Umoja wa Falme za Kiarabu uko tayari kumpokea Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao kama mjumbe wa amani na upatanisho Umoja wa Falme za Kiarabu uko tayari kumpokea Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao kama mjumbe wa amani na upatanisho  

Papa Francisko kuwasha moto wa udugu Falme za Kiarabu

Dr. Sultan Ahmed Al Jaber, Waziri katika Umoja wa Falme za Kiarabu, (UAE), katika tamko lake kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwake anasema, huu ni ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo Umoja wa Falme za Kiarabu unaendelea kuweka kumbu kumbu safi ya: watu kupokelewa, maridhiano pamoja na watu kushirikishwa katika ujenzi wa udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, anatarajia kufanya hija ya kitume ya ishirini na saba huko Abu Dhabi, kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu". Akiwa huko kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa mahubiri yake pamoja na hotuba kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini.

Dr. Sultan Ahmed Al Jaber, Waziri katika Umoja wa Falme za Kiarabu, (UAE), katika tamko lake kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwake anasema, huu ni ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo Umoja wa Falme za Kiarabu unaendelea kuweka kumbu kumbu safi ya: watu kupokelewa, maridhiano pamoja na watu kushirikishwa katika sera na mikakati ya maisha ya watu wa Umoja wa Falme za Kiarabu; mambo msingi katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Tangu mwanzo wa uwepo wake, Umoja wa Falme za Kiarabu umekita mizizi yake katika haki msingi, uhuru wa kidini na kiimani pamoja na kupambana na mifumo mbali mbali ya ubaguzi unaoweza kujionesha kwa misingi ya kidini au kikabila. Papa Francisko atakutana na Wakristo milioni moja wanaoshuhudia imani sanjari na uwepo wa ndugu zao Waislam ambao ni wengi zaidi kwa idadi. Waamini wa dini mbali mbali wamekuwa wakisali kwa uhuru kama kielelezo cha Jamii ambayo inakita mizizi na utambulisho wake katika ukweli na uwazi.

Umoja wa Falme za Kiarabu una wananchi wanaotoka katika nchi 200. Hawa ni watu kutoka makabila, lugha na jamaa wanaoishi na kufanya kazi katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Ukarimu ni sehemu ya vinasaba vya watu wa Umoja wa Falme za Kiarabu ambazo wamerithi kutoka kwa muasisi wa taifa hili Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan. Hii ni nchi ambayo inajitahidi kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kukuza na kudumisha umoja, ustawi na maendeleo ya wengi, kwa kuheshimiana na kuthaminiana na kwamba, tamaduni zote zinaangaliwa katika usawa pasi na upendeleo!

Dr. Sultan Ahmed Al Jaber anakaza kusema, Umoja wa Falme za Kiarabu ulianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na Vatican kunako mwaka 2007 na tangu wakati huo, viongozi wakuu kutoka Serikalini wametembelea Vatican na hivi karibuni wamemtembelea na kutoa mwaliko kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kushiriki katika Mkutano wa Majadililiano ya Kidini Kimataifa, tukio ambalo litawashirikisha wakuu mbali mbali wa kidini kutoka ndani na nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Mwaka wa Maridhiano ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kwa kukazia ukarimu na ushiriki mkamilifu wa watu kutoka katika mataifa mbali mbali katika mchakato wa ujenzi, ustawi na maendeleo ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Serikali inatambua na kuthamini umoja na utofauti unaofumbatwa katika maisha ya wananchi wake, changamoto ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Waziri Sultani

 

01 February 2019, 17:11