Siku ya Wavuvi Duniani kwa Mwaka 2021: Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Siku ya Wavuvi Duniani kwa Mwaka 2021: Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Siku ya Wavuvi Duniani 2021: Utu, Heshima Na Haki Msingi Za Binadamu

Sekta ya uvuvi ni muhimu katika kukuza uchumi na kama sehemu ya maboresho ya lishe bora. Lakini inakabiliwa na uvunjivu mkubwa wa haki msingi za binadamu, hali ambayo imekuzwa zaidi kutokana na UVIKO-19. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2020, wavuvi 24, 000 wamepoteza maisha yao kutokana na ajali kazini, huu ndio unaojulikana kama uvuvi wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wavuvi Duniani huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba. Kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa kunako mwaka 1998. Lengo ni kuwaenzi wavuvi wanaotekeleza wajibu wao katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, wanachangamotishwa kuwa makini katika matumizi ya rasilimali iliyoko majini, ili iweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika ujumbe wake kwa Siku ya Wavuvi Duniani kwa Mwaka 2021 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusima kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wavuvi pamoja na familia zao. Itakumbukwa kwamba, Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” lakini unajulikana zaidi kama “Stella Maris” ulianzishwa na waamini walei, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko hapo tarehe 4 Oktoba 1920, kwa kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Huu ni utume ambao umekuwa ni msaada mkubwa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao katika masuala ya: maisha ya kiroho, kiuchumi na kisaikolojia. Ndiyo maana Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini!

Sekta ya uvuvi ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kama sehemu ya maboresho ya mchakato wa lishe bora. Lakini hii pia ni sekta ambayo inakabiliwa na uvunjivu mkubwa wa haki msingi za binadamu, hali ambayo imekuzwa zaidi kutokana na janga kubwa la maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2020, wavuvi 24, 000 wamepoteza maisha yao kutokana na ajali kazini, huu ndio unaojulikana kama uvuvi wa kifo. Kumbe, huu ni mwaliko kwa wadau wote kuhakikisha kwamba, wanaboresha hali ya usalama kazini na mazingira ya kufanyia kazi. Wapewe ujira unaokidhi mahitaji msingi ya familia zao. Sekta ya uvivu inakabiliwa na changamoto ya utekaji nyara unaofanywa na watu wasiojulikana; wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya! Vatican inapenda kukazia umuhimu wa kujizatiti kikamilifu katika kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Yote haya yakiheshimiwa, kipaji cha ubunifu; umoja na mafungamano ya kijamii yataendelezwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa hakika bila ya mchango wa wavuvi na mabaharia, ulimwengu ungekufa kwa baa la njaa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, zaidi ya theluthi mbili ya samaki wote duniani wamevuliwa kupita kiasi au wanavuliwa wote na zaidi ya theluthi moja wako katika hali ya kupungua kwa sababu ya vitu kama kutoweka kwa makazi ya samaki, uchafuzi na ongezeko la joto duniani.  FAO inasema siku ya uvuvi duniani inasaidia kutanabaisha umuhimu wa sekta hiyo kwa maisha ya binadamu, viumbe vya majini, na maisha yanayoyasaidiwa ndani na nje ya maji iwe katika mito, maziwa na bahari. FAO inasema samaki wana mchango mkubwa katika uhakika wa chakula duniani na ni muhimu kwa lishe bora ya watu wote ulimwenguni hususani kwa jamii zinazoishi karibu na mito, pwani na kwenye vyanzo vingine vya maji. Jamii nyingi za wavuvi sio tu zinategemea samaki kwa ajili ya uhakika wa chakula bali pia na ajira na kipato. Na hii ndio maana FAO inasema makazi mengi ya wavuvi yako katika maeneo ya karibu na bahari, maziwa au mito. Mbali ya umuhimu wa maji kwa ajili ya kuishi na kama njia ya usafiri shirika hilo linasema maji hayo ni muhimu kwa uvuaji wa samaki ambao ni chanzo cha protini mwili.

Athari katika uvuvi na jinsi ya kuzikabili: FAO inasema ukaribu huo wa watu katika vyanzo hivyo vya maji umesababisha athari kubwa za uchafuzi wa mazingira ya bahari, maziwa na mito na maeneo ya pwani kutokana na shughuli za kibinadamu na viwandani. Na hii imesababisha kupungua kwa akiba ya samaki na kuwalazimu wavuvi kwenda mbali zaidi ya maeneo waliyoyazowea kuweza kupata samaki. FAO inaonya kwamba endapo hatua madhubuti na za pamoja zisipochukuliwa sasa mgogoro huo unaweza kusababisha athari kubwa kwa siku za usoni. Maadhimisho ya Siku ya Wavuvi Duniani yasaidie kuleta suluhu za matatizo na changamoto zinazowakabili wavuvi pamoja na familia zao. Wavuvi wadogo wadogo wanatoa ajira kwa asilimia 90% ya watu wanaojihusisha na masuala ya uvuvi. Asilimia 65% ya uvuaji wote unafanyika katika nchi zenye kipato cha chini na upungufu wa chakula.

Siku ya Wavuvi 2021
23 November 2021, 15:08