Rais mteule Hakainde Hichilema wa Chama cha Upinzani cha UPND ameibuka kidedea kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Zambia tarehe 8 Agosti 2021. Rais mteule Hakainde Hichilema wa Chama cha Upinzani cha UPND ameibuka kidedea kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Zambia tarehe 8 Agosti 2021. 

Rais Mteule Hakainde Hichilema wa Zambia! Ashusha Rungu Kwa E. Lungu!

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Zambia, tarehe 16 Agosti 2021 amemtangaza Bwana Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND) kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais kwa kupata kura 2,810,777. Amemshinda Bwana Edgar Lungu, Rais anayemaliza muda wake kutoka katika Chama cha Patriotic Front (PF) aliyejinyakulia kura 1,814,201.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Bwana Esau Chulu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Zambia, Jumatatu tarehe 16 Agosti 2021 amemtangaza Bwana Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND) kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais nchini Zambia kwa kupata kura 2,810,777. Amemshinda Bwana Edgar Lungu, Rais anayemaliza muda wake kutoka katika Chama cha Patriotic Front (PF) aliyejinyakulia kura 1,814,201. Kinyang’anyiro cha Urais nchini Zambia, kiliwashirikisha wagombea 16 katika uchaguzi mkuu uliofanyika, Jumapili tarehe 8 Agosti 2021. Wananchi milioni saba nchini Zambia walikuwa wamejiandikisha kupiga kura kati ya wakaazi milioni 19. Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, matokeo haya ni ushawishi mkubwa wa vijana nchini Zambia ambao wanataka kuona mageuzi makubwa katika uchumi wa Zambia pamoja na fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia (ZCCB), lilisema, katika ushindani huu mkubwa, kwa wale watakaoshindwa kihalali wakubaliane na matokeo na hivyo kuanza kujipanga tena upya! Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala huu si wakati wa kujikita katika uchoyo na ubinafsi.

Wananchi wenye haki ya kupiga kura walipaswa kuhakikisha kwamba, wanasukumwa na dhamiri nyofu kuwapigia kura wale wanaodhani kwamba, wataweza kuwaongoza vyema. Zambia ilifanya uchaguzi mkuu wa: Rais, Wabunge 156 na Viongozi wa Wilaya 117. Rais anayemaliza muda wake Edgar Lungu, baada ya kuangalia mwenendo wa matokeo akatangaza kwamba, Uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Agosti 2021wa Rais na Wabunge haukuwa huru na wa haki kufuatia vurugu zilizojitokeza katika mikoa mitatu nchini Zambia. Rais mteule wa Zambia Bwana Hakainde Hichilema alizaliwa tarehe 4 Juni 1962, huko Wilayani Monze, Zambia na kwa sasa ana umri wa miaka 59. Ni kati ya wafanyabiashara wazito nchini Zambia na takwimu zinaonesha kwamba, vitega uchumi vyake vina thamani ya dola za Kimarekani milioni 389 kwa takwimu za Mwaka 2021. Anasema ameingia kwenye medani za kisiasa si kwa ajili ya kutaka kuganga njaa kwa raslimali na utajiri wa Zambia, bali ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Zambia. Pia ni mkulima anayemiliki mashamba makubwa ambaye amewahi kugombea Uchaguzi mkuu kwa mara tano kati ya mwaka 2006, 2008, 2011, 2015, 2016 na kwa mwaka 2021 wananchi wa Zambia wameamua kumpatia fursa hii, ili aweze kuwaonesha dira na mwanga mpya hususan kwenye masuala ya fedha na uchumi.

Chama cha Upinzani cha UPND kinataka kurekebisha soko la fedha na kuinua uchumi nchini Zambia. Chama hiki cha upinzani kinataka kuwakomboa wananchi wa Zambia kutoka kwenye mzigo wa deni kubwa wanalodaiwa na China kiasi cha kuhatarisha usalama, ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Zambia katika ujumla wao! Chama cha UPND wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, kilitoa ahadi kumi na kati yake ni pamoja na kupandisha thamani ya fedha ya Zambia, Kwacha. Kupunguza bei za pembejeo za kilimo, ili kuwamotisha wakuliza kuzalisha zaidi mazao ya chakula na biashara ili kujiongezea pato. Zambia kwa sasa inapania kutoa elimu bure kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu pamoja na kuongeza kiwango cha mshahara wa watumishi wa umma. Kada ya wahudumu wa sekta ya afya kuajiriwa na Serikali kuu na kwamba, Serikali inayoingia sasa madarakani inataka kuzalisha ajira kwa vijana wa kizazi kipya sanjari na kupunguza bei ya mafuta. Wakandarasi wazawa watapewa kipaumbele cha kwanza katika ujenzi wa Zambia kuliko ilivyokuwa kwenye uongozi uliopita ambapo Kampuni za Kichina zilipewa upendeleo wa pekeee.

Mwishoni, kutakuwepo na kiwango cha chini cha mshahara ambacho wafanyakazi wote nchini Zambia watapaswa kulipwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi! Wananchi wa Zambia wanamkumbusha Rais mteule Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND) kwamba, ahadi ni deni, sasa na ni wakati wa utekelezaji wake baada ya kumshushia rungu Rais anayemaliza muda wake Edgar Lungu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu!

Uchaguzi Zambia
16 August 2021, 15:02