Katekesi Kuhusu Mt. Yosefu: Baba Mwenye Huruma Na Mapendo

Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa haki iliyomwilishwa katika malezi, makuzi na elimu kwa mtoto Yesu, akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. Rej. Lk 2:52. Hivi ndivyo alivyofanya Mwenyezi Mungu kwa Israeli, akamfundisha kutembea, huku akiwa amemshika mkono na kumwonesha upendo na kumlisha. Rej. Hos 11: 3-4.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu ambaye kimsingi ni msaada, faraja na msimamizi. Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu: Mtakatifu Yosefu na mazingira alimoishi kadiri ya Maandiko Matakatifu; mjini Bethlehemu mahali alipozaliwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Unabii. Nazareth ni mahali alipokulia Yesu. Hii ni miji miwili yenye uhusiano wa karibu sana na maisha ya Mtakatifu Yosefu. Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inaelezea kuhusu Ukoo wa Kristo Yesu: 1: 12-16. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inamwonesha Mtakatifu Yosefu katika historia ya wokovu. Wainjili wote wanamtambua Yosefu kuwa ni Baba Mlishi wa Kristo Yesu, aliyekuja hapa ulimwenguni kutimiza historia ya Agano Jipya na la milele na kwamba, historia ya wokovu inayojenga mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kwa Mwinjili Mathayo, historia ya wokovu inapata chimbuko lake kwa Abrahamu, lakini Mwinjili Luka anakwenda mbali zaidi hadi kufikia asili ya mwanadamu yaani Adamu.

Mwinjili Mathayo anawasaidia waamini kumwelewa Mtakatifu Yosefu, katika hali ya ukimya bila makuu, lakini, kiungo muhimu sana katika historia ya wokovu na moyo wa sala. Kimsingi, Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu amekwisha kugusia mazingira alimoishi Mtakatifu Yosefu; Wajibu na dhamana yake katika historia ukombozi. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa haki na mchumba wake Bikira Maria. Alikuwa ni mtu mkiya sana, aliyejitahidi kujifunza kwa kusikiliza na hivyo kumwachia Neno wa Mungu nafasi ya kuendelea kukua na kukomaa. Huu ni ukimya uliogeuzwa na kumwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu alizaliwa katika mazingira duni na maskini na kwamba, unyenyekevu ndiyo njia inayowapeleka waamini kwa Mungu Baba wa mbinguni. Mtakatifu Yosefu alijisadaka sana ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Akalazimika kukimbilia nchini Misri na kukaa huko kama mkimbizi, kashfa inayoendelea kujitokeza hata katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yosefu alidhulumiwa, lakini alionesha ujasiri mkubwa kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Baba Mlishi wa Yesu. Mwinjili Mathayo anamwelezea Mtakatifu Yosefu kwamba, alikuwa mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo. Mt. 1:16. Mwinjili Luka kwa upande wake anakazia kwamba, Kristo Yesu alipelekwa Hekaluni “kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana” Lk 3:23. Kumbe, Wainjili wanakazia dhamana na nafasi ya Mtakatifu Yosefu kama Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Katika Mapokeo ya Kale, jina la mtu lilikuwa ni muhtsari wa mtu. Kumbe, mtu kubadilisha jina, kulimaanisha mabadiliko katika mtu huyo. Tangu mwanzo, Mtakatifu Yosefu alipashwa habari kuhusu Bikira Maria na kuzaliwa kwa Mtoto ambaye ataitwa Yesu. Jina la Yesu maana yake ni Mungu anaokoa. Yeye ndiye atakaye waokoa watu na dhambi zao. Rej. Mt 1: 21. Mtakatifu Yosefu anaonesha kwamba, kitendo cha kuasili watoto ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa kibaba na kimama.

Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake Jumatano tarehe 19 Januari 2022 amemtaja Mtakatifu Yosefu kuwa ni Baba Mwenye Huruma, shuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; aliyejitaabiisha katika malezi, makuzi na elimu kwa Mtoto Yesu. Nabii Hosea akizungumzia kuhusu upendo wa kibaba anasema, Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda nikamwita mwanangu atoke Misri. Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya. Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao. Rej. Hos 11: 1, 3-4. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua akisema, Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa haki iliyomwilishwa katika malezi, makuzi na elimu kwa mtoto Yesu, akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. Rej. Lk 2:52. Hivi ndivyo alivyofanya Mwenyezi Mungu kwa Israeli, akamfundisha kutembea, huku akiwa amemshika mkono na kumwonesha upendo na kumlisha. Rej. Hos 11: 3-4.

Wainjili wanamwonesha Kristo Yesu katika mahubiri yake akitumia neno “Baba” alipokuwa anamzungumzia Mungu Mwenyezi na upendo wake mkuu na wa milele. Mifano yake mingi inamweka Mwenyezi Mungu kuwa ndiye mhusika mkuu. Mfano wa Baba Mwenye Huruma, maarufu kama sehemu ya “Injili ya Mwana Mpotevu.” Rej. Lk 15: 11-32 inakazia kuhusu dhambi, upendo na huruma ya Baba wa milele, iliyomsukuma Baba kutoka mbio kwenda kumlaki “Mwana mpotevu” alipokuwa anarejea nyumbani, akamwona kwa mbali na kumwonea huruma, akamwendea mbio, akamwangukia shingoni na kumbusu sana. Kwa upande wake, Mwana mpotevu alitegemea kupata adhabu kali kama sehemu ya utekelezaji wa haki na badala yake akaonjeshwa huruma na upendo.

Waamini wakumbuke daima kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hashangazwi na dhambi, makosa pamoja na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini anashangazwa na kusikitishwa zaidi na tabia ya watu kujifungia katika nyoyo zao, kukosa imani na upendo kwake. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo. Hii ndiyo kazi kubwa iliyotekelezwa na Mtakatifu Yosefu katika malezi na makuzi ya Mtoto Yesu. Kimsingi, mambo ya Kimungu yanawafikia waamini kwa njia ya uzoefu na mang’amuzi ya kibinadamu. Jambo la msingi kwa kina mwamini ni kutafakari kutoka katika undani wa maisha yake, ili kuangalia ikiwa kama ameonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake na hivyo kugeuka kuwa ni mashuhuda wa tunu hizi msingi katika maisha ya Kikristo. Hili si tatizo la hisia bali ni mang’amuzi kutoka katika undani wa mtu aliyeonja kwamba, anapendwa na kupokelewa jinsi alivyo katika udhaifu wake wa kibinadamu na hivyo kutoa nafasi kwa upendo wa Mungu kuweza kuleta mabadiliko nyanya katika maisha.

Mwenyezi Mungu anamwamini mwanadamu si tu katika karama na mapaji aliyomkirimia bali pia hata katika udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa katika Waraka wake wa Pili kwa Wakorintho anapozungumzia kuhusu maono na mafunuo anagusia mwiba ulioko mwilini mwake, ili asijivune kupita kiasi, akasali na kumsihi Bwana mara tatu, ili kimtoke lakini, Mwenyezi Mungu akamjibu na kumhakikishia kwamba Neema yake inatosha kwa maana uweza wa Mungu hutimilika katika udhaifu. Rej. 2 Kor 12: 7-9. Mwenyezi Mungu anamwezesha mwamini kutembea na udhaifu wake kama kielelezo cha huruma na upendo wake wa daima.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukimbilia huruma ya Mungu hasa katika Sakramenti ya Upatanisho na katika maisha ya sala binafsi kwa kufanya uzoefu na mang’amuzi ya ukweli na huruma yake. Shetani, Ibilisi anapenda kuwatumbukiza watu katika uwongo, ili awasute. Kinyume chake, Mwenyezi Mungu anawaongoza na kuwasaidia watu kutembea katika mwanga wa ukweli, ili kuwakomboa. Huu ni ukweli, unaowapokea na kuwakumbutia; unaowainua na kuwasamehe. Kamwe waamini wasichoke kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Mtoto Yesu ni kielelezo cha Ubaba wa Mungu anayependa upendo kwa kusamehe na kusahau. Huu ni mwaliko kwa waamini kumpatia Mungu nafasi ili aweze kuwaonesha upendo na msamaha, tayari hata wao kugeuka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, ili kuamka tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Baba Mtakatifu amehitimisha Katekesi kwa sala kwa ajili ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mwenye Huruma, akimwomba, ili aweze kuwafunda waamini kukubali na kutambua kwamba, wanapendwa jinsi walivyo hata katika udhaifu wao. Awasaidie watu wa Mungu ili wasiweke vikwazo kuhusu udhaifu wao mbele ya ukuu wa huruma na upendo wa Mungu. Mwenyezi Mungu apende kuamsha ndani mwao ile hamu ya kukimbilia Kiti cha huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kupata msamaha na maondoleo ya dhambi; ili kupendwa na kuoneshwa huruma. Binadamu katika udhaifu wao, wapende na kuoneshwa huruma. Mwenyezi Mungu awe karibu na watu wote waliotenda makosa na kwa sasa wanatumikia adhabu zao. Mwenyezi Mungu apende kuwasaidia kupata haki na huruma, ili waweze kuanza kutembea tena. Jambo la kwanza wajisikie kusamehewa, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu.

Mt. Yosefu: Huruma

 

19 January 2022, 16:08

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >