Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Hotuba Elekezi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Makardinali wapya, Jumatano tarehe 4 Oktoba, Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Baadaye jioni Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu pamoja na Kardinali Jean-Claude Holleric, Mwezeshaji mkuu wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu walitoa hotuba za ufunguzi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwenye Ukumbi wa Sinodi. Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu amesema, Kanisa ni Jumuiya ya wafuasi wamisionari ambao huchukua hatua ya kwanza, ambao wanajihusisha na wanasaidia juhudi ambazo huzaa matunda ya kufurahi. Jumuiya inayoinjilisha inatambua upendo wa Kristo na inatumwa kwa ushupavu kwenda kwa wengine, kuwatafuta wale walioanguka, kuwakaribisha waliotengwa sanjari na kuonesha nguvu ya huruma ya Baba wa milele isiyokuwa na kikomo! Rej. Evangelii gaudium 24.
Upendo wa Mungu unaganga na kuponya mapungufu na madhaifu ya binadamu na kwamba, huu ndio utume wa Kanisa linalopaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa upendo huu wa Mungu. Hatua ya kwanza ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliwahusisha watu wa Mungu katika hatua za awali na hivyo Kanisa limejifunza kutembea kwa pamoja katika umoja ili kujenga Kanisa la Kisinodi linalosikiliza kwa makini, huku wakiwa wameunga na Maaskofu wao chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha ushirika wa Kanisa, moja, takatifu, katoliki la mitume. Huu ni umoja na ushirika wa watu wa Mungu pamoja na viongozi wao wakuu, ushirika unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti, ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu, ili kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Kumbe, Sinodi hii ni kielelezo cha umoja waamini, umoja wa Mama Kanisa na umoja wa kihierakia. LG 1. Huu ni umoja unaosimikwa katika tofauti msingi za: Miito, utume, hali ya maisha, amana na utajiri, karama na zawadi mbalimbali kutoka kwa Roho Mtakatifu. Sinodi hii ni chombo cha umoja na huduma kwa Kanisa na kwa ulimwengu katika ujumla wake!
Kwa upande wake, Kardinali Jean-Claude Holleric, Mwezeshaji mkuu wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu amejikita katika hati ya kutendea kazi, matunda ya ushiriki wa watu wa Mungu kuanzia mwaka 2021 wakiwa wanatembea na Kristo Yesu ndani ya Kanisa lake, kielelezo cha umoja na ushirika wa watu wa Mungu katika ujumla wao, tayari kumwimbia Mwenye Mungu wimbo wa sifa na utukufu, Laudate Deum, changamoto ya toba na wongofu wa ndani. Huu ni wakati kwa Mababa wa Sinodi kujifunza dhana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi maana kwa Ubatizo, waamini wanawekwa wakfu na hivyo huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha urika wa Maaskofu pamoja na Ukuhani wa waamini wote. Hati ya kutendea kazi ni matunda ya mchakato wa mang’amuzi ya Sinodi inayoyoendelea, kwa kujikita katika sala na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kazi za Makundi ya lugha ni kunogesha majadiliano katika roho ili kujenga umoja na ushirika tayari kupyaisha maisha na utume wa Kanisa.