Jenerali Mabeyo ndani ya Studio za Radio Vatican:Maisha yetu yana misingi ya lazima!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Alhamisi tarehe 18 Mei 2023 wakati mjini Vatican ilikuwa inaadhimishwa siku ya Kupaa kwa Bwana, Maaskofu Katoliki wa Tanzania, wakiwa katika hija yao ya kitume mjini Roma kuanzia tarehe 14 -21 Mei, walishiriki Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta Roma, iliyoongozwa na Askofu Mkuu Beatus Kinyaia jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Tanzania. Mara baada ya Misa hiyo, Studio za Radio Vatican zilipata mgeni maarufu kutoka Tanzania. Kwa hiyo Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inayofuraha kubwa kukuletea mahojiano maalumu kabisa na mgeni huyo. Yafuatayo ni mahojiano yote kamili:
Ndani ya Studio zetu za Radio Vatican, tunaye Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, anayejulikana sana, na ni Mkuu wa Majeshi mstaafu wa Tanzania ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa nane wa Majeshi ya Ulinzi kwa kuliongoza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lijulikanalo (JWTZ). Lakini pia ndani ya studio hizi tunaye Major Adam John Minzi msaidizi wake. Jenerali Mabeyo aliteuliwa na Rais John Magufuli mnamo tarehe 6 Februari 2017. Na baada ya kifo cha Rais Mpendwa John Pombe Magufuli mnamo Machi 2021, Jenerali Mabeyo alichukua jukumu kubwa sana la kuhakikisha mpito mzuri wa madaraka kwa Rais mpya, Mama Samia Suluhu Hassan. Alistaafu shughuli hiyo mnamo Juni 2022. Na kabla ya mwaka kuisha, yaani mwezi Juni ijayo tangu kustaafu kwake tunayo bahati kubwa sisi hapa kuwa naye ili kuzungumza machache katika Studio za Radio ya Papa. Karibu sana na… Unaweza kuwaeleza wasikilizaji wetu awali ya yote ni kitu gani kimekuleta katika mji wa milele?
Kwanza ninasema tunashukuru sana, Radio Vatican kwa kunikaribisha hapa, angalau kuongea na ninyi na kupitia ninyi na wasilizaji wote wa Radio Vatican watakuwa wanasikiliza tunayoyaongea. Kilichonileta hapa, labda niseme tu ni bahati ambayo nimepewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambao waliona mimi ni wasindikize katika hija yao hapa Roma, sasa sijuhi walizingatia nini, katika kuniteua, lakini ni faraja kwamba mimi ninawawakilisha walei wote wakatoliki, kwa ajili ya kuwasindikiza hao Maaskofu wetu; lakini vile vile nikiwawakilisha walei wote Tanzania kwa ajili ya kushiriki nami hija ya maaskofu.
Mkiwa mko karibu kumalizia hija yenu maana tangu mmeanza kufika mmetembelea mabaraza mbali mbali ukiwa na hawa maaskofu, je ni kitu gani ambacho kimegusa zaidi?
Katika hija hii kwakweli imenifanya nifarijike, nifarijike kiroho kwamba ninazidi kuwa karibu na mwenyezi Mungu kwa sababu maeneo mengi, maaskofu wameyajadili, maeneo yanayogusa maisha yetu ya kila siku, si kwa wakatoliki tu bali kwa watu wote. Na ndio maana wanatusisitiza huku katika kuimarisha jumuiya ndogo ndogo. Jumuiya ndogo ndogo ndiyo wanasema ya kwanza ukiacha familia, kwa sababu familia ndio tunasema ni Kanisa la mwanzo. Lakini Jumuiya ndogo ndogo, tunakuwa na watu wa aina tofauti, tofauti kwa hiyo tunaimarishana kiroho, lakini pia tunaimarishana, kijamiii, kichumi nk. Sasa hii imekuwa ni nafasi nzuri sana kwa sababu maaskofu wamekuwa wakijaribu kuelezea ni nini maisha yetu katika Jumuiya. Ni nini maisha yetu kikanisa, nini nini maisha yetu kijamii kwa ujumla kwa maana ya Taifa lote la Tanzania. Kwa hiyo mimi imenipa faraja kubwa sana kwa sababu yale ambayo pengine yalikuwa yananitatiza sasa yanapata majibu. Ninashukuru sana kwa nafasi na fursa niliyopewa.
Kwa namna moja au nyingine umestaafu hivi karibuni lakini vile vile ukapewa tena majumu mengine na Serikali. Ni namna gani ya kuunganisha vitu viwili, yaani kubaki katika imani ya kikatoliki na juu ya shughuli zako?
Mimi ninaona kama utofauti ni mdogo sana kwenye jamii kuna misingi yake, kwenye ukatoliki kuna misingi yake, lakini misingi ya kikatoliki haipishani na misingi ya kijamii ya kila siku. Maisha yetu yana misingi yake ya lazima, na miiko yetu lazima uifuate, sasa hii ukiwa muumini na imani yako ya dini, pengine sio katoliki lakini hata dini nyingine zote. Ukiwa na misingi ile imara, hata utendaji wake wa kila siku utaimarika zaidi, kwa sababu utakuwa unaoanisha misingi ya dini inakukataza nini, na kukuruhusu nini; na misingi ya kazi inakuzuia nini na inakuruhusu nini, ukiyaoanisha pomoja unaimarika zaidi. Mimi nina imani kabisa kuwa hapa ninaimarika zaidi. Ni kweli kabisa, kwa hiyo kuunganisha kazi na sala, kwa kuchukulia ile ya Mtakatifu Benedikto “Ora et Labora”, yaani “Kazi na Sala”. Ni masuala yanayokwenda pamoja na ambayo hayawezi kupisha kimoja na kingine. Hata Mtakatifu Yosefu ni mfanya kazi lakini kwa sababu ya sala zake ziliweza kumsaidia katika kuimarisha kazi yake, kwa sababu ya sala hizi alizokuwa anasali.
Ijumaa tarehe 19 Mei 2023 mtakutana na Baba Mtakatifu Francisko, ni hisia gani unayo na kitu gani ambacho unafikiri kwamba utakapokutana naye kumsikiliza na kumwona?
Ni kubwa Sana, ni matarajio makubwa kwamba nitakapoonana naye, moyo wangu mimi labda siku moja na mimi ninaweza kuitwa Mtakatifu. Yeye ni Kiongozi mkubwa wa dini yetu katoliki katika dunia. Miongozo yote ya ukatoliki inatoka hapa lakini hata mabadiliko yanayotokea mara kwa mara yanatengezwa katika makao makuu hii, yakiongozwa na Baba Mtakatifu. Hakuna kitu kitakachofanyika cha kikatoliki ambacho hakijapitishwa na Baba Mtakatifu. Mimi ni faraja kumwona kwa maana sijawahi kumuona. Nilikuja hapa mwaka jana, tukatarajia labda tungepata siku moja hata ya kumpungia mkono, hatukuweza kupata hiyo fursa, safari hii tumepangiwa ratiba, lakini ni matarajio yetu na tunaendelea kumuomba Mungu aimarishe afya yake siku hiyo Ijumaa(tarehe 19 Mei 2023) ambayo ni kesho, basi tuweze kupata hiyo nafasi kwa sababu hiyo ni nafasi ya pekee, wengine nyumbani, wanaiita ni upako, ukiupata unafarijika kwamba na mimi nimesafishika katika kuonana na Baba Mtakatifu. Na mimi ninasema asanteni sana kwa kuniruhusu kuja huku Vatican, ninawashukruni tena zaidi, Mababa Maaskofu, walisema mmoja wa Walei atakayeongozana na Mababa maaskofu basi niwe mimi, na mimi nilipokea kwa mikono mikunjufu.
Na bado Jumapili (21 Mei 2023) utakutana/tutakutana/mtakutana na umati mkubwa kutoka Tanzania, lakini wako Roma na Italia kwa ujumla, ili kuweza kusali pamoja kanisani. Ni hisia gani pia unayo kwa ujumla maana utajisikia kwamba haupo tena Italia bali utajisikia ndani ya jiji katika jumuiya ya Tanzania ukiwa Roma.
Ni faraja kubwa na nimekwishaanza hizo hisia maana kila siku tukionana na wachache, wananiuliza au wananiomba, “utusomee somo la kwanza,” nikasema mimi niko tayari. Na hii nimekuwa nikipata faraja kwa sababu kila ibada tuliyokuwa tukiifanya ya misa Takatifu kila siku asubuhi, tumekuwa na baadhi ya wanawakwaya, mimi si mwanakwaya, lakini ninapenda kwaya, na kwa bahati nzuri mke wangu ni mwanakwaya mzuri na ni mtunzi wa nyimbo za kiroho. Bahati mbaya safari hii hakuweza kuongozana na sisi, pengine kutokana na safari yenyewe, inahusu ni nini, lakini ningependa kuja naye, lakini na mimi nitarudishia upako nitaupata kwamba Mama nimeimba na wanakwaya kwa niaba yako na wanawakaya wengine.
Tuko mwezi wa Mama Maria ni ujumbe gani unawaachia wasikilizaji wetu mahali popote walipo
Mama Maria ni mwombezi wetu na wakati wote tunaposali Rosari Takatifu tunamtumia Mama Bikira Maria kama Mwombezi wetu na wakati wote wote Mama Bikira Maria amekuwa ni mwombezi wa amani na tunaweza kujikumbushe vile vile wale watoto wa Fatima alipokutana nao aliwambia wakati wote kusali Rosari Takatifu, kwa ajili ya kuiombea dunia amani na sisi tunaomba amani wakati wote. Wakati wote tumtumie Mama Bikira Maria kuomba amani ya Dunia. Tunaona wengi wanafarakana. Sisi Tanzania tumebahatika, lakini tunahitaji kutambua hilo ili amani hiyo idumu wakati wote. Na tunaona majirani zetu. Tunaona majirani zetu wanapata shida. Jirani zetu Congo, majirani zetu Burundi, majirani, Mozambique, walikuwa kila wakati wanazunguka Rwanda na maeneo mengine. Tunaona ugaidi unakuja Somalia, unatelemka Kenya, ulitaka kujaribu Kwetu Tanzania, lakini tunashukuru umoja wetu na mshikamano wetu; na mshikamano wetu umetusaidia kuhakikisha kwamba amani inadumu. Na hii ni kwa sababu ya wakati wote tunasali, kumuomba Mama Bikira Maria ambaye ni mwombezi wetu, kuhakikisha kwamba amani yetu inadumu daima. Na hilo ninawaomba watanzania wakati wote tuendelee kuomba hiyo amani. Na amani tunaitengeneza sisi wenyewe. Amani hatuwezi kuitelemshiwa tu hivi hivi. Ni sisi, lazima tuhakikishe kwamba tuna amani. Mnajua kuwa tunatofautiana kwa lugha katika mawazo kupitia vikundi mbali mbali, kupitia wanasiasa, na hapo mnapotofautiana mnashindwa kuzungumza na kuelewana, na mnaishia kugombana. Sasa tunasema kwamba tutofautiane kwa mawazo, lakini tupate suluhisho kwa amani. Njia ya kupigana sio suluhisho kwani mnaingia kwenye shida, watu wanaingia kwenye shida, watu watabaki na vilema, watu watafariki. Tutakosa ile fursa tunayoitarajia kwamba Tanzania ni ya watu wenye furaha, na watu wakarimu. Mfano halisi ni Sudan, Majenerali wawili wanagombana, wanaoumia ni nyasi…
Watu wa kawaida kabisa na wanakimbi kimbia hawana mahali pa kwenda kukaa. Je watakwenda kukaa wapi? Wameacha nyumba zao, nyingine zimebomolewa, wanapata shida, lakini ni kwa sababu ya watu wawili walioshindwa kuelewana. Wana wafuasi wao na wao wanawashawishi kwamba tunatakiwa kweli tupigane. Nadhani njia ya kupigana sio suluhisho, suluhisho ni kuongea mkaelewana. Tunamwona mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, ameanzisha mazungumzo, maridhiano na vyama ambavyo finafikiria na vina mtazamo tofauti na chama kingine, sasa mkizungumza ina maana mtafika mahala na mtasema nadhani tufuate njia hii, basi vinginevyo utakuwa na tamaa ya madaraka kwamba ‘mimi lazima niwe kwa vyovyote vile, na ninyi mnatumiwa vibaya, ninyi niwajinga, sijuhi nini’…unachochea hasira, mimi ninadhani hatuhitaji kuwa na hasira, tunahitaji kusema kuwa njia unayoifanya siyo sahihi, tufanye hivi, basi. Na mkielewana mnaendelea na amani yenu.
Jana wakati mmekaribishwa ubalozi wa Tanzania nchini Italia ulisema kuwa wakati unamalizia kazi uliacha nchi katika usalama… lakini siku za hivi karibuni kumeanza kuonekana uharibifu wa makanisa ya kidini nchini, kuanzia na la Geita, hivi karibuni Zanzibar na kahama, je hii kwa upande wako inasababishwa na nini?
Jana nilimsikiliza hata mheshimiwa Waziri alivyozungumza pale ubalozini, akawaomba maaskofu kuimarisha mafunzo haya, mahubiri yao wanapokuwa wanakutana na waamini. Ni jambo linalogusa wote, pengine kwamba maadili yetu yanamomonyoka au watu wamekosa muda wa kukaa na familia zao. Kwa hiyo mambo mengi yanatakiwa yaanzie kwenye ngazi ya familia. Kama kwenye familia mna maadili mema, kwa vyovyote vile familia ile itakuwa katika maadili hayo hayo. Lakini pengine huwa, tunasema namna gani huwezi kukamilika katika ngazi ya familia peke yake na ndio maana tuna taasisi tofauti tofauti. Viongozi wetu wa dini wanapotupa maadili haya ya kidini na tukayaimarisha, kuyasimamia yanatusaidia kuwa na familia bora. Lakini tukienda pia upande wa pili hata kwenye serikali vile vile kuna maadili ambayo unayakuta kule kazini, nayo ukiyazingatia yanakuimarisha kijamii kwa sababu sisi ni watumishi wa jamii na hao viongozi wa dini ni watumishi wa kiroho wanaimarisha roho zetu ili ziwe maadili mema hata katika jamii. Kwa hiyo ninachokiona kama wengine pia wanachoona kwamba haya maadili ya msingi labda tumeyaacha kuyasisitiza na tunapoyaacha yanatuletea matokeo ambayo sasa ndio tunayo yaona; matokeo ambayo pengine tumewaachia nafasi. Vyombo hivi, sasa hivi tunasema dunia ya Utandawazi, kwa sababu hakuliona nyumbani kwao, lakini ameliona kupitia vyombo vya utandawazi, anaenda kujaribu, anafikiri atanufaika. Na changamoto zingine ni za kimaisha anaona ni namna gani aondokane na changamoto ya kimaisha. Fursa zipi anaweza akazitumia, lakini sasa zingine hatuziiti fursa ni uhalifu, Yeye anafikiria ile ni fursa anakwenda, anafanya uharifu ili anufaike, lakini anavunja sheria iliyowekwa, anasabababisha taharuki katika jamii. Hiyo inatokana na changamoto tunazokutana za kimaisha. Sasa ni namna gani ya kujikomandi, unaweza ukakuta hata serikali sasa inasisitiza namna gani ya kuwajengea misingi bora vijana ya kijamii ili waweze kuwa mababa wazuri, wamama wazuri wa kutegemewa huko mbeleni. Dunia ya sasa lazima itakuwa inaendelea kubadilika sio ile tuliyoanza nayo sisi. Kwa sasa lazima vile vile kuwe na mnyumbuko wa aina fulani na namna gani dunia inakuja, tutaishi, kama tunaweza kuharibikiwa? Sasa hilo ni muhimu sana kulitazama lakini mafundisho haya ni ya msingi sana, mafundisho ya kijamii na mafundisho ya kiroho na kwa mtu mafundisho ya kiroho ni ya muhimu sana, kwa sababu ndio yanayomjengea mtu ule ustahimilivu. Wengine tunakosa ustahimilivu kwa sababu hatujajengwa katika misingi ya kustahimili, umepata shida kidogo unakata tamaa haraka au unatafuta jibu la mkato. Hakuna jibu la mkato lazima kila wakati utafakari, nifanyeje katika changamoto hii, njia zilizo wazi na njia zipi zilizo ngumu lakini zinanipeleka katika kufanikiwa. Hilo mimi ninaamini kwamba tunaweza. Ni kweli matukio mengi yametokea, lakini yametokea ni ya uharibifu, ni ya uhalifu, alitaka kupata nini.... anaenda kubomoa Kanisa, anaenda kubomoa Tabernakulo, anataka apate nini, mimi ninaliona kama kuna mapungufu fulani, lakini ndiyo tunayo ambiwa vile vile ukiwa na hizi changamoto nazo zinatengeneza ugonjwa wa akili. Kwa hiyo tunakiwa tutengeneze afya ya akili, ukitengeneza afya ya akili, ili wote wawe na uvumilivu, waweze kujitahidi, njia zinaweza zikabadilika.
Kama unalo jambo jingine la mwisho unalopenda kuwaachia wasikilizaji wetu Raradio Vatican na Radio Maria walio wadau wakubwa sana...
Tunashukuru, mimi la kwangu ni hilo: tudumu katika sala, tuendelee kumtumainia Mwenyezi Mungu kwamba yeye peke yake ndiye mwamuzi wa yote. Hakuna mtu mwingine sisi tutakuwa na utashi wetu, lakini mwenyezi Mungu ndiye mwenye utashi pekee. Tuendelee kumtumaini yeye daima. Lakini mwisho kabisa kabisa niwashukuru Radio Vatican kwa kunipa hii fursa, sikuwahi kufikiria hata siku moja, huwa nasikiliza tu nikifungulia radio nasikia Radio Vatican, lakini sikuwa najua kabisa kwamba siku moja ningeweza kuja na kuongea katika Radio Vatican. Asanteni sana kwa nafasi hii mliyonipatia.
Jenerali Mabeyo alikuwa anamsindikizaji, kwa kujitambulisha, kuwasalimia na kuelezea yake ambayo yamemgusa katika ziara hii.
Ninaitwa Major Adam John Minzi, msaidizi binafsi wa Jenerali Venance Mabeyo Mkuu wa Majeshi Mstaafu. Nimshukuru Mungu kupata fursa hii. Nimemsindikiza, lakini nimefika katika nchi Takatifu, nimebarikiwa sana, kwakweli nimeona imani yangu kwa kiwango kikubwa inazidi kuongezeka kwa kufika katika mji huu ambao nimepata bahati ya kusali katika makanisa ya kihistoria, ya watakatifu. Kwa mfano leo tulikuwa na misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo, kwakweli tumebarikiwa sana, na katika safari nzima nimejifunza mambo mengi hasa yanayo tuhusu sisi walei nadhani nitakuwa balozi mzuri sana, hasa katika suala linalo tuhusu sisi walei. Ikumbukwe katika Ziara ya Kitume ya Maaskofu (TEC), mjini Vatican na ambao walikutana na Baba Mtakatifu tarehe 19 Mei, inahitimishwa na Misa Takatifu tarehe 21 Mei 2023 ambayo itatangazwa mbashara na Radio Maria, kuwapatia fursa ya kushiriki tukio hili muhimu kwa Kanisa la Tanzania.