 na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya. Mungu ni mwema kila wakati.

Sikiliza

 

25 July 2018, 09:19