Vatican News
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anamshukuru na kumpongeza Papa Francisko kwa mchango wake katika Jumuiya ya Kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anamshukuru na kumpongeza Papa Francisko kwa mchango wake katika Jumuiya ya Kimataifa.  (ANSA)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anampongeza Papa Francisko!

Umoja wa Mataifa unamshukuru Papa Francisko kwa jitihada zake kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mapambano dhidi ya umaskini duniani. Kwa kukazia umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa: pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza Malengo ya Maendeleo endelevu ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, Ijumaa tarehe 20 Desemba 2019 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano maalum na Gazeti la La Stampa linalochapishwa nchini Italia amesema anapenda kukutana na Baba Mtakatifu Francisko ili kumshukuru kwa jitihada zake kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mapambano dhidi ya umaskini duniani unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowapokea. Baba Mtakatifu ameendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030 kwa kusimama kidete kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Huu ni mchango mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Kimsingi vitendo vyote hivi ni uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Umoja wa Mataifa umeanzisha kampeni ya kulinda na kuhifadhi maeneo ya kidini ili kudumisha uhuru wa kuabudu na kuwawezesha waamini wa dini mbali mbali kushuhudia imani na kushiriki ibada mbali mbali katika amani. Nyumba za ibada sehemu mbali mbali za dunia zinapaswa kuwa ni mahali pa salama zaidi, lakini inasikitisha kuona kwamba, siku hizi nyumba za ibada zimekuwa zikishambuliwa mara kwa mara na watu wenye misimamo mikali ya kidini.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni kielelezo makini cha jinsi ya kuwekeza katika ujenzi wa mafungamano ya kijamii, kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Elimu makini inapaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa mafungamano ya kijamii, kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na mahubiri ya chuki dhidi ya waamini wa dini nyingine.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, anakaza kusema, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Chanzo kikuu cha wakimbizi na wahamiaji ni vita, kinzani, nyanyaso, dhuluma pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumekuwepo pia na ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani sanjari na kukua na kupanuka kwa miji na majiji. Mambo yote haya kwa kiasi kikubwa yanachangia ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Kuna maelfu ya watu wasiokuwa na makazi maalum, kiasi kwamba, Umoja wa Mataifa umeshindwa kutoa suluhu ya haraka na ya kudumu. Tarehe 17 Desemba 2019, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (United Nations High Commission for Refugees, UNHCR) limeandaa jukwaa litakalo wahusisha wadau mbali mbali kutoa maoni yao jinsi ya kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

UNHCR itawasilisha hali halisi jinsi ilivyo kwa wakati huu na kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto kama hizi kwa siku za mbeleni. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa sehemu mbali mbali za dunia. Lengo la jukwaa hili ni kupambana pia na biashara ya binadamu na viungo vyake; sababu zinazopelekea watu kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa kufunga safari zisizo na uhakika pamoja na kutafuta suluhu ya vita na migogoro mbali mbali duniani. Ushirikiano na mshikamano wa kimataifa ni jibu makini katika kukabiliana na changamoto za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Kuna haja pia kushirikishana nyajibu na majukumu.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP25 umehitimishwa huko mjini Madrid, nchini Hispania kwa kushindwa kutekeleza malengo ya kauli mbiu ya mkutano huo iliyohimiza kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua. Lengo la mkutano wa Madrid lilikuwa ni kukamilisha kanuni za utekelezaji mkataba wa Paris wa mwaka 2015 ambao unaitaka Jumuiya ya Kimataifa kupunguza kiwango cha joto duniani ifikapo mwaka 2020. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anasema amesikitishwa sana na matokeo ya mkutano huu, lakini kamwe hawezi kukata wala kujikatia tamaa. Ni matumaini yake kwamba, Mwaka 2020 nchi nyingi zaidi zitaweza kujizatiti katika kudhibiti ongezeko la kiwango cha joto duniani, kwa kufuata ushauri wa wanasayansi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Lengo la Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, ifikapo mwaka 2050, kiwango cha uzalishaji wa hewa ya ukaa kiwe kimefika zero kabisa!

Utengenezaji pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia duniani ni matokeo ya vita baridi na kwa sasa hali ya usalama wa Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuzorota sana, kiasi kwamba, baadhi ya mikataba na itifaki za Jumuiya ya Kimataifa kuhusu tema hii zimefutika kabisa. Kwa wakati huu, utengenezaji, ulimbikizaji na majaribio ya makombora ya silaha za maangamizi yanazidi kupamba moto sehemu mbali mbali za dunia. Mambo yote haya yanachagizwa na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia; pamoja na udukuzi wa mitandao unaendelea kuhatarisha umoja na mafungamano ya Kimataifa kiasi kwamba, baadhi ya nchi kwa sasa zinaanza kujihami. Mambo yote haya hayakubaliki kisiasa na kimaadili. Kuna hali ya kulega lega kwa uhusiano wa kidipomasia kati ya China na Marekani, hali ambayo inahatarisha sana masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ili kujenga na kudumisha uhakika wa usalama na amani duniani, kuna haja anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa dhati na kwa mantiki hii, Umoja wa Mataifa hauna budi kuwa na sauti ya mwisho!

Umoja wa Mataifa mwaka 2020 utakuwa unaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake na Mwaka 2045, utakuwa ni Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa tarehe 24 Oktoba 1945 huko San Francisco, California, nchini Marekani ili kulinda misingi ya: haki, amani, usalama, haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa, uhuru na demokrasia. Huu ni muda wa kuanzisha mchakato wa majadiliano kuhusu mustakabali wa Umoja wa Mataifa kwa siku za usoni. Kwa namna ya pekee, vijana wanatarajiwa kuhamasishwa zaidi kwani hawa ndio wadau wakuu wa Umoja wa Mataifa. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana ili kukabiliana na changamoto mamboleo mintarafu: haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kutoka kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ni mfumo mpya wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa:Papa Francisko
17 December 2019, 12:10