Msaada wa vyakula kutoka mashirika la Mpango chakula Ulimwenguni kwa ajili ya kusaidia watoto na watu wakimbizi barani Afrika  Msaada wa vyakula kutoka mashirika la Mpango chakula Ulimwenguni kwa ajili ya kusaidia watoto na watu wakimbizi barani Afrika  

Msaada wa kibinadamu wa milioni £ 54.5 kwa watu wa maziwa makuu,Afrika!

Ufadhili mpya wa € milioni 54.5 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu utatolewa ili kuwasaidia watu walio katika mazingira magumu walioathiriwa na majanga ya asili au ya wanadamu,magonjwa ya milipuko na makazi yao katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.Na tarehe 14 Aprili ni siku ya ugonjwa wa Chagas ambapo takribani ya watu 10,000 kila mwaka wanakufa kwa sababu hiyo

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya tarehe 13 Aprili imetangaza ufadhili mpya wa € milioni 54.5 wa ajili ya misaada ya kibinadamu. “Msaada huu wa kuokoa maisha utatolewa kwa watu walio katika mazingira magumu walioathiriwa na majanga ya asili au ya wanadamu, magonjwa ya milipuko na makazi yao katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.” Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa kutoka Bruxelles, inasema kuwa “msaada huo utakidhi mahitaji ya walio hatarini zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Burundi na itasaidia wakimbizi wa Burundi waliko DRC, Rwanda na Tanzania. Kamishna wa Usimamizi wa Mgogoro Janez Lenarčič amesema: “Watu wengi katika eneo la Maziwa Makuu wanakabiliwa na mizozo na vurugu, majanga ya asili, pamoja na milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa kama vile kipindupindu, surua na Ebola, tishio ambalo limeibuka hivi karibuni katika Kanda hiyo”. Covid-19 na athari zake za kiafya na kijamii na kiuchumi zinazidisha hali mbaya ya kibinadamu. Kiwango cha mgogoro wa kibinadamu, hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ni cha kutia wasiwasi sana. Msaada wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) utatumika kutoa chakula, huduma ya afya na ulinzi, kuboresha utayari wa dharura na majanga na kuongeza ufikiaji wa elimu kwa watu waliokimbia makazi yao”.

Aprili, 14 ni siku ya ugonjwa wa Chagas ambapo unaua karibu watu 10,000 kila mwaka

 Shirika la kimataifa la kufanikisha uwepo wa tiba nafuu duniani, Unitaid linaloratibiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, limesema uwepo wa Covid-19 umefanya hali kuwa mbaya zaidi kwa hali ambayo tayari ilikuwa mbaya kutokana na ugonjwa wa Chagas. Imesema hayo tarehe 13 Aprili  katika kuelekeza siku ya ugonjwa wa Chagas, ambayo inafanyika kila mwaka tarehe 14 Aprili. Ugonjwa wa Chagas, ni ugonjwa ambao unaambukizwa na mdudu ambaye ananyonya damu anayeitwa Trypanosoma cruzi au T. cruzi, na ambaye kwa mujibu wa Unitaid linathibitisha kuwa kwa sasa unaathiri watu kati ya milioni 6 na 7 ulimwenguni kote na unaua watu wanaokadiriwa kuwa 10,000 kila mwaka, Aidha, Unitaid wanaeleza kuwa katika bara la Amerika ya Kusini ambako umeenea kwa wingi, ugonjwa wa Chagas unasababisha vifo vingi kuliko ugonjwa wowote wa vimelea ikiwemo malaria. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO), takriban watu milioni 75 wako katika hatari ya kuambukizwa, wengi wao wakiwa miongoni mwa watu maskini na wanaoishi pembezoni zaidi. Licha ya viwango vya juu vya ugonjwa na mzigo mkubwa wa kiuchumi, ni asilimia 7 tu ya watu walio na ugonjwa wa Chagas wanaogunduliwa, na ni asilimia 1 tu wanaopata huduma inayofaa. Ugonjwa huu ukiachwa bila kutibiwa unaweza kusababisha matatizo makubwa ya moyo na mmeng'enyo wa chakula, kwa mujibu wa maelezo ya  shirika hilo linaloratibiwa na WHO.

Wenye ugonjwa wa Chagas pia wako hatarini zaidi kwa Covid-19 

Covid-19 imeyafanya mambo kuwa mabaya zaidi. Wengi wa wale wanaougua ugonjwa wa Chagas ni miongoni mwa makundi ya watu walio katika hatari zaidi ya janga la COVID-19. Wagonjwa walioambukizwa na ugonjwa pia wako katika hatari ya kupata COVID-19 iliyo kali. Zaidi pia, kuelekeza kwa rasilimali za kupambana na magonjwa mengine, kwenda katika mapambano dhidi ya COVID-19 kumeongeza shinikizo maradufu kwenye vituo vya afya na pia wasiwasi wa wagonjwa kupata maambukizi ya COVID-19 pindi wanapotembelea vituo vya afya kumeleta changamoto mpya za mapambano dhidi ya Chagas.  Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanatajwa kuwa njia kuu ya kuambukiza ugonjwa wa Chagas. Kwa mujibu wa Mauricio Cysne, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Nje katika Unitaid anasema, “ugonjwa wa Chagas huathiri watu milioni 6-7 kwa mwaka Amerika Kusini yote. Ni ugonjwa wa kimyakimya ambao unaathiri watu maskini zaidi, walio katika mazingira magumu zaidi na unaua pole pole”. Karibu wanawake milioni 2 wa umri wa kupata watoto wanakadiriwa kuathiriwa na Chagas. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni njia kuu ya kuambukiza, kwani ugonjwa huo unakuwa haujagunduliwa au kutibiwa kwa mama na mtoto mchanga.”   Unitaid inatahadharisha kuwa wakati maambukizi mengi  bado yanatokea Amerika Kusini, ugonjwa huu unazidi kuenea katika maeneo mengine na maambukizi yanaonekana katika maeneo kama Marekani, Ulaya, Canada, Japan na Australia.

14 April 2021, 12:45