Jukwaa la Kazi la Laudato si nchini Australia Tamko la Haki na Amani kwa mwaka 2021-2022: Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Jukwaa la Kazi la Laudato si nchini Australia Tamko la Haki na Amani kwa mwaka 2021-2022: Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. 

Jukwaa la Kazi la Laudato si: Kilio cha Dunia Mama na Maskini!

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limetoa Tamko la Haki na Amani kwa Mwaka 2021-2022: “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini” Umuhimu wa toba na wongofu ili kubadili: akili, nyoyo na tabia za watu. Hii ni changamoto inayochota utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kitaalimungu na Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na busara ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kama sehemu ya mchakato wa kufunga rasmi maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si”, tarehe 25 Mei 2021, Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kuzinduliwa kwa Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, safari shirikishi ya miaka saba, kama sehemu ya mchakato wa kujizatiti kikamilifu katika maendeleo na ikolojia fungamani. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kila mtu akichangia kadiri ya nafasi na uwezo wake. Ni mwaliko wa kushirikishana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuanzisha majadiliano mapya kuhusu namna ya kuujenga mustakabali wa dunia hii, kwa kuwahusisha watu wote kwa sababu changamoto za mazingira zinawahusu na kuwaathiri watu wote.

Vipaji vya kila mmoja na ushiriki wake vinahitajika kama vyombo vya Mungu kwa ajili ya kuyatunza maumbile, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake. Rej. “Laudato si”, 14. Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, linatekelezwa katika kipindi cha miaka saba. Mwaka wa kwanza ni mchakato wa ujenzi wa jumuiya, ushirikishanaji wa rasilimali na utengenezaji wa sera na mikakati ya utekelezaji kadiri ya mwono wa ikolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ikolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ikolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Mwaka wa Saba, utatumika kumsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Kazi ya Uumbaji.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limetoa Tamko la Haki na Amani kwa Mwaka 2021-2022: “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini” Maskofu wanasema, kuna haja kwa familia ya Mungu kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kubadili: akili, nyoyo na tabia za watu. Hii ni changamoto inayochota utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kitaalimungu na Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na busara ya watu wa Mataifa. Tamko la Haki na Amani kwa Mwaka 2021-2022: “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini” linatoa msingi na umuhimu wa juhudi za waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Juhudi hizi zinakwenda sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii.

Hili ni tamko linalozama zaidi katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wanapaswa kuiangalia kazi ya Uuumbaji kama Kisakramenti, ili kuendelea kushangaa na kufurahia uzuri kwa kazi ya Uumbaji. Maaskofu wanakazia zaidi toba na wongofu wa ndani, ili kupata mwelekeo mpya wa maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na kushikamana na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa utekelezaji wa Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, safari shirikishi ya miaka saba, kama sehemu ya mchakato wa kujizatiti kikamilifu katika maendeleo na ikolojia fungamani. Malengo yaliyoko mbele yao kwa sasa: Ni kusikiliza na kujibu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini”. Umefika wakati wa kuibua sera na mikakati ya uchumi wa ikolojia; mfumo wa maisha ya fungamani; tasaufi na elimu ya kiikolojia; Mafungamano ya kidugu na ushiriki wa watu wa Mungu katika utekelezaji wake kwa vitendo.

Kwa namna ya pekee kabisa, Tamko la Haki na Amani kwa Mwaka 2021-2022: “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini” ni mwaliko kwa waamini wa Kanisa Katoliki pamoja na familia zao; Jumuiya za waamini pamoja na vyama na mashirika ya kitume kusikiliza na kutafakari misingi ya taalimungu inayodadavuliwa kwenye Tamko la Haki na Amani kwa Mwaka 2021-2022: “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini”, ili hatimaye, kutekeleza kwa vitendo Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”. Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Australia ni rejea makini itakayowasaidia waamini katika safari ya miaka saba kama sehemu ya utekelezaji wa Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP.” Hii ni safari fungamani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jukwaa hili ni muhimu sana katika kuelimisha mwingiliano kati ya binadamu na mazingira yanayopaswa kuheshimiwa, kutunzwa na kuendelezwa, ili kukuza haki ya mazingira. Kwa hakika, Kanisa linaendelea kujipambanua kuwa ni mtetezi wa mazingira nyumba ya wote.

Tamko Australia

 

 

16 August 2021, 15:57