Askofu mteule Guido Marini wa Jimbo Katoliki la Tortona, Italia. Askofu mteule Guido Marini wa Jimbo Katoliki la Tortona, Italia. 

Askofu Guido Marini Jimbo la Tortona: Mshereheshaji Mstaafu!

Askofu mteule Guido Marini alizaliwa tarehe 31 Januari 1965 huko Genoa, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 4 Februari 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre Baadaye alijiendeleza katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran na kujipatia Shahada ya Uzamivu Kuhusu Sheria za Kanisa na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani. Mshereheshaji

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Agosti 2021 amemteua Monsinyo Guido Marini (56) kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki laTortona, nchini Italia. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Guido Marini alikuwa ni Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Guido Marini alizaliwa tarehe 31 Januari 1965 huko Genoa, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 4 Februari 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na Kardinali Giovanni Canestri. Baadaye alijiendeleza kwa masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran na kujipatia Shahada ya Uzamivu Kuhusu Sheria za Kanisa na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani. Na mwaka 2007 alijipatia Shahada ya Uzamivu katika Saikolojia ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesianum.

Tangu mwaka 1988 hadi mwaka 2003 amekuwa ni Katibu muhtasi wa Maaskofu wakuu watatu wa Jimbo kuu la Genoa. Amewahi kuwa pia Jaalimu wa Sheria za Kanisa, Mkurugenzi wa Maisha ya Kiroho Seminari ya Jimbo kuu la Genoa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akamteuwa kuwa ni Mshereheshaji Mkuu wa Kipapa hadi mwaka 2013. Wakati wa mkutano wa Baraza la Makardinali kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, alisimamia maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa huku akishirikiana na Kardinali Tarcisio Betone, aliyekuwa Msimamizi mkuu wa mali za Kanisa yaani “Camerlengo” kama anavyojulikana kwa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu Francisko alipoingia madarakani, akaridhia uteuzi wake kunako mwaka 2014 na hivyo kuendelea na utume huu hadi mwaka 2019 alipomwongezea majukumu ya kuwa Mratibu mkuu wa Kwaya ya Kipapa. Kati ya Mwaka 2018 hadi mwaka 2019 alikuwa anafundisha Liturujia katika Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselm, mjini Roma. Amekuwa pia mhubiri mzuri wa mafungo, semina na makongamano mbalimbali. Amewasindikiza vijana wengi katika maisha na utume wao, akiwasaidia kiroho!

Askofu Guido Marini

 

30 August 2021, 15:15