Umoja wa Mataifa unasalia kuwa tegemeo la mabilioni ya watu duniani wakati huu wa mahangaiko  katikati ya janga la UVIKO19,uharibifu wa mazingira, vita na majanga mengineyo Umoja wa Mataifa unasalia kuwa tegemeo la mabilioni ya watu duniani wakati huu wa mahangaiko katikati ya janga la UVIKO19,uharibifu wa mazingira, vita na majanga mengineyo 

Rais mteule wa Baraza Kuu la UNGA76 asema matumaini ndio msingi

Tumaini limeongezeka katikati ya janga la Uviko ambapo ni wakati wa kusimama kidete na kutoa matumaini kwa kuwa“tumeshuhudia utu ubora wa juu kabisa. Kujitoa kwa wahudumu,madaktari,wauguzi na watu wa kawaida wakitoa maisha yao sadaka ili kusaidia wengine.Tumeona chanjo imetengenezwa katika kasi isiyo ya kawaida.Amebainishwa na Rais mteule wa Baraza Kuu la UNGA76

Na Sr Angela Rwezaula -Vatican.

Jumanne tarehe 14 Septemba 2021, Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 umefungwa rasmi na kutoa fursa ya kufunguliwa kwa mkutano mwingine wa 76 wa Baraza Kuu hilo la UNGA76,siku hiyo hiyo ambapo  rais wake mteule Bwana Abdulla Shahid kutoka Maldives amebainisha matumaini ya Umoja huo kusalia kuwa tegemeo la mabilioni ya watu duniani wakati huu wa mahangaiko  katikati ya janga la UVIKO19, uharibifu wa mazingira, vita na majanga mengineyo. Bwana Sahid akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, UN News, jijini New York, Marekani kabla ya kuapishwa rasmi tarehe 14 Septe kupokea kijiti cha kuongoza Baraza hilo,  Bwana Shahid amesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo ndilo chombo chenye uwakilishi mpana zaidi katika Umoja huo limeundwa ili kuweka mwongozo wa muundo wa matumaini yao.

Ametoa mfano wa jinsi tumaini lilivyoongeza katikati ya janga la Uviko na kwamba ni wakati wa kusimama kidete na kutoa matumaini kwa kuwa “tumeshuhudia utu katika ubora wa juu kabisa. Tumeona kujitoa kwa hali na mali kwa wahudumu walio mstari wa mbele. Tumeona madaktari, wauguzi na watu wa kawaida kabisa wakitoa maisha yao sadaka ili kusaidia wengine. Hicho ni tumaini. Tumeona chanjo imetengenezwa katika kasi isiyo ya kawaida. Hilo ni tumaini.” Akagusia pia hatua atakazochukua kukabili mabadiliko ya tabianchi amesema: “natarajia kuitisha kikao maalum ili kupatia nchi fura ya kukutana na kupitisha tamko la mwisho la kisiasa. Ndio tumeazimia kupunguza joto kwa nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi. Ndio! Tunajali ubinadamu. Nchini Maldives ambako ninatoka, kila siku tunaishi na tishio la mabadiliko ya tabianchi lakini katu hatukati tamaa. Ubinadamu utashinda tishio hilo na tutaishi.” Bwana Shahid aliulizwa jinsi akavyotumia uongozi wake kuhamasisha usawa wa jinsia ambapo amesema: "ninaahidi kwamba katu sitokaa katika jopo la mkutano lisilo na uwiano kijinsia. Natarajia kuhakikisha kuwa suala la usawa wa kijinsia linaendelea kuwa moja ya vipaumbele vyangu vya juu wakati wote wa uongozi wangu.”

Nataimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kuwekeza kwa vijana: Rais huyu mteule wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amezungumzia pia ushirikiano wa kimataifa akisema ndio njia pekee ya kusonge mbele akisema kuwa, “nataka kupatia fursa wanadiplomasia vijana kutoka nchi ambazo hazina uwakilishi wa kutosha na ndio maana nimezindua mpango wa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa mafunzo kwa vijana. Ni kuwapatia fursa ya kufanya kazi na ofisi yangu ili wapate uzoefu wa kile kinachofanyika hapa. Kuwekeza katika ushirikiano wa kimataifa ndio tunapaswa kufanya sasa. Na uwekezaji mzuri zaidi wa ushirikiano wa kimataifa ni kuwekeza kupitia kwa vijana.” Mkutano wa UNGA76 ambao unaanza leo utamalizika mwezi Septemba mwaka 2022 ukijumuisha vikao mbalimbali ambapo wiki ijayo kutaanza mjadala wa wazi wa ngazi ya juu ukijumuisha hotuba za viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.

15 September 2021, 15:25