Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu mkuu Mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora Tanzania: Jengeni utamaduni wa umoja na mshikamano kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Ufalme wa Mungu Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu mkuu Mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora Tanzania: Jengeni utamaduni wa umoja na mshikamano kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Ufalme wa Mungu  (ANSA)

Kardinali Protase Rugambwa: Jengeni Utamaduni wa Umoja na Mshikamano Na Wote

Kardinali Protase Rugambwa awataka watanzania wawe tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano na watu wengine hata ambao si watanzania kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni mwaliko wa kuendelea kujifunza kujenga umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, ili watu wote waweze kufurahia maisha na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Anasema, Tanzania kumenoga! Karibuni Nyote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ni katika asili ya watu wa Mungu, Roho Mtakatifu ametenda kazi ya kutangaza na kushuhudia Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu, Fumbo ambalo limewafikia watu wa Mataifa katika lugha zao za asili, kupitia kwa wazazi, makatekista, mapadre, wamisionari bila kuwasahau mabibi na mababu. Makardinali wapya wanaitwa na kutumwa kuwa ni wainjilishaji, kwani wao wameinjilishwa kwanza, tayari kupyaisha kumbukumbu na zawadi ya imani. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia zaidi uwakilishi wa Makardinali toka sehemu mbalimbali za dunia, kama ilivyokuwa siku ile ya Pentekoste ya kwanza, hawa ni Makardinali na Maaskofu wa nyakati hizi, ili kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; tayari kusimama kidete na kuwa ni wainjilishaji, huku wakimwilisha ndani mwao, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuendelea kumwaminia Roho Mtakatifu anayetengeneza utofauti na umoja; kiongozi mpole na thabiti.

Makardinali wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa uinjilishaji mpya.
Makardinali wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa uinjilishaji mpya.

Mara baada ya Ibada ya kusimikwa kwa Makardinali wapya, Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Italia, ilimkaribisha Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora kwa hafla ya “kufa mtu.” Hii ni hafla iliyohudhuriwa na baadhi ya Maaskofu walioandamana na Kardinali Protase Rugambwa kutoka Tanzania pamoja na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya Italia. Mama yake Kardinali Protase Rugambwa ni kati ya waamini waliokuwa wamesheheni furaha kutoka katika sakafu ya moyo wake tarehe 30 Septemba 2023, aliposhuhudia Askofu mkuu mwandamizi Protase Rugambwa, akiwa miongoni mwa Makardinali wapya waliosimikwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Mama Immakulata anakiri kwamba, kwa hakika, hii imekuwa ni siku yake ya furaha tangu kuzaliwa kwake, anaendelea kuamini uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yake na kwamba, Mwenyezi Mungu amemtendea makuu na jina lake lihimidiwe. Hakutegemea kwamba, angeweza kumzaa mtoto ambaye baadaye amekuja kuwa ni Kardinali na hivyo kuheshimishwa ulimwenguni kote! Anamshukuru Bikira Maria na anamwomba, aendelee kumwombea Kardinali Protase Rugambwa ili awe na nguvu, imani thabiti na upendo kwa watu wote wa Mungu. Anawaombea akina mama wote waendelee kujikita katika malezi na makuzi bora ya watoto wao na wawapatia nafasi ya kujiunga na seminari ili hatimaye, waweze kumtumikia Mung una jirani zao kama Kardinali Protase Rugambwa. Wampende Mwenyezi Mung una kudumu katika ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora
Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora

Kardinali Protase Rugambwa katika hotuba yake amewashukuru wote waliobahatika kujumuika kumpongeza pamoja na kumtakia heri na fanaka katika maisha na utume wake, tangu siku ile Baba Mtakatifu Francisko alipotia nia ya kuwatangaza Makardinali wapya ishirini na moja. Kwa hakika, wamekuwa ni msaada mkubwa kwake: kiroho, kimwili na ki-hali. Kardinali Protase Rugambwa, anamshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na Baba Mtakatifu kwa yote anayomtendea katika maisha yake. Anawashukuru wale wote waliofika mjini Vatican kuhudhuria tukio hili kubwa katika historia ya maisha na utume wake na hivyo kuongeza nguvu katika Kanisa kwa kuwa ni wasaidizi na washauri wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Protase Rugambwa, anawaomba watu wa Mungu kuendelea kumkumbuka na kumwombea, ili sala zao ziendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora na kama Kardinali. Ameishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Italia na kuwataka watanzania kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, mambo msingi yanayowatambulisha watanzania, licha ya tofauti zao msingi. Wawe tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano na watu wengine hata ambao si watanzania kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni mwaliko wa kuendelea kujifunza kujenga umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, ili watu wote waweze kufurahia maisha na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Kardinali Protase Rugambwa, ametumia fursa hii, kuwakaribisha watu wote wa Mungu nchini Tanzania kwani “ati nyumbani kumenoga.”

Rais Samia Suluhu Hassan amemtumia Kardinali Protase Rugambwa, salam
Rais Samia Suluhu Hassan amemtumia Kardinali Protase Rugambwa, salam

Wakati huo huo, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametuma salam za pongezi za dhati kwa Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa kwa kusimikwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali. Kauli mbiu ya utume wake wa kikardinali ni "Euntes in Mundum Universum", yaani “Enendeni Ulimwenguni Mwote” Mk 16:15, juu ya utume unaojali watu wote, sehemu zote na wakati wote. Rais Samia ameungana na watanzania wote kumwombea Kardinali Protase Rugambwa kheri, afya njema na mafanikio katika utumishi wake. Salam hizo za pongezi zimetolewa na Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia na kwamba, Rais Samia anatoa pongezi za dhati kwa kusimikwa Kardinali Protase Rugambwa, ambaye anaandika historia kwa kuwa ni Kardinali wa tatu kutoka Tanzania.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia
Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia

Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kwamba, viongozi wa dini ni sehemu muhimu sana ya jamii katika muktadha wa ukuaji, ustawi na maendeleo nchi sanjari na utambulisho wa wananchi husika. Amemtakia Kardinali Protase Rugambwa heri na baraka tele katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora. Amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kuandaa “halfa hii ya kukata na shoka”. Kwa namna ya pekee amewapongeza watanzania kwa moyo wa uzalendo, moyo wa sadaka na majitoleo sanjari na kuendelea kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa watanzania kitaifa. Amewasihi viongoni wa Kanisa waendelee kuliombea Taifa la Tanzania na viongozi wake ili waweze kutimiza malengo na ahadi zote za maendeleo kwa watanzania. Na kwa upande wa viongozi wa Kanisa, waendelee pia kutekeleza ahadi zao kwa Kanisa. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kwamba, huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika katika ujumla wake.

Kardinali Protase Rugambwa
02 October 2023, 15:12