Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wawekezaji kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo ya viwanda. Wafanyakazi wajikite zaidi katika uaminifu na uadilifu kazini. Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wawekezaji kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo ya viwanda. Wafanyakazi wajikite zaidi katika uaminifu na uadilifu kazini. 

Tanzania Kuendelea Kutoa Zaidi Ushirikiano Kwa Wawekezaji!

”Mmewekeza kwa wakati na kwenye nchi sahihi na uwekezaji huu lazima utawaletea faida kwa sababu sera zetu za uwekezaji ni sahihi. Niwahakikishie kwamba Serikali yetu imejipanga vizuri katika kuwahudumia wawekezaji". Mkoa wa Pwani umepongezwa kwa kutumia vizuri fursa ya maendeleo ya viwanda Tanzania kwa kutenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji mkoani humo!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda kuunganisha magari cha GFA kilichoko Kibaha mkoani Pwani na ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji wote kwamba, Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano. ”Nimeridhishwa na kufarijika kuona hali ya kazi inayofanyika kiwandani hapa, niwahakikishie kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wenu. Mheshimiwa Rais aliona kazi yenu kupitia mitandao na akanituma nije nione”. Waziri Mkuu ametembelea kiwanda hicho Jumatatu, Aprili 19, 2021. Amesema hayo ndiyo mawazo ya viongozi wa nchi tangu Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufu na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. ”Mmewekeza kwa wakati sahihi na kwenye nchi sahihi na uwekezaji huu lazima utawaletea faida kwa sababu sera zetu za uwekezaji ni sahihi. Niwahakikishie kwamba Serikali yetu imejipanga vizuri katika kuwahudumia wawekezaji”. Pia, Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutumia vizuri fursa ya maendeleo ya viwanda nchini kwa kutenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri zake zote.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waendelee kuiunga mkono na kuiamini Serikali yao. Pia, Waziri Mkuu amewataka Watanzania walioajiriwa na kampuni hiyo wafanye kazi kwa bidii na wawe waaminifu na waadilifu. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amesema mkoa huo katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi 2021 umejenga viwanda 1,100 na kufanya mkoa huo kuwa na viwanda 1,438 kati yake vikubwa ni 82 kikiwemo na cha GFA. “Viwanda hivi vimetoa ajira za moja kwa moja 50,000 na za muda 100,000”. Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa GFA, Bw. Jawaad Karmali alisema kiwanda chao kina uwezo wa kuunganisha magari ya aina yote kutokana na teknolojia waliyo nayo ila kwa sasa wameanza kwa kuunganisha malori. Alisema kiwanda chao kimeajiri watumishi takribani 100, huku uwekezaji wao ukigharimu sh. bilioni 12. Uwekezaji huo unafanyika kwa awamu mbili, ambapo katika awamu ya kwanza wameshatumia sh. bilioni nne.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Suzana Steven Chaula baada ya kutoridhishwa na utendaji wake. Akizungumzia kuhusu Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Mhandisi Ronald Rwakatare, Waziri Mkuu amesema suala hilo atalikabidhi kwa Mamlaka ya uteuzi. Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo Jumatatu, Aprili 19, 2021 wakati alipotembelea kituo cha Kikuu cha DART-Gerezani ambapo alionesha kutoridhishwa na utendaji wa viongozi hao. “Tangu Mtendaji Mkuu ameingia DART ana miaka mitano hakuna hata basi moja alilonunua, na anasema hana fedha kwani abiria hawasafiri si kila siku wanapigania kule Kimara na wote wanalipa unasemaje hakuna fedha ya kununulia magari”. Waziri Mkuu amesema kuwa tangu mradi huo ulipoanza mabasi yamekuwa yakipungua kutoka 140 hadi 85. “Watendaji wapo tu wamekaa ofisini wanapigwa na AC (viyoyozi) wananchi wanaumia.

Hatuna sababu ya kumbakiza mtu kama hafanyi kazi”. Amesema wakala huo ulianzishwa na Serikali kwa ajili ya kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi lakini viongozi hao wameshindwa kusimamia vizuri na hivyo kusababisha mradi huo kutoendelea vizuri. Waziri Mkuu amesema mapato mengi ya Serikali yamekuwa yakipotea kutokana na uendeshaji wa wakala huo. “Kwa nini ukatishaji wa tiketi haufanyiki kwa njia ya kielektroniki kwa asilimia 100? Tiketi zinauzwa kwa vifurushi.” “Haiwezekani watu wanafanya ujanja ujanja tu wakuja na tiketi zao za mfukoni alafu wakimaliza anauza za POS (Mashine ya Kielektroniki ya Kukusanyia Mapato) na wasimamizi wapo tu Mkurugenzi wa Fedha yupo tu ameshindwa kusimamia hili na lipo mikononi mwake”. “Kwa nini mnauza tiketi kwa vifurushi hamtumii mashine kukata tiketi. Mnaua wakala huu kwa sababu wauzaji wa tiketi wanakuja na tiketi zao na nyingine mnazileta nyinyi. Hamuwezi kusimamia mradi huu wa kimkakati”.

Pia, Waziri Mkuu ametembelea karakana ya UDA ya Kurasini, Dar es Salaam na ameshuhudia baadhi ya mabasi ya wakala huo yakiwa mabovu na alipouliza yanakabiliwa na changamoto gani Mhandisi Rwakatare alisema yanatatizo la mfumo wa gia (Gearbox). Hata hivyo Mheshimiwa Majaliwa alibaini kuwa magari hayo yanachangamoto nyingine na siyo gearbox pekee kwa sababu baadhi yake yalikuwa yameondolewa baadhi ya vipuri, viti pamoja na matairi. “…Unanidanganya gearbox ndiyo imeharibika wakati magari chakavu hivi yameharibika kabisa, kama gearbox ndio tatizo mbona kwenye magari mengine mmetoa hadi viti na matairi? Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Forodha Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Njaule Mdendu ahakikishe mzigo ya wateja katika bandari hiyo inatoka kwa wakati. Ametoa agizo hilo alipotembelea Kituo cha Forodha Bandari Kavu iliyopo Ubungo mkoani Dar es Salaam.

20 April 2021, 11:35