Jumapili ya Utume wa Bahari tarehe 11 Julai 2021: mambo msingi utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jumapili ya Utume wa Bahari tarehe 11 Julai 2021: mambo msingi utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Jumapili ya Utume wa Bahari 11 Julai 2021: Utu na Haki Msingi!

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa mwaka 2021, linajikita zaidi kubainisha: Haki na wajibu wa Mabaharia na Wavuvi; Matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo; Matukio ya uharamia baharini pamoja na janga la UVIKO-19. Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2021 bado unaonesha umuhimu wa Mabaharia

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” unaojulikana na wengi kama “Stella Maris” ulianzishwa tarehe 4 Oktoba 1920 na waamini walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Ni jukumu na wito wa waamini walei kuutafuta Ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. Wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo! Ili kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, Papa Pio XI tarehe 17 Aprili 1922 aliridhia kuanzishwa kwake. Leo hii kuna jeshi kubwa la watu wanaojisadaka zaidi kuwadumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Wadau wa Utume wa Bahari wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji, kwa kuwafunulia watu sura pendelevu ya Mama Kanisa: kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu wa Mungu na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Takribani miaka 100 iliyopita, imekuwa ni kipindi muafaka cha ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na mataifa mbalimbali duniani. Jumapili tarehe 11 Julai 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2021, ikiwa ni mwaka wa pili wa maadhimisho haya wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa bado inakabiliwa na changamoto ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa mwaka 2021, linajikita zaidi kubainisha: Haki na wajibu wa Mabaharia na Wavuvi; Matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo; Matukio ya uharamia baharini pamoja na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2021 bado unaonesha umuhimu wa Mabaharia na Wavuvi licha ya maambukizi makubwa ya Virusi vya ugonjwa wa UVIKO-19. Meli zimekuwa zikisafirisha dawa na vifaa tiba ili kupambana na UVIKO-19 pamoja na kuendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi kitaifa na Kimataifa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinazonesha kwamba, walau asilimia 90% ya biashara yote duniani inategemea sana Mabaharia ambao ni zaidi ya milioni 1.7. Umoja wa Mataifa, Shirika la Kazi Duniani ILO pamoja na Shirika la Bahari Duniani, IMO (International Maritime Organization, IMO yanalenga kuragibisha umuhimu wa usafirishaji wa abiria na mizigo; usalama wa mabaharia na bidhaa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030. Mashirika haya yamekuwa yakiwapongeza Mabaharia pamoja na wavuvi wakati wa shida, magumu na changamoto mbalimbali walizokutana nazo wakati wanatekeleza dhamana na utume wao. Kundi hili ni la watu muhimu sana na linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee hata katika chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Lakini hadi sasa, utekelezaji wake bado unagonga mwamba. Ulinzi na usalama wa Mabaharia na Wavuvi bado uko mashakani sana.

Takwimu zilizotolewa Mwezi Septemba 2020 zinaonesha kwamba, Mabaharia 400, 000 walikwamishwa baharini kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Na wengine hadi wakati huu, hawajapata nafasi ya kwenda majumbani mwao, hali ambayo inaziathiri pia familia zao. Mabaharia wanakumbana na hali ya kutengwa, upweke hasi pamoja na kukosa upendo kutoka katika familia zao. Wengi wao wana mashaka makubwa kuhusu hatima ya maisha yao binafsi pamoja na familia zao. Kutokana na kufanya kazi ngumu kwa muda mrefu, wengi wao kwa sasa wanakabiliwa na ugonjwa sonona! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutambua kwamba, hawa ni binadamu, wana utu, heshima na haki zao msingi. Kumbe, kuna haja ya kuboresha mazingira ya kazi: kiakili, kimwili na kiroho pia! Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainisha kwamba, tangu mwezi Januari 2021 kuna matukio mbalimbali ya uharamia baharini yametendeka. Vyombo vya usafiri baharini 33 vilitekwa nyara, vingine kuchomwa moto na kushambuliwa na watu wasiojulikana. Huu ni udhaifu mkubwa unaojionesha katika sekta ya usarishaji baharini.

Lakini, ikumbukwe kwamba, Mabaharia wana haki ya kutekeleza dhamana na wajibu wao bila kuogopa kushambuliwa, kutekwa nyara au kuuwawa. Maharamia baharini wamekuwa wakisababisha majanga makubwa kwa Mabaharia pamoja na vyombo vya usafiri baharini, hali inayochangia kuporomoka kwa uchumi wa kitaifa na Kimataifa. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linatoa wito kwa Serikali, Mashirika ya Kimataifa na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba, tatizo la maharamia baharini linapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Ugavi wa bidhaa katika nchi mbalimbali unapaswa kutazamwa upya sanjari na kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi unatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wamiliki wa vyombo vya usafiri majini wahakikishe kwamba, wanatafuta mbinu muafaka ya kuwalinda mabaharia, vyombo vya kazi na mizigo wanayosafirisha. Shirikisho la Wafanyakazi Wa Usafirishaji Kimataifa, “Internationa Trasport Worker's Federation, ITF” linasema, idadi ya meli zinazotelekezwa tangu mwaka 2019 inaongezeka maradufu kutoka meli 40 katika kipindi cha mwaka 2019 hadi kufikia meli 85 kwa mwaka 2020. Sababu kubwa, ni vyombo hivi kukosa tena thamani, wakiwepo pia Mabaharia wake.

Katika muktadha kama huu, Mabaharia wanakosa malipo, mahitaji na haki zao msingi na hivyo kujikuta wakiogelea katika “mkondo wa maji marefu ya maisha”. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linawataka wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba, wanatekeleza Itifaki ya Wafanyakazi wa Baharini ya Mwaka 2006 “Maritime Labour Convention, MLC 2006” iliyoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa kunako mwaka 2014. Mabaharia wanatakiwa kukatiwa Bima ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza pale ambapo meli na mabaharia wanatelekezwa baharini. Katika miaka ya hivi karibuni, ajali za meli baharini zimepungua kwa kiasi kikubwa, lakini bado kuna majanga asilia yanayotishia maisha ya Mabaharia pamoja na vyombo vya kusafirishia. Wakati mwingine, wamiliki wa vyombo hivi wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya kupata faida kubwa na kuwasahau Mabaharia pamoja na familia zao. Inasikitisha kuona watoto wanageuka kuwa yatima, wanawake wa Mabaharia wanabaki kuwa ni wajane!

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu linahitimisha ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2021 kwa kuwaweka Mabaharia, Wavuvi pamoja na Familia zao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari, ili aweze kuwafariji katika shida na mahangaiko yao. Linawakumbuka na kuwashukuru wale wote ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya kiroho na kimwili kwa Mabaharia, Wavuvi pamoja na Familia zao. Ni matumaini ya Baraza hili la Kipapa chini ya uongozi wa Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson na Monsinyo Bruno Marie Duffè kwamba, wadau wote wa Utume wa Bahari wataendelea kwa ari na moyo mkuu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuonesha uso mpendelevu na ukarimu wa Mama Kanisa kwa watu wa Mungu. Waendelee kuwa ni faraja kwa Mabaharia na Wavuvi na Familia zao, ili wao pia waweze kujisikia kuwa ni sehemu hai ya watu wa Mungu ndani ya Kanisa.

Utume wa Bahari 2021
07 July 2021, 14:30