Mkutano wa Afya Kimataifa: Global Health Summit: Umetoa tamko la Roma la Mwaka 2021 Kuhusu Afya: Umuhimu wa kushikamana katika mapambano dhidi ya UVIKO 16. Mkutano wa Afya Kimataifa: Global Health Summit: Umetoa tamko la Roma la Mwaka 2021 Kuhusu Afya: Umuhimu wa kushikamana katika mapambano dhidi ya UVIKO 16. 

Tamko la Roma la Mwaka 2021 Kuhusu Afya: Chanjo ya UVIKO-19

Tamko la Roma la Mwaka 2021 Kuhusu Afya lina vipengele 16 vinavyopaswa kufanyiwa kazi na Nchi Tajiri Duniani, G20. Wajumbe wa mkutano huu, wameshirikisha uzoefu, mang’amuzi na changamoto walizokutana nazo katika mapambano dhidi ya janga la UVIKO-19. Hakutakuwepo na amani wala utulivu duniani hadi pale janga la UVIKO-19 litakapokuwa limedhibitiwa kikamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Zaidi ya viongozi 20 wakuu wa nchi, serikali na mashirika 12 ya kimataifa, likiwemo Shirika la Afya Duniani, WHO, Umoja wa Afrika, Shirika la Biashara Duniani, WTO pamoja na Benki ya Dunia, WB, tarehe 21 Mei 2021 wameshiriki Mkutano wa Afya Kimataifa kwa njia ya mtandao. Baadaye wametoa “Tamko la Roma la Mwaka 2021 Kuhusu Afya”: “The Rome Declaration.” Tamko hili lina vipengele 16 vinavyopaswa kufanyiwa kazi na Nchi Tajiri Duniani, G20. Wajumbe wa mkutano huu, wameshirikisha uzoefu, mang’amuzi na changamoto walizokutana nazo katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hakutakuwepo na amani wala utulivu duniani hadi pale janga la UVIKO-19 litakapokuwa limedhibitiwa kikamilifu. Jambo hili linawezekana ikiwa kama chanjo itaweza kutolewa kwa watu wengi zaidi kwa kuzingatia usalama na ufanisi wake. Juhudi zote hizi hazina budi kuungwa mkono na sera pamoja na mikakati mbalimbali ya kupambana na UVIKO-19. Shirika la Afya Duniani, WHO limeutangaza Mwaka 2021 kuwa ni Mwaka wa Wahudumu Katika Sekta ya Afya.

G20 zitaendelea kuunga mkono juhudi za WHO katika kujibu changamoto za UVIKO-19 kwa kuwekeza zaidi katika mchakato wa maboresho afya ya msingi pamoja na kuweka vitega uchumi. Sekta ya umma na binafsi ziungane na kushirikiana katika mapambano dhidi janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona. Hii ikiwa ni pamoja na vifaa tiba. Mchakato wa chanjo ya Kimataifa dhidi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. G20 zitachangia gharama ili kufanikisha zoezi la kutoa chanjo hasa kwa nchi maskini zaidi duniani, ikiwa kama hali ya uchumi itaruhusu! Wadau mbalimbali wanaohusika na mchakato wa kutengeneza chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 wanapaswa kushirikiana na kutoa taarifa ya jinsi ya kuboresha mapambano dhidi ya UVIKO-19. G20 zimejiwekea kanuni 16 zitakazosaidia kupambana na UVIKO-19 pamoja na kujiweka tayari kupambana na dharura ya kiafya itakayojitokeza kwa siku za usoni.

Hii ni pamoja na kuboresha miundombinu ya afya kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2030. Kuwepo na ushirikiano katika sekta mbalimbali ili kuwa na mfumo mmoja wa kupambana na majanga katika sekta ya afya. Lazima kuwepo na uwajibikaji mkubwa kwa upande wa Serikali husika pamoja na kuzingatia mchakato wa utengenezaji na ugavi wa chanjo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa na uwezo wa kutengeneza dawa yenye ubora na viwango vya hali ya juu na yenye usalama. Jumuiya ya Kimataifa ijiandae kuzuia majanga kwa kuragibisha umuhimu wa chanjo kwa kutoa elimu ya afya bora. Kuna haja ya kuzijengea ujuzi na uwezo wa kuzalisha chanjo kwa kuzipatia vibali vya kutengeneza, kwa kuzipatia nchi hizi teknolojia itakayoziwezesha kuzalisha chanjo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika sekta ya afya pamoja na kuunda kikosi kazi kitakachokuwa tayari kutoa chanjo kwa magonjwa yanayoweza kuzuiwa.

Juhudi zaidi zielekezwe katika kupata chanjo ya ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria pamoja na magonjwa ambayo bado ni tishio kubwa kwa afya ya binadamu. Umefika wakati wa kuwekeza kwenye nguvu kazi, yaani wafanyakazi katika sekta ya afya, kwa kuzijengea jumuiya uwezo wa kupambana na magonjwa. Mchakato wa uchunguzi wa magonjwa, ukusanyaji wa takwimu na ushirikishaji wa takwimu ni mambo muhimu sana. Jumuiya ya Kimataifa iwekeze katika tasnia ya mawasiliano, ili watu waweze kupata habari sahihi kwa wakati muafaka. Shughuli zote hizi zinapaswa kuratibiwa kikamilifu sanjari na kupambana na maradhi, ujinga na umaskini wa hali na kipato. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujiandaa kikamilifu kupambana na magonjwa ya milipuko, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano na jamii husika. Kuna haja ya kuwa na fungu kwa ajili ya kujikimu wakati wa dharura inayodumu kwa muda mrefu.

Tamko la Roma

 

 

22 May 2021, 15:09