Tafuta

Vatican News
Mkutano wa 19 wa AMECEA, mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, 2018 Mkutano wa 19 wa AMECEA, mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, 2018 

AMECEA: Watu hata katika tofauti zao msingi wanaweza kushikamana na kushirikiana kwa dhati!

Mababa wa AMECEA wanasema, Mwenyezi Mungu ndiye kiini cha tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu! Lakini, pia ndiye kiungo muhimu cha tofauti hizi katika maisha ya binadamu, ili kusaidiana, kushirikiana, kushikamana na kukamilishana katika Mungu ambaye ni Muumbaji na Kristo Yesu ambaye ni Mkombozi wa walimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Hili ni tukio la furaha na kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewakutanisha Mababa wa AMECEA ili: kusali, kutafakari na kuibua mbinu mkakati utakaoliwezesha Kanisa Afrika Mashariki kupambana na changamoto za tofauti ili kujenga na kudumisha usawa, umoja na udugu unaofumbatwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Ni wakati wa kuendelea kuboresha sera, mikakati na mafanikio yaliyokwisha kupatikana tangu AMECEA ianzishwe. Askofu Joseph Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Vatican News amesema kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA, imewasaidia sana Mababa wa AMECEA kutafakari na kupembua tofauti, umoja na changamoto zilizopo kati yao, kwa kutambua kwamba, tofauti hizi zinaimarishwa kwa kujikita katika umoja uliopo kati yao kwa njia ya Kristo Yesu pamoja na kuendelea kumtegemea Mwenyezi Mungu ambaye ndiye asili ya utajiri wa tofauti hizi, ili kutegemeana, kushirikishana na kukamilishana katika mambo mema na matakatifu.

Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiini cha umoja na mshikamano wao. Tofauti hizi pia ni utajiri mkubwa katika: Imani, maisha na utume wa Kanisa kama ilivyojidhihirisha hata katika Liturujia ya Ibada ya Misa Takatifu katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa AMECEA. Wote wanaunganishwa na Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumbaji na Kristo Yesu, ambaye ni Mkombozi wa dunia na Roho Mtakatifu anayewatakatifuza, ili waendelee kushikamana katika imani, matumaini na mapendo, hata katika tofauti zao msingi.

Hii ni changamoto ya kujikita zaidi katika mambo yanayowaunganisha zaidi, kuliko kuendekeza yale yanayowagawa na kuwasambaratisha kama familia ya Mungu Afrika Mashariki na kati. Tofauti hizi zinajikita katika lugha, mila, tamaduni na namna ya kufikiri na kutenda. Mababa wa AMECEA wanamshukuru Mungu kwa Ethiopia na Eritrea kutiliana sahihi mkataba wa amani na maridhiano hapo tarehe 17 Julai 2018 na hivyo kukata mzizi wa vita, utengano na tabia yakulipizana kisasi ambayo imedumu takribani miaka 20 kati ya nchi hizi mbili ambazo zilikuwa zimeungana na kutengana rasmi kunako mwaka 1991 na huo ukawa ni mwanzo wa chuki na uhasama kati ya Serikali za pande hizi mbili.

Askofu Joseph Roman Mlola anakaza kusema katika imani, haya ni majibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ile sala ya familia ya Mungu katika nchi za AMECEA iliyokuwa ikiombea haki, amani na maridhiano kati ya watu. Watu walikuwa na kiu ya kuona umoja, upendo na mshikamano vinatawala kwa kuvuka tofauti za mipaka ambayo iliwekwa na wakoloni kwa mafao ya nchi zao; mipaka ambayo pengine inatokana na itikadi za kisiasa na kidini, lakini bado kwa njia ya neema, watu wa Mungu wanaweza kuungana na kufurahia umoja katika haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hii ndiyo changamoto pia iliyotolewa na Kardinali Berhaneyesus Souraphiel, Mwenyekiti wa AMECEA wakati wa Ibada ya kufungua Mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA, huko Addis Ababa, Ethiopia.

Kwa upande wake, Padre Stephen Mbugua Ngari, Makamu wa Chuo Kikuu cha Tangaza, Kenya amesikika akisema kwamba, tofauti msingi katika nchi nyingi za AMECEA zimesababisha majanga na maafa makubwa, kiasi cha watu kushindwa kutumia utajiri na rasilimali zilizopo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ubaguzi unaosimikwa katika ukabila, udini, utaifa, rangi, itikadi na jinsia umeendelea kuwapekenyua wananchi wa Afrika Mashariki na Kati.

Umefika wakati kwa familia ya Mungu Ukanda wa AMECEA kujisikia kuwa ni wamoja na kwamba, tofauti zao msingi ni utajiri unaopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe kisiwe ni chanzo cha maafa na utengano. Ni matumaini yake kwamba, AMECEA itaweza kufanya utafiti wa kina na kuangalia sababu msingi zinazopelekea tofauti mbali mbali katika eneo hili kuwa ni chanzo cha maafa na mipasuko ya kijamii. Kuwepo na mchakato utakaowawezesha wananchi wa AMECEA kushirikiana kwa dhati ili kujenga mafungamano na maelewano zaidi, kuliko ilivyo kwa sasa kwa Maaskofu kukutana mara chache kwa mwaka wakati wa mikutano yao mikuu!

Ukabila, uchu wa mali na madaraka vimekuwa ni chanzo kikuu cha vita na kinzani Sudan ya Kusini na katika baadhi ya Nchi za AMECEA. Watu wamechoka na vita wanataka kuona haki, amani na maridhiano vikitawala kati yao! Tangu mwaka 2013 vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipowaka moto, kumekuwepo na mikataba ya mara kwa mara, lakini yote hii, haijafua dafu, ili kuwapatia wananchi wa Sudan ya Kusini amani ya kudumu. Ikumbukwe kwamba, amani inafumbatwa katika misingi ya: Ukweli, haki, upendo na uhuru kama anavyobainishwa Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa kunako mwaka 1964. Amani ni mchakato wa maisha unaohitaji majadiliano katika ukweli na uwazi; sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Sikiliza

 

21 July 2018, 16:03