Vatican News
Youth For Climate: Mtandao wa vijana wa kizazi kipya wanaotaka kuwashinikiza wanasayansi, wanasiasa na watunga sera kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira! Youth For Climate: Mtandao wa vijana wa kizazi kipya wanaotaka kuwashinikiza wanasayansi, wanasiasa na watunga sera kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira!  (AFP or licensors)

Vijana wasimama kidete kudai sera za utunzaji bora wa mazingira!

Mtandao wa vijana wa kizazi unasema, bado kuna uwezekano wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza badala ya kujikita katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko! Kuna madhara makubwa ya uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Greta Thunberg ni msichana mwenye umri wa miaka 16 ambaye ameibuka kuwa kweli ni mwanaharakati mahiri wa mazingira kutoka Sweden anaendelea kujipambanua katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya, kusimama kidete, ili kuwashinikiza wanasayansi, wanasiasa na watunga sera za kitaifa na kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza katika utunzaji bora wa mazingira. Bado kuna uwezekano wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza badala ya kujikita katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Kuna idadi kubwa ya watu wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa pamoja na mazingira katika ujumla wake. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, watu kati ya milioni 6-7 kila mwaka wanashambuliwa na magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira. Haya yamesemwa na wanasayansi katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira huko Nairobi, Kenya. Wanasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika sera za maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa teknolojia rafiki kwa mazingira.

Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanapenda kuunga mkono tafiti za kisayansi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kuwashinikiza wanasiasa na watunga sera kuanza kuchukua hatua madhubuti ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa ajili ya matumaini ya vijana wa kizazi hiki na kile kijacho! Msichana Greta Thunberg amekuwa ni “moto wa kuotea mbali” nchini Sweden tangu Septemba 2018 alipoamua kufanya mgomo wa chakula kila siku ya Ijumaa mbele ya Ukumbi wa Bunge la nchi yake.

Leo hii, kuna zaidi ya miji 1700 sehemu mbali mbali za dunia wanafanya maandamano ili kuwashinikiza viongozi wa Serikali kuanza kutekeleza Itifaki ya utunzaji bora wa mazingira iliyokubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa. Wazazi na walezi wanadai kwamba, wanawapenda sana watoto wao, lakini wao ndio wa kwanza kuharibu mazingira! Vijana wanasema, wataendelea kufanya mgomo hadi pale wanasiasa watakapoamua kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote. Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015, unazitaka nchi tajiri zaidi duniani kuonesha mshikamano wa dhati katika mchakato wa mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa vizazi vijavyo!

Ongezeko la hewa ya ukaa na joto duniani, kutasababisha pia kuongezeka kwa kina cha bahari sehemu mbali mbali za dunia, hali ambayo itapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Uchafuzi mkubwa wa mazingira unaendelea kuhatarisha upatikanaji wa maji safi na salama, sehemu ya haki msingi za binadamu na matokeo yake, ni watu wengi kuendelea kupoteza maisha kutokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu. Hali hii ina madhara makubwa katika mchakato mzima wa uchumi na maendeleo.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, sera na mikakati ya uchumi na maendeleo inapaswa kusikiliza kilio cha Dunia Mama na maskini, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Vijana wanasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi; kwa kuwekeza katika sera na mikakati ya uchumi endelevu na fungamani. Mwelekeo huu hauna budi kwenda sanjari na na ujenzi wa haki jamii, ili kujenga jamii inayofumbatwa katika haki na usawa.

Vijana na mazingira
15 March 2019, 11:30