2021.01.19  Ni muhimu Chanjo iweze kuwafikia hata nchi Maskini kwa mujibu wa Msemaji mkuu wa Shirika la Afya ulilmwenguni 2021.01.19 Ni muhimu Chanjo iweze kuwafikia hata nchi Maskini kwa mujibu wa Msemaji mkuu wa Shirika la Afya ulilmwenguni  

Hofu ya Who katika usawa wa chanjo dhidi ya Covid-19 kwa chi

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani (WHO)amesema dunia imepoteza takriban watu milioni moja na wengine waliofariki ikiwemo wafanyakazi wa Shirika hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa,hivyo wajibu wa kila mtu ni kukahikisha kwamba changamoto zozote zinakabiliwa.Hofu yake ni ule ubinafsi wa chanjo ya Covid-19,kutoweza kuwafikia nchi maskini kwani huo ni mwelekeo wa anguko kuu la kijamii.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus ameonya juu ya ukosefu wa usawa katika usambazaji na upatikanaji wa chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 licha ya kwamba chanjo hiyo imepatikana katika kipindi kifupi zaidi kulinganishwa na chanjo zingine. Dkt. Tedros amesema kuwa miaka 40 iliyopita virusi vipya vilizuka na kuzua janga. Dawa za kuokoa maisha zilibuniwa zaidi ya muongo mmoja uliopita kabla ya nchi maskini kuweza kuzifikia na janga lilikuwa limekwisha. Kwa sasa mwaka mmoja umepita na virusi vipya vimezuka na kusababisha janga. Chanjo zimebuniwa, kile kitakachofanyika baada ya hapa ni juu ya wote.  Dk. Tedros amesema hayo Jumatatu tarehe 18 Januari 2021 kwenye mkutano wa bodi ya shirika hilo la kikao cha 148 mjini Geneva Uswisi, ambapo amesema kuwa kuna fursaa sasa ya kubadili historia na kuandika simulizi tofauti: kubadili makosa ya virusi vya ukimwi, HIV na homa ya mafua H1N1 na vya sasa vya COVID-19. Akiendelea na ufafanuzi wake amesema kubuniwa na kupitishwa kwa chanjo salama na iliyo na uwezo chini ya muda wa mwaka mmoja tangu kuzuka kwa virusi ni hatua kubwa na inayotia matumaini. Lakini kuibuka kwa aina tofauti ya virusi kunahitaji usambazaji haraka wa chanjo.

Kukabiliana na hatari ya ukosefu wa usawa kati ya matajiri na maskini

Hata hivyo ameonya kwamba, lazima kukakabiliana  na hatari kwamba hata wakati chanjo zikileta matumaini, kuna kikwazo cha usawa kati ya dunia ya walionavyo na wasionavyo.  Katika ukosefu wa usawa huu amesema chanjo za mwanzo zinavyoanza kusambazwa, ahadi ya uwiano katika usambazaji iko hatarini. Zaidi ya dozi milioni 39 zimetolewa angalau  nchi 49 za kipato cha juu. Na ni chanjo 25  tu zimetolewa katika nchi maskini. Yaani si milioni 25 au elfu 25, ni 25.  Kwa upande huo amethibitisha uwazi wake kwamba dunia iko katika hatari ya anguko na gharama hiyo italipwa katika nchi maskini zaidi. Aidha amesema hata wakati walikuwa wakizungumza suala hilo la usawa bado kuna nchi zinazungumzia makubaliano kati ya nchi mbili badala ya kupitia mpango wao wa COVAX.

Kuna chanjo za kutosha kwa kila mti lakini lazima kufanya kazi pamoja

Serikali zote zinataka kupatia kipaumbele utoaji chanjo kwa wahudumu wa afya na wazee kwanza lakini sio sawa kwamba vijana na watu walio na afya bora katika nchi tajiri wapate chanjo kabla ya wahudumu wa afya na wazee katika nchi maskini, amebainisha maoni yake Dk Teodros. Aidha amesisitiza kuwa kuna chanjo za kutosha kwa kila mtu lakini ni lazima kufanya kazi pamoja kama familia moja ili kuwapa kipaumbele  cha wale walio hatarini zaidi kwa ugonjwa uliokithiri na vifo katika nchi zote. Akiendelea amesema,  katika kipindi cha miezi 9 kumekuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha usambazaji sawa wa chanjo lakini, katika wiki chache zilizopita amesikia kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wakiuliza iwapo COVAX itakuwa na chanjo wanazozihitaji na iwapo nchi tajiri zitaweka ahadi zilizotoa. Kwa njia Dk. Tedros ameonya ubinafsi katika utoaji wa chanjo na hivyo amependekeza mambo matatu yatakayohakikisha chanjo inapatikana kwa wote.

Mikataba ya Covax iwe wazi na kupewa kipaumbele

Kwanza amependa kutoa wito  kwa nchi zilizo na mkataba kuwa wazi kuhusu mikataba hiyo na COVAX ikiwemo kuhusu idadi, bei na siku ya kuwasilishwa. Ametoa  wito kwa nchi hizo kupatia COVAX kipaumbele na kupatia COVAX dozi zao hususan baada ya kuchanja wahudumu wake wa afya na wazee ili nchi zingine ziweze kufanya hivyo. Pili, ametoa wito kwa wazalishaji wa chanjo kutoa takwimu kamili kwa  Shirika la Afya Ulimweguni (WHO) kwa ajili ya kukaguliwa na kuharakisha upitishaji, pia kutoa wito kwa wazalishaji kuruhusu nchi zilizo na mkataba na COVAX kupatia dozi COVAX na kuipa kipaumbele COVAX wakati wa uwasilishaji wa chanjo. Na hatimaye pendekezo la tatu ametoa wito kwa nchi zote kutoa chanjo ambazo zimefikia viwango vya kimataifa kwa ajili ya usalama, uwezo na viwango na kuimarisha utayari wa usambazaji.

Ifikapo mwezi Aprili katika Siku ya Afya chanjo iwe imefika kila nchi

Katika matazamia ya “Siku ya Afya Duniani 2021 Dk. Tedros ametoa changamoto kwa nchi wanachama kuhakikisha kwamba ifikapo tarehe 7 mwezi Aprili, chanjo dhidi ya COVID-19 ziwe zimesambazwa katika kila nchi, kama ishara ya matumaini ya kutokomeza janga hilo na ukosefu wa usawa uliokita mizizi katika mojo ya changamoto za afya ulimwenguni.  Kwa kuongezea  amesema mwaka mmoja tangu kuzuka kwa ugonjwa wa virusi vya Corona ni dhahiri kwamba wote tunakabiliwa na hatari isiyotabirika lakini pia fursa isiyotabirika ya kufanya afya kuwa kiini cha maendeleo na msingi kwa ajili ya dunia salama na yenye usawa zaidi. Akihitimisha Mkuu huyo wa Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) amesema dunia imepoteza takriban watu milioni moja na wengine waliofariki ikiwemo wafanyakazi wa  Shirika hilo (WHO), zaidi ya mwaka mmoja sasa na hivyo wajibu wa kila mtu ni kukahikisha kwamba changamoto zozote zinazotukabili, wote  tunazikabili, mafunzo yoyote ambayo tunapata kutokana na uwepo wa janga, tunajifunza na fursa zozote tulizonazo za kujenga Dunia iliyo bora zaidi.

19 January 2021, 12:24