Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan ni sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan ni sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Shindano la Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan Kwa Mwaka 2022

Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, ilianzishwa kunako mwaka 2019. Haya ni matunda ya ushirikiano na majadiliano ya kidini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib,. Tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan ilitolewa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib. Amani na Udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Katika kipindi cha Mwaka 2019 Baba Mtakatifu alifanya hija ya kitume nchini Morocco na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu ambako kuna idadi kubwa ya waaamini wa dini ya Kiislam. Lengo lilikuwa ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili waamini wa dini hizi mbili waweze kufahamiana, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Al Malik al- Kamil kunako mwaka 1219. Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ilianzishwa kunako mwaka 2019.

Haya ni matunda ya ushirikiano na majadiliano ya kidini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulioanzishwa tarehe 2 Desemba 1971 ilitolewa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Viongozi hawa ndio waasisi pia wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu. Tuzo hii pamoja na mambo mengine, inataka kunogesha jitihada za watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali zinazojipambanua katika kutafuta, kujenga na kukuza mahusiano na mafungamano ya kibinadamu. Inalenga kujenga madaraja ya majadiliano ya kidini sehemu mbalimbali za dunia; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi Tuzo hii ni alama ya ushirikiano na mshikamano kati ya waamini wa dini mbalimbali wanaojipambanua katika huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mchakato wa mashindano ya Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, kwa Mwaka 2022 umezinduliwa rasmi Alhamisi, tarehe 1 Julai 2021. Tuzo hii itatolewa kwa mtu mmoja mmoja, kikundi au taasisi ambazo zitajipambanua katika utekelezaji wa sera za maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na kusaidia kuimarisha umoja, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Tuzo hii inatolewa wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa inajitahidi kujikwamua kutoka kwenye madhara makubwa yaliyosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu katika kipindi hiki, inataka kuwatambua watu binafsi na taasisi ambazo zitachuana ili hatimaye, washindi kupatikana watakaobeba tuzo hii kwa Mwaka 2022. Wahusika ni pamoja na: wafanyakazi wa Serikali, Marais, Wabunge, Majaji wa Mahakama kuu pamoja na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa. Tuzo hii inawajumuisha pia wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, Vyuo Vikuu na Viongozi wa kiroho.

Itakumbukwa kwamba, Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Desemba 2019 iliwasilisha mapendekezo ya kuwa na Siku ya Udugu wa Kibinadamu Kimataifa kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres na matunda yake ni Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Tarehe 21 Desemba 2020 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likapitisha Azimio Kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu inayoadhimishwa tarehe 4 Februari ya kila mwaka. Lengo kuu ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani. Yote haya yanapania “kufyekelea” mbali “ndago” za uchoyo na ubinafsi, ili kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Siku hii inawakumbusha watu wote wa Mungu kwamba, ni ndugu wamoja!

Jopo la Majaji wa Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, kwa Mwaka 2022 ni pamoja na Mheshimiwa Muhammadu Issoufou, Rais wa zamani wa Niger; Mh. Jose Ramos Horta, Rais wa zamani wa Timor ya Mashariki, Mheshimiwa Bibi Phumzel Mlambunguka kutoka Umoja wa Mataifa, Kardinali Michael Czerny, SJ., Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, Bibi Leah Bissar, Rais wa Mradi wa Alaa Deen wa kupambana na siasa na misimamo mikali ya kiimani pamoja na Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, Katibu mkuu wa Tume. Jopo litaendelea kupokea majina ya washindani hadi tarehe Mosi Desemba 2021 na mshindi atatangazwa rasmi tarehe 4 Februari 2022. Kwa maelezo zaidi unaweza kufuatilia kwenye tovuti ifuatayo: https://zayedaward.org 

Tuzo 2022

 

 

01 July 2021, 17:35