Vatican News
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa: Watanzania jengeni mabweni ili watoto wasome kwa raha! Waziri Mkuu Kassim Majaliwa: Watanzania jengeni mabweni ili watoto wasome kwa raha!  (AFP or licensors)

Watanzania jengeni mabweni watoto wasome kwa raha zaidi!

Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwa sababu wataishi hapa, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wananchi kwenye Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa washirikiane kujenga mabweni katika shule ya sekondari Mnacho ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembelea umbali mrefu kwenda shuleni hapo. Ameyasema hayo Jumatatu, Novemba 19, 2018 wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni, ambalo ujenzi wake unagharimu sh. milioni 92.4 ikiwa ni mchango uliotolewa na wadau wa elimu.“Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwa sababu wataishi hapa, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio katika Kata hiyo na za jirani washirikiane na kuanzisha mradi wa ujenzi wa mabweni mengine kwa kuwa hilo moja lililojengwa na wadau halitoshi kulingana na idadi ya wanafunzi. Amesema yeye yuko tayari kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata yao, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za jamii inatimia.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi hao washirikiane na walimu kufuatilia maendeleo ya taaluma kwa watoto wao shuleni na kujiridhisha kama wanafanya vizuri darasani na iwapo watabaini changamoto waweze kuzitatua kwa pamoja. Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo, Mkuu wa shule ya sekondari Mnacho, Mwalimu David Mwakalobo amesemma ujenzi wa bweni hilo lenye uwezo kulaza wanafunzi 80 ulianza Septemba 19, 2018 na unatarajiwa kukamilika Januari, 2019. “Kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni bweni hili litakidhi mahitaji ya kuwalaza wanafunzi wa kike tu. Tunaendelea kuwaomba wahisani waendelee kutusaidia ili tupate bweni lingine kwa ajili ya kuwalaza wanafunzi wa kiume.”

Mwalimu Mwakalobo amesema iwapo watafanikiwa kuwa na mabweni ya kuwalaza wanafunzi wote 334 shuleni hapo yatawasaidia katika kutatua changamoto ya utoro na mdondoko wa kitaaluma kwa wanafunzi kwa sababu wengi wanatoka mbali. Pia mradi wa ujenzi wa mabweni utasaidia walimu kuwa karibu na wanafunzi wakati wote, hivyo kupata muda mwingi wa kuwasaidia wanafunzi kimasomo kwa sababu watakuwa wanaishi shuleni. “Mradi huu pia utapunguza wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito.” Ameongeza kuwa uwepo wa mabweni shuleni hapo utaongeza ari ya wanafunzi kupenda shule tofauti na hali ilivyo sasa kwa sababu wengi wanalazimika kutembea muda mrefu kwa kuwa wanatoka vijiji vya mbali, jambo linalowafanya wasipende shule.

19 November 2018, 14:29