Sala huko Taize Sala huko Taize 

Taize,Von der Leyen:Hakuna anayejiokoa mwenyewe!

Rais wa Tume ya Ulaya,Bi Ursula von der Leyen,katika ujumbe aliotuma kwa washiriki wa mkutano wa Vijana wa Ulaya ulioandaliwa na kuongozwa na Jumuiya ya Taizé ambao,kwa sababu za janga covid-19,utafanyika kwenye jukwaa la digitali kuanzia tarehe 27 Desemba hadi 1 Januari 2021,anasisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kukabiliana na mgogoro wa janga la sasa.

Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican.

Hakuna mtu anayejiokoa peke yake. Tunahitajiana ili kumaliza janga na kujenga uchumi ulio wa  kijani zaidi na mzuri pia kuweza kumaliza uharibifu wa uumbaji. Ndivyo ameandika Rais wa Tume ya Ulaya, Bi Ursula von der Leyen, katika ujumbe wake aliotuma kwa washiriki wa mkutano wa vijana wa Ulaya, ulioandaliwa na unaoongozwa na Jumuiya ya Taizé na ambao kutokana na sababu za janga Covid-19, utafanyika mwaka huu kwenye jukwaa la digitali kuanzia tarehe 27 Desemba hadi 1 Januari 2021.

Katika ujumbe wake anaandika kuwa: “Kamwe haijawahi kutokea kama mwaka huu kwa wanaume na wanawake ulimwenguni kote kuweza kugundua jinsi gani hatima zetu zinaingiliana na tunashirikishana udhaifu huo. Maisha yetu yote yamegeuzwa na janga kwa njia moja au nyingine. Na nchi zetu zote zinapaswa kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Tunaweza kuzingatia juu ya tofauti zetu, juu ya kutokubaliana kwetu na kutokuelewana kwetu.”

Bi Ursula aidha emeandika kuwa “Au tunaweza kuchagua kuunganisha nguvu,  kwa ajili ya wema ambao ni wa kulinda hadhi ya kila mwanadamu na uzuri wa uumbaji”. Wakati wa changamoto kubwa kwa Ulaya na ulimwengu, anaandika rais wa Tume ya Ulaya kuwa “ingekuwa rahisi kukata tamaa. Lakini kama Ndugu Alois alivyokumbusha ishara za tumaini zinatoka kila pembe ya dunia. Idadi kubwa ya wanaume na wanawake wametumia wakati wao na hata kuhatarisha maisha yao kusaidia wazee, wagonjwa, na wapweke. Vijana wa mataifa yote wamejihami kwa jili ya sayari yetu. Na hapa Ulaya, tumeamua kuunganisha nguvu ili kusaidia nchi ambazo zimeathiriwa zaidi na janga hili. Mwaka huu wa mateso umekuwa mwaka wa mshikamano”.

Ikumbukwe kila mwaka Jumuiya ya kiekumene ya Taize nchini Ulaya huandaa tukio la  Mkutano wa Maombi kimataifa kwa vijana, na kufanyika katika vituo vya nchi mbali mbali barani Ulaya katika tarehe za mwisho wa mwaka na kufungua mwaka wakiwa katika maombi na tafakari. Kwa bahati mbaya mwaka huu, maelfu na maelfu ya vijana hawataweza kuonekana wamebeba mifuko yao wakielekea Taize , badala yake nyuso zao zitaonekana kupitia jukwaa la kidigitali kuanzia tarehe 27 Desemba hadi tarehe Mosi 2021.

26 December 2020, 14:30