Aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, amezikwa tarehe 26 Juni 2020 Kijijini kwake Munsinzira kwa heshima zote za kitaifa, mazishi yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka Afrika Mashariki. Aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, amezikwa tarehe 26 Juni 2020 Kijijini kwake Munsinzira kwa heshima zote za kitaifa, mazishi yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka Afrika Mashariki. 

Aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza Azikwa Munsinzira

Wananchi wa Burundi pamoja na viongozi mbali mbali wameshiriki kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu Rais Pierre Nkurunziza. Kwa upande wake Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye amesema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na Marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, tarehe 26 Juni 2020 amezikwa kijijini Munsinzira, kilichoko kwenye mkoa wa Gitega katikati mwa nchi ya Burundi. Wananchi wa Burundi pamoja na viongozi mbali mbali kutoka ndani na nje ya Burundi wameshiriki kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu Rais Pierre Nkurunziza. Kwa upande wake Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye amesema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na Marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo. Mama Denise Nkurunziza, mjane wa Rais Nkurunziza, katika salam za rambirambi na shukrani kwa wananchi wa Burundi, amebainisha kwamba, kifo cha mume wake ni ustashi wa Mwenyezi Mungu. Amewaombea watu wa Mungu nchini Burundi, ili waweze kupata viongozi shupavu watakaoweza kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo.

Familia ya Marehemu Rais Nkurunziza imesema, itaendeleza mema mengi yaliyoachwa na Rais Nkurunziza katika maisha yake; urithi ambao utavaliwa njuga na Mama mjane pamoja na watoto wake! Wamemwomba Mwenyezi Mungu awajalie nguvu ya kuweza kukubali na kuupokea msiba huu kwa imani na matumaini katika Mungu anayewatia nguvu! Naye Waziri Mkuu wa Tanzania, Kasim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kuisaidia nchi ya Burundi ili ifanikiwe katika adhma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoombwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza wakati wa uhai wake. Waziri Mkuu aliyasema hayo Ijumaa, Juni 26, 2020, alipozungumza kabla ya mazishi ya Rais Nkurunziza yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ingoma uliopo Gitega nchini Burundi, Mheshimiwa Majaliwa alisema ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. “Marehemu Rais Pierre Nkurunziza alitamani sana kukabidhi madaraka huku akiwa ametimiza kiu yake ya kutaka Burundi iwe mwanachama wa SADC jambo ambalo halikuwezekana naamini Mheshimiwa Rais utalisimamia suala hilo hadi litimie”.

Alisema Rais Dkt. Magufuli amemtuma afikishe salamu za pole kwa mke na familia ya marehemu, Rais wa Burundi na wananchi wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza kilichotokea Juni 9, 2020. Waziri Mkuu alisema Tanzania na Burundi ni ndugu na anaamini undugu na mshikamano huo utaendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuuimarisha mshikamao huo. Alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi kumpa ushirikiano Rais wao mpya Evariste Ndayishimiye kama walivyofanya kwa marehemu Nkurunziza ili aweze kuliongoza Taifa hilo vizuri. Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge. Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura jana asubuhi Juni 26, 2020, Mheshimiwa Majaliwa alipokelewa na Waziri Mkuu wa Burundi, Prosper Bazombaza. Baada ya mazishi hayo Mheshimiwa Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Burundi kabla ya kurejea nyumbani Tanzania.

27 June 2020, 13:20