Vatican News
Picha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres akiwa ziara ya siku tatu (31 Agosti -2 Septemba 2019) nchini Congo DRC kutazama hali halisi ya nchi hiyo Picha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres akiwa ziara ya siku tatu (31 Agosti -2 Septemba 2019) nchini Congo DRC kutazama hali halisi ya nchi hiyo   (AFP or licensors)

CONGO DRC:Bwana Guterres awatia moyo walinda amani na kujitolea!

Ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na viongozi wengine waandamizi wa Umoja wa Mataifa kwa siku tatu kuanzia tarehe 31 Agosti 2019 nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo,DRC imewatia moyo walinda amani na kujitolea nchini humo ikiwa ni pamoja na pongezi kwa raia wote kwa ushirikiano wao katika hali halisi wanayokabiliana nayo yaani ghasia na magonjwa.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican News

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na viongozi wengine waandamizi wa Umoja wa Mataifa tarehe 31 Agosti 2019 wameanza ziara ya siku tatu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo wananchi wanakabiliwa na ukosefu wa usalama na janga la afya linaloendelea ikiwemo Ebola ambayo hadi sasa watu 2000 wamekwisha fariki. Bwana Guterres amewasili katika mji wa Goma ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambako ndiko kitovu cha mlipuko wa Ebola. Huko Goma amepokelewa na mwakilishi wake maalum nchini humo, Bi Lela Zerrougui  a baada ya kakagua kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa na amewashukuru kwa huduma yao na kujitolea kuweka maisha yao hatarini ili kuwalinda wananchi. Akizungumza na waandishi wa habari,Bwana Guterres ameeleza kufurahishwa kwake na ustahimilivu wa watu wa DRC na akasisitizia ushirikiano wa Umoja wa Mataifa katika kupambana na ugaidi, lakini siyo tu nchini DRC japokuwa ni suala la barani Afrika na duniani kote.  Kwa upande wa hali mbaya ya Ebola na masuala mengine makubwa ya afya kama vile surua, malaria na kipindupindu, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameahidi kuwa “Umoja wa Mataifa tunasimama bega kwa bega na mamlaka za Congo DRC na watu wa nchi hii ili kufanya kila tuliwezalo kukabiliana na changamoto hizi.”

Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus: Surua na Malaria vyaua kulikoko Ebola

Licha ya mlipuko wa Ebola lakini pia wananchi nchini DRC wanakabiliwa na madhara mabaya ya magonjwa mengine kama surua na malaria, ambapo  magonjwa hayo mawili kwa pamoja yanaua watu wengi zaidi kuliko hata  Ebola, amekumbusha hayo Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya ulimwenguni Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus. Dk. Tedros ambaye pia ni sehemu ya wajumbe wa Umoja wa Mataifa ambao wako ziarani amesema hii ndiyo maana uwekezaji katika mifumo ya afya kwa kuzingatia afya ya msingi ni muhimu ili kushughulikia mahitaji yote ya kiafya kwa njia kamilifu. Wakati wa ziara yake hii ya kwanza tangu alipoanza kuuongoza Umoja wa Mataifa mwezi Januari 2017, Bwana Guterres atakutana na viongozi wa ngazi za juu za serikali, wadau katika mchakato wa amani wa DRC, raia, poilisi na wanajeshi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo. Viongozi wengine alioambatana nao ni pamoja na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika Maziwa makuu Michel Kafondo; Matshidiso Moeti ambaye ni Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika; Mike Ryan Mkurugenzi mtendaji wa programu ya dharura za afya ya (WHO) na Ibrahima Socé Fall, Mkurugenzi mkuu msaidizi wa huduma za dharura za WHO.

Siku yake ya pili ya Ziara ya Bwana Guterres: shukrani kwa wananchi kwa ushirikiano

Katika siku ya pili ya ziara yake nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza heshima aliyonayo kwa wananchi wa DRC pamoja na kujitolea kwa walinda amani waliopoteza maisha wakiwahudumia wananchi. Bwana Guterres ameyasema hayo akizungumza Jumapili , tarehe 1 Septemba 2019,  katika mkutano na vyombo vya habari katika mji wa Beni ambao ni kitovu cha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambapo amesema watu wa eneo hili pia wanakabiliwa na matatizo mengine mazito kama vile surua, malaria na ukosefu wa usalama. Akiwahutubia wanahabari kwa lugha ya kifaransa Bwana Guterres amesema, “ni matumaini yangu kuwa uwepo wangu hapa leo unasisitiza tena uungaji mkono wangu  kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO katika mapambano dhidi ya makundi yenye silaha ambao wanasambaza hofu na vifo. MONUSCO na wadau wake yaani vikosi vya ulinzi vya DRC, na polisi wa kitaifa wa DRC wanaendelea kufanya kazi pamoja kuleta amani na usalama katika ukanda huu.”

Aidha, Katibu Mkuu Bwna Guetteres aidha ametoa  salamu zake za rambirambi kwa familia na wapendwa wa waathirika wa vurugu na akatoa wito kwa makundi yote yenye silaha kwa haraka kusitisha mashambulizi yao kwa wananchi pamoja na vikosi vya usalama vilivyotumwa kuwalinda wananchi wa Congo DRC, “walinda amani wamelipia gharama kubwa katika kulinda amani. Lakini hayo yanaimarisha lengo letu. Tutafanya kila tuwezalo kumaliza ukosefu wa amani katika eneo hili. Ni muhimu watu wa Beni wafahamu kuwa tunakisikia kilio cha mateso yao.” Bwana Guterres ameongeza kuwa, mfumo wa Umoja wa Mataifa umejizatiti kuzisaidia mamlaka za DRC, jamii na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya ukosekanaji wa usalama, na kuwa atalijadili suala hili pamoja na mamlaka za kitaifa katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa katika siku zijazo.

Tarehe 2 Septemba Katibu wa Umoja wa Mataifa amekutana na Rais Tshisekedi mjini Kinshasa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres tarehe 2 Septemba  mara baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Congo Felix Tshisekedi mjini Kinshasa, amezungumza na wanahabari kuwaeleza kwa ufupi kuhusu mkutano wake na rais na masuala waliyoyajadili kuanzia usalama na mlipuko wa magonjwa. Bwana Guterres ameanza kwa kuwaeleza wanahabari kuwa katika siku mbili alizokuwa jimboni Kivu Kaskazini, ameona kuwa kuna upepo wa matumaini unaovuma nchini DRC. Aidha amewaeleza kuwa amekuwa na fursa ya kukutana na Rais Tshisekedi na kuzungumzia dhamira yao kuwa leo ni kuna tukio la kihistoria nchini Congo, hali ambayo inaweza kutegemea maendeleo ya taasisi za kidemokrasia, uwepo wa serikali inataka kuibadilisha nchi, lakini pia uwepo wa upande wa upinzani ambao pia wanachangia katika upande muhimu wa maisha ya kisiasa ya nchi,  kuheshimu haki za binadamu na maono kwa mstakabali wa DRC.

Siku ya tatu ya ziara ya Bwana Guterres amesema UN haitawatelekeza watu wa DRC

"Nilikuwa Kivu Kaskazini na niliweza kuona ukubwa wa tishio la kundi la ADF na matendo yao ya kigaidi yasiyo vumilika dhidi ya watu wa Congo.” hata ni kwa mujibu wa Bwana Guterress ba kuongeza kusema, “tumekubaliana kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO wataimarisha uwezo wao kwa ajili ya hatua dhidi ya ADF na pia wataimarisha ushirikiano wao na vikosi vya Jamhuri ya kidemokrasia ya ili kushughulikia vema suala la usalama wa watu ambapo si tishio kwa watu wa DRC tu, bali pia tishio la kimataifa." Kadhalika  Bwana Guterres akijibu maswali ya waandishi wa habari amesema, “tumekuwa na mjadala mzuri na rais wa Jamhuri hii na nina uhakika kuwa ndani ya mpango mkakati wa MONUSCO, Baraza la usalama litaamua masuala kadhaa ambayo yanaweza kuboresha MONUSCO na ushirikiano wake na serikali ya DRC ili kuweka mazingira ambayo yataruhusu siku moja, MONUSCO kutokuwa na muhimu tena hapa, pia kuwa na uhusiano kati ya MONUSCO na Umoja wa Mataifa ambapo utakuwa wa kawaida kwa  watu wa Umoja wa Mataifa  ambao watafanya kazi na watu wa serikali kwa ajili ya ustawi wa watu wa DRC. Lakini kwa sasa bado tuko na DRC na niseme kwa uwazi kabisa: Umoja wa Mataifa hautawatelekeza watu wa DRC."

Kwa upande wa Ebola Bwana Guterres amesema kuwa, ni muhimu sana kupambana na Ebola ingawa pia ameona kuwa mapambano hayo hayahusu Ebola pekee, kwani kuna magonjwa mengine kama Surua, Maralia na kipindupindu. Hata hivyo emonesha namna alivyo furahi kukutana na manusura wa Ebola ambao walipatiwa matibabu kwa haraka na kupona, na kwamba : “kuna operesheni ya chanjo ya muhimu dhidi ya Ebola inayoendelea. Kuna vituo vya ukaguzi lakini pia vituo vya matibabu ambavyo nimevitembelea na sasa kuna tiba dhidi ya Ebola. Hayo ni mabadiliko makubwa.” Ikumbukwe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa nchini humo DRC kwa ziara ya siku tatu tangia Jumamosi tarehe 31 Agosti 2019.

03 September 2019, 13:17