Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania iko imara na itaendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu kwani hii ndiyo siri ya mafaniko na maendeleo nchini Tanzania. Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania iko imara na itaendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu kwani hii ndiyo siri ya mafaniko na maendeleo nchini Tanzania. 

Serikali ya Tanzania Iko Imara: Amani na Umoja Kudumishwa!

Watanzania wametakiwa kuchapa kazi kwa bidii, juhudi na maarifa na kwamba, Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi mkuu ipo imara na imejipanga kisawasawa na wala hakuna "kudema". Itaendelea kudumisha amani na utulivu kama siri ya mafanikio ya maendeleo na ustawi wa watanzania wote. Miradi ya kimkakati itaendelea kujengwa, ili kuboresha uchumi na kipato!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo imara na miradi yote ya kimkakati inaendelea kujengwa, hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani nayo. Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo makini na inaendelea kuwatumikia Watanzania. ”Tuendelee kuchapa kazi”. Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumanne, Aprili 20, 2021 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, Dar es Salaam. ”Siri ya kuwepo mafanikio na maendeleo nchini ni utulivu na amani. Tulianza vizuri tangu Serikali ya Awamu ya kwanza, tutaendelea kuimarisha amani na utulivu.” Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania watumie muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo kuliko mambo mengine yasiyo na tija.

Akizungumzia kuhusu mradi huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema amefurahi kukuta majengo yamekamilika na kwamba ameridhika na maendeleo ya ujenzi wake. Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe wanakamilisha kazi iliyosalia haraka ili mwaka huu 2021wananchi waanze kuishi hapo. Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA, Bw. Daud Kondoro amesema mradi huo una jumla ya block tano na ambazo zina uwezo wa kuchukua familia 656. Amesema mbali na ujenzi wa nyumba hizo za makazi pia katika eneo hilo wanajenga maduka makubwa pamoja na vizimba kwa ajili ya wajasiriamali kufanya biashara. Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika Mei 2021. Hadi sasa umefikia asilimia 94 ya utekelezaji wake na gharama yake ni shilingi bilioni 50. Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota, Waziri Mkuu alikagua kituo cha Reli ya Kisasa cha Tanzanite jijini Dar es Salaam.

 

21 April 2021, 11:49