Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa Siku 10 za Kuombea Amani Duniani: Kulinda maisha kunajenga amani! Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa Siku 10 za Kuombea Amani Duniani: Kulinda maisha kunajenga amani! 

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan: Ujumbe wa Kuombea Amani 2021

Tangu wakati wa hija ya Kitume ya Mt. Yohane Paulo II, familia ya Mungu nchini Japan kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti ya kila mwaka imekuwa ikisali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Huu ni muda wa kusali na kutafakari kuhusu Injili ya amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Majadiliano katika ukweli na uwazi, yasaidie kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kunako mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan. Hii ni miji inayokumbukwa sana kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilisiginwa. Mwanadamu akaonja ukatili wa silaha za nyuklia, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano duniani. Ilikuwa ni tarehe 6 Agosti 1945 bomu la kwanza la atomiki lilirushwa mjini Hiroshima na tarehe 9 Agosti 1954 mji wa Nagasaki ukalipuliwa kwa bomu la atomiki, huu ni mwaka wa 76 tangu mabomu hayo ya atomiki yaliporushwa nchini Japan. Tangu wakati wa hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II, familia ya Mungu nchini Japan kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti ya kila mwaka imekuwa ikisali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Huu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari kuhusu Injili ya amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Majadiliano katika ukweli na uwazi, yasaidie kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema sala ni silaha nzito kwa ajili ya kusaidia mchakato wa majadiliano kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kusaidia kuenzi ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na mshikamano kama kielelezo cha amani ya kudumu. Tarehe 20 Septemba 2017 Vatican ikaridhia Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ, kwa ajili ya Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kuanzia tarehe 6-15 Agosti 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Kulinda maisha kunajenga amani.” Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, kwa nyakati mbalimbali limekuwa likitoa ujumbe kwa ajili ya kumbukumbu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Maaskofu wanasema, leo hii bado kuna vita, kinzani na migogoro mbalimbali. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Kuna vita baridi inayoendelea kati ya China na Marekani, hali inayodhohofisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linawahamasisha wadau katika mgogoro huu, kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Tarehe 22 Januari 2021, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, ulioridhiwa na Mataifa zaidi ya 50 ulianza kutumika rasmi. Huu ni Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake. Wachambuzi wa masuala ya mikataba ya Kimataifa wanakiri kwamba, Mkataba huu ni dhaifu sana kwani bado kuna idadi kubwa ya Mataifa hayajaridhia, changamoto na mwaliko kwa nchi ambazo bado hazijaridhia kufanya hivyo haraka iwezekanavyo, kwani silaha za maangamizi zinatishia usalama na amani duniani. Myanmar, Afghanstan na maeneo mengine duniani, bado kuna uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na kwamba, amani inaonekana kana kwamba, iko mbali. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa, badala ya kusingizia usalama wa Taifa na ustawi wa nchi husika.

Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, hadi kufikia tarehe 6 Agosti 2021 zaidi ya watu 4,280,666 wamekwisha kufariki dunia. Watu zaidi ya 201,724,792 wamewambukizwa na wagonjwa zaidi ya 181,478,645 wamelazwa hospitalini. Maaskofu Katoliki Japan wanasikitika kusema kwamba, huduma ya afya imegubikwa na upendeleo pamoja na maamuzi mbele na waathirika wakubwa ni maskini. Chanjo ya kinga dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 bado hijawafakia wananchi katika nchi maskini zaidi duniani. Hii ni hatari inayoweza kuendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbalimbali za dunia. Chanjo inapaswa kutolewa kwa watu wote, ili kulinda maisha ya watu wengine katika jamii. Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Japan Mwezi Novemba 2019, alikazia umuhimu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani. Aliwataka vijana kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unagusia kwa namna ya pekee kuhusu: magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni katika kulinda na kudumisha uhai wa kila kiumbe, hapo amani inaweza kuundwa na kudumishwa kikamilifu!

Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia”. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema amani ni safari ya matumaini, mwaliko kwa wananchi wa Japana kuendelea kuwajibika kulinda na kudumisha amani, umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu unaofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Maaskofu wanawataka watu wa Mungu nchini Japan kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya amani, ili amani ya Kristo iamue miyoni mwao. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu.

Ifuatayo ni Sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani: Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Palipo chuki nieneze upendo. Palipo na mashaka pawe na imani. Palipo na tumaini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu, unijalie; Nisitafute kufarijiwa bali kufariji Nisitafute kupendwa bali kupenda. Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa. Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele, AMINA.  Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu: kutubu, kuongoka na kujiaminisha mbele ya Mungu ili aweze kuwageuza kuwa ni vyombo vya amanbi, upendo na mshikamano wa kweli na hivyo kutorudia tena kwenye makosa ya kihistoria.

Nagasaki 2021

 

 

 

06 August 2021, 15:03