Watu wa Afrika ya Kati wanahitaji msaada wa dola milioni 340 kwa mwaka 2019!
Sr. Angela Rwezaula - Vatican
Ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) katika taarifa iliyotolewa tarehe 7 Januari 2019 huko Bangui, nchini Afrika ya Kati (CAR), imesema idadi ya watu wanaohitaji msaada na ulinzi mwaka huu imeongezeka kutoka watu milioni 2.5 hadi 2.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na mwaka 2018.
Kati ya hao ni watu milioni 1.9 wanahitaji msaada wa dharura na haraka.
Katika mantiki hiyo OCHA kwa pamoja na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), imezindua tarehe 7 Januari 2019 ombi kwa ajili ya mpango wa msaada kwa mwaka 2019, la dola milioni 430.7 kusaidia watu milioni 1.7 walio hatarini zaidi nchini hiyo. Kwa kuzingatia malengo matatu, mpango huo unatarajiwa kuokoa maisha, kuimarisha ulinzi wa watu walioathirika na kuhakikisha utu na wakati huo huo wakiwezesha uwasilishaji wa huduma muhimu za kuokoa maisha.
Ombi hilo limetolewa wakati huu ambapo hali ya kiusalama inakwenda polepole na kwa kushuhudia ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia na wafanyakazi wa kutoa misaada ambapo visa elfu moja vya kiulinzi vimeripotiwa kwa mwaka 2018. Idadi ya visa dhidi ya watoa huduma ya misaada imeongezeka kutoka watu 337 kwa 2017 hadi kufikia 396 mwaka 2018. Licha ya hali ngumu katika sekta zote, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Bi. Najat Rochdi amesisitizia juu ya hali ya kujitolea na ujasiri wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu katika kuleta matumaini kwa watoto, wanawake na wanaume waathirika wa mzozo.
Watu 900,000 wamepata msaada kwa mwaka 2018
Bi Rochd akiendelea na ufafanuzi huo amesema “Mwaka 2019, hatutaendeleza juhudi ila tutaziimarisha ili kuepukana na hali mbaya zaidi. Kwa mantiki hiyo ninatoa wito kwa wasamaria wema wasisahau nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na watuunge mkono kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza hatua za miaka iliyopita na kutoa msaada wa kibinadamu”. Mwaka 2018, Ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ( OCHA) ilipokea ufadhili wa dola 253.9 na kuwezesha uwasilishaji wa misaada kwa watu 900,000 katika mpango wa kuwasilisha misaada ya kibinadamu.