Daraja Takatifu ya Ushemasi Ni Mlango wa Huduma Kwa Kanisa
Na Padre Karoli Joseph Amani, - Vatican.
Huduma ya Kanisa iliyowekwa na Mungu hutimizwa kwa daraja mbalimbali na wale ambao tangu zamani waliitwa maaskofu, mapadre na mashemasi. Mama Kanisa anakiri na kufundisha kwamba kuna ngazi mbili za kushiriki huduma ya ukuhani wa Kristo: Uaskofu na Upadre. Ushemasi umewekwa ili kuwasaidia na kuwatumikia maaskofu na mapadre. Ndiyo sababu neno “Sacerdos” yaani “Kuhani” katika matumizi ya sasa humaanisha maaskofu na mapadre, lakini siyo mashemasi. Hata hivyo mafundisho ya imani Katoliki hufundisha kwamba ngazi za kushiriki ukuhani (uaskofu na upadre) na ngazi ya huduma (ushemasi) zote tatu hutolewa kwa tendo la Kisakramenti liitwalo “kutoa Daraja,” yaani Sakramenti ya Daraja: Wote wawaheshimu mashemasi kama Kristo Yesu, pia askofu kama sura ya Baba na mapadre kama Baraza la Mungu na kama kusanyiko la mitume: bila wao haiwezekani kuongea juu ya Kanisa. Rej. KKK 1554. Kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2023, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwakilishi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 29 Aprili 2023 ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Mashemasi 28 kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kati yao akiwemo Shemasi Renovatus Edward Mugisha kutoka Jimbo Katoliki la Kayanga, Tanzania.
Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle katika mahubiri yake amesema katika Sakramenti ya Daraja Takatifu, Ushemasi ni ngazi ya huduma inayoelekezwa katika kuwasadia maaskofu, mapadre na waamini walei. Hivyo neno “Sacerdos” haliwalelekei mashemasi. Kwa daraja ya ushemasi, shemasi anafananishwa na Kristo Yesu aliyejifanyiza shemasi kwa huduma yake kwa watu wote. Watarajiwa wa ushemasi huingizwa katika utume mtakatifu kupitia mlango wa daraja hiyo ya ushemasi- diakonia yaani huduma. Daraja hiyo ni mlango wa huduma ambayo hata hivyo haupaswi kufungwa baada ya kupata Daraja Takatifu ya Upadre. Mlango huo kimsingi ni Kristo Yesu Mwenyewe aliye njia, ukweli na uzima. Akifafanua Maandiko Matakatifu, Kardinali Tagle alisisitiza mambo mawili muhimu mintarafu ushemasi. Kwanza ni kwamba, Kristo Yesu aliwaitwa Mitume ili wakae naye na baadaye waweze kutumwa (Marko 3:13-19). Katika kukaa na Yesu, Mitume walisikiliza mafundisho yake, walishuhudia matendo yake, walipokea masahihisho aliyowapatia na kuona jinsi watu walivyompokea, hivyo wafuasi walifanikiwa siku kwa siku kumfahamu vizuri na kumfuata. Kama wafuasi hata waamini wanapaswa kukaa na Yesu na kumfuata.
Kardinali Tagle alionya kwamba katika ulimwengu mamboleo bila shaka watajitokeza watu, vitu na mazingira fulani hatari ambavyo vinaita kukaa navyo na kubaki navyo. Umaarufu, fedha na fahari nyingine za dunia vinawaita na kualika kukaa navyo na kubaki navyo kuliko kukaa na kubaki Kristo. Aliye mfuasi wa Kristo akipokea mwaliko wa aina hiyo hataweza tena kumtumikia Kristo wa kulihudumia Kanisa la Mungu. Shemasi wa Kanisa Katoliki hapaswi kabisa kupokea mwaliko wa namna hiyo, kwani ikiwa anaukubali na kuyachagua mambo hayo basi atakwenda mbali Yesu na atalidhoofisha Kanisa. Pili, kukaa na Kristo humaanisha kukaa katika mwili wake yaani, Kanisa. Kadiri ya Mtume Paulo (Waefeso 4: 11-13) kukaa na Yesu hakumaanishi uwepo mgando (baridi) ndani ya kundi. Bali ni uwepo ule unaoangazwa na Roho Mtakatifu aliye mtoaji wa mapaji mbalimbali kwa waamini. Mapaji hayo yanabeba lengo mahususi ambalo ni kujenga Fumbo la mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hilo huwezekana kama waamini huenenda katika unyenyekevu na umoja. Wafuasi wanapofanya mashindano wao kwa wao, ni ishara kwamba wanachokifanya ni kujihudumia mwenyewe badala ya Mungu na Kanisa. Katika somo la kwanza (Matendo ya Mitume 6: 1-7b) waamini wamepewa mfano wa mshikamano katika utume baina ya Mitume na Mashemasi saba waliojaa Roho Mtakatifu na hekima. Matunda mazuri ya mshikamano huo ni kwamba; Kanisa (mwili wa Kristo) likajengwa na wafuasi wa Kristo wakaongezeka maradufu. Basi, waamini wafungue mioyo kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya kulijenga Kanisa la Kristo Yesu. Daima wakumbuke kwamba hakuna mashiko yoyote kuwazia kujitengenezea mnara binafsi na kuwaonea wivu wengine kwa kutazama vipaji vyao kama tishio dhidi utume na umaarufu wa baadhi ya watu ndani ya Kanisa. Kila mwamini anavyo vipaji, lakini pia kila mmoja wao anavihitaji vipaji vya wengine kwa ajili ya kufakisha utume wake na hivyo kuujenga mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle alihitimisha mahubiri yake kwa kuwahimiza watarajiwa wa ushemasi “Litumikieni Kanisa katika unyenyekevu na furaha.”
Sherehe za kumpongeza Shemasi Renovatus Edward Mugisha kutoka Jimbo Katoliki la Kayanga, Tanzania, zilifanyika katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana zikihudhuriwa wa umati mkubwa wa watanzania waishio Roma akiwemo Mhashamu Askofu Mkuu Protase Rugambwa na ujumbe kutoka ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ukiongozwa na Bi. Jubilata Shao (Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia) ambaye alimwakilisha Balozi wa Tanzania nchini Italia Bw. Mahmoud Thabit Kombo, ambaye alihudhuria Ibada ya Misa Takatifu ulipotolewa daraja ya ushemasi na kulazimika kwenda kwenye majukumu mengine. Monsinyo Gilbert Ndyamukama aliwasilisha kwa Shemasi Renovatus Edward Mugisha salamu na pongezi kwa niaba ya Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga. Aidha, awashukuru wote kwa kushirikiana katika maandalizi ya shangwela kwa ajili ya Shemasi Mugisha anayesubiriwa jimboni Kayanga kama mpira wa kona. Sanjali na pongezi kwa shemasi mpya, Askofu Mkuu Protase Rugambwa aliwaasa wanajumuiya ya watanzania waishio Roma kudumisha ushirikiano katika matukio muhimu yanayowagusa wanajumuiya. Aliwashukuru kwa ushirikiano kwa kipindi chote alipokuwa akiishi nao mjini Roma na pia kuwakaribisha mahali anakoelekea sasa kiutume yaani nchi ya asali na maziwa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Vilevile, Askofu mkuu Protase Rugambwa aliwasihi watanzania waishio Italia kuendeleza na kuimarisha ushirikiano mzuri na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwani kimsingi ndiko nyumbani kwao wanapokuwa Italia. Mashemasi 28 kutoka Afrika na Asia, nchi 16 tofauti. Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwakilishi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, akishirikiana na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu aliyemaliza muda wake, ambaye sasa Askofu mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Askofu Mkuu Emilio Nappa, Katibu Mwambata, Askofu John Okoye wa Jimbo Katoliki Awgu- Nigeria na Askofu Bruno Ateba wa Jimbo Katoliki Maroua-Mokolo Cameroon.