Mkutano wa Kimataifa wa Imani:Mahitaji ya watu wa asili yanasikilizwa zaidi
Na Francesca Merlo na Christopher Wells - Abu Dhabi.
Bibi Mona Polacca, kiongozi wa watu Asilia kutoka Kabila la Kihindi huko Mto wa Colorado, alizungumza Jumatatu tarehe 6 Novemba kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Imani uliofanyika tarehe 6-7 Novemba 2023 huko Abu Dhabi Nchi za Falme za Kiarabu kabla Kilele cha Mkutano wa COP28, mwezi ujao akishiriki mawazo yake juu ya uhusiano mtakatifu kati ya ubinadamu na mazingira. Kufuatia na hotuba yake, Bibi Mona alizungumza na Christopher Wells, Mwandishi wa Radio Vatican, Vatican News, akisisitiza haja ya haraka ya viongozi wa kidini na jumuiya duniani kote kuungana katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Na asili, kama moja
"Dhana hii ya kuwa na uhusiano na maumbile yote, usawa wetu na utangamano ambao tumeagizwa kuudumisha na jinsi tunavyoishi, jinsi tunavyoitunza dunia kwa sababu inatujali: Ni maelewano matakatifu," alisema Bibi Mona. Alishiriki mtazamo wa Watu wa Asili ambao unaona jukumu la binadamu kama wasimamizi wa dunia, akisisitiza umuhimu wa kudumisha uwiano na ulimwengu asilia. Pia aliakisi umuhimu wa kukusanyika pamoja ili kubadilishana maoni na uzoefu katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi. "Sote tuna uzoefu mbalimbali nayo," alisema, "Uzoefu wetu unaweza kuanzia, ukame, hadi mafuriko makubwa, kupanda kwa kina cha bahari, mambo kama hayo yanayotokea kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi." Kwa kuzingatia hilo, aliendelea, Mkutano huo unatoa fursa kwa uzoefu, akili na imani hizi tofauti kuja pamoja ili kusaidia kupata masuluhisho yanayoonekana kulinda mazingira.
Mahitaji ya kiasili yanasikilizwa
Bibi Mona aliendelea kuzungumzia nafasi ya kihistoria ya watu wa kiasili katika kutetea uhifadhi wa mazingira. Alikumbuka uzoefu wake wa mnamo miaka ya 1990, wakati "watu wa kiasili kwa mara ya kwanza waliruhusiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa." Alibainisha kwamba wakati huo “walitoa ujumbe wa kuitaka Umoja wa Mataifa kuhifadhi na kulinda mazingira, Dunia Mama.” Alitaja kwamba maonyo yaliyotolewa na Watu Asilia wakati huo sasa yanatimia, yakikazia uharaka wa ujumbe wao. Kilichomgusa Bibi Mona kuwa muhimu sana katika miaka ya hivi karibuni ni mabadiliko ya umakini. Kwa hiyo alikazia kusema kuwa, "Ninaona huo sio ujumbe tena ambao watu wa kiasili walileta Marekani lakini sasa ni ujumbe wa viongozi wote wa kidini, imani zote za ulimwengu," alisema, akielezea mabadiliko ya maadili na vipaumbele ambavyo miongoni mwa viongozi wa imani kama hatua chanya kuelekea hatua ya pamoja na mabadiliko chanya.
Hatua nzuri mbele
Kwa njia hiyo Bibi Mona alionesha matumaini yake kwa siku zijazo kwamba: "Naona hii ni hatua kubwa mbele katika kushughulikia na kuchukua hatua, hasa kufanya maombi kuwa sehemu ya hatua," alisema. Hatimaye, alitoa sala ya dhati kwa ajili ya kilele cha COP28, akisema, "Ninaomba kwamba COP28 kuhusu mabadiliko ya tabianchi ione hatua kali sana, zilizochukuliwa, ahadi kali, na utimilifu wa malengo hayo kushughulikia mabadiliko ya tabianchi."