Maelfu ya watanzania na watu wenye mapenzi mema wamefurika Jijini Mwanza kutoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyeaga dunia tarehe 17 Machi 2021. Maelfu ya watanzania na watu wenye mapenzi mema wamefurika Jijini Mwanza kutoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyeaga dunia tarehe 17 Machi 2021. 

Dkt. Magufuli Ameacha Alama ya Kudumu! We! Achana na Jiwe!

Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa pole kwa Wanakanda ya Ziwa Victoria na anawasihi katika kipindi hiki cha majonzi wawe watulivu, waendelee kushikamana, kushirikiana na kupendana kama ilivyokuwa awali. Kila mwananchi aendelee kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Hayati Dkt. Magufuli pahala pema. Watanzania wameonesha mahaba kwa Uncle Magu, Mtu wa watu!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Mwanza, Tanzania.

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi mahiri na ameacha alama Taifa zima na ndiyo sababu analiliwa na wananchi nchi nzima hadi vijijini. Ameyasema hayo leo Jumatano, Machi 24, 2021 alipozungumza na wananchi kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza kabla ya shughuli za kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli ambayo iliongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla. ”Mpendwa wetu kaka yetu kiongozi wetu Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi shupavu aliyeliongoza Taifa hili kwa umahiri mkubwa na Mwanza ni mahali pa kihistoria kwa kiongozi wetu, ameishi hapa, amefanya kazi hapa na katika utumishi wake amefanya mambo makubwa ambayo yameweka alama kwenye mikoa hii ya Kanda ya Ziwa.”

Akiwasilisha salamu za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema kwamba, Rais anawapa pole Wanakanda ya Ziwa na anawasihi katika kipindi hiki cha majonzi wawe watulivu, waendelee kushikamana, kushirikiana na kupendana kama ilivyokuwa awali. Amesema kila mwananchi kwa dini yake na dhehebu lake aendelee kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Hayati Dkt. Magufuli pahala pema. Waziri Mkuu amesema baada ya viongozi kumaliza kuaga, mwili utazungushwa katika uwanja huo ili kutoa nafasi kwa wananchi kumuaga Hayati Dkt. Magufuli na kisha mwili utazungushwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza. Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya mwili huo kuzungushwa katika jiji hilo, utaelekea Chato mkoani Geita kwa kupita katika daraja la Kigongo-Busisi na mwili utakapofika hapo utasimama kwa dakika kumi ili kutoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo ambapo ni nyumbani kwa Mama Janet Mgufuli mke wa marehemu kuaga mwili wa hayati Dkt. Magufuli. 

Mapema asubuhi tarehe 24 Machi 2021 Mheshimiwa Majaliwa aliwaongoza viongozi mbalimbali na wananchi wa mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kuupokea mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Mwanza. Vilio, huzuni na simanzi zilitawala kwa wananchi waliojipanga pembezoni mwa barabara kuanzia uwanja wa ndege wa Mwanza hadi uwanja wa CCM Kirumba, ambapo ulipofika katika eneo la Nyamanoro ambako marehemu aliwahi kuishi msafara ulisimama ili kutoa fursa kwa waliokuwa majirani kumuaga. Hayati Dkt. Magufuli alifariki dunia Jumatano Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Ijumaa Machi 26 wilayani Chato mkoani Geita.

24 March 2021, 10:51