Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, linaadhimisha Kongamano la Kwanza la Kitaifa kwa Mapadre ili kuhamasisha wito, maisha na utume wa Mapadre. Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, linaadhimisha Kongamano la Kwanza la Kitaifa kwa Mapadre ili kuhamasisha wito, maisha na utume wa Mapadre. 

Kongamano la Kwanza la Mapadre Kitaifa Pwani ya Pembe: Utume!

Kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe. Kipaumbe ni: Utangazaji na Ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu; Umoja, Mshikamano na Udugu; Haki, Amani na Upatanisho pamoja na kujikita katika Injili ya huruma kama nyenzo ya kupambana na changamoto katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Daraja takatifu ya Upadre inawawezesha Mapadre kupokea chapa ya Roho Mtakatifu ili kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hapa ni mahali ambapo, imani inapyaishwa tena kadiri Padre anavyojiweka mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa toba na wongofu wa ndani, jambo ambalo linamwezesha kuzaa matunda ya ajabu katika maisha na utume wa Kanisa. Yote haya yanawezekana ikiwa kama Padre ana imani thabiti na anatambua kile anachopaswa kutenda na anakitenda kwa ari na moyo mkuu. Mapadre watambue kwamba, wao kimsingi ni watu wa imani, waliopewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo ndani ya Kanisa kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Jambo hili ni muhimu sana katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ambamo uchoyo na ubinafsi unaonekana kushika kasi ya ajabu, Mapadre wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wakitumbukia katika ubinafsi na uchoyo kutokana na ubinadamu wao na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu na dhamana waliyokabidhiwa na Mama Kanisa walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Mapadre wanayo dhamana ya kuwahudumia Watu wa Mungu kiroho na kimwili: kwa njia ya huduma mbalimbali za kijamii sanjari na Uinjilishaji, kwani kwa njia ya Fumbo la Umwilisho; Neno wa Mungu amejifanya mtu, katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Unyenyekevu katika huduma ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu. Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika ujumbe wake kwa maadhimisho la Kongamano la Kwanza Kitaifa kwa Ajili ya Makleri nchini Pwani ya Pembe, “Ivory Coast.” Kongamano hili linaadhimishwa mjini Yamoussoukro kuanzia tarehe 8 hadi Jumapili tarehe 11 Julai 2021. Wajumbe 300 kutoka katika Majimbo ya Kanisa Katoliki 15 pamoja na watawa wanashiriki. Kardinali Jean-Pierre Kutwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abijan, nchini Pwani ya Pembe ndiye aliyefunga maadhimisho haya. Kongamano hili lilianza katika ngazi ya majimbo kati ya mwaka 2018 na Juni 2019.

Kongamano hili lilisitishwa kunako mwaka 2020 kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Lengo la Kongamano hili la Kitaifa ni kuchochea ari na mwamko wa kimisionari, toba na wongofu wa ndani. Huu ni mwaliko unaowataka Mapadre kuishi wito wao kadiri ya mwanga wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium”. Kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji iliyoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe. Kipaumbe ni: Utangazaji na Ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu; Umoja, Mshikamano na Udugu wa Kibinadamu; Haki, Amani na Upatanisho wa Kitaifa pamoja na kujikita katika Injili ya huruma kama nyenzo ya kupambana na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Toba na wongofu wa ndani kwa Mapadre ni changamoto ya kusimama kidete katika imani, matumaini na mapendo huku wakiwa na ari mpya katika maisha yao ya kiroho yanayowasukuma kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo Yesu, kama dhamana waliyokabidhiwa na Mama Kanisa.

Makleri ni vyombo vya Roho Mtakatifu katika kuwatakatifuza Watu wa Mungu, ndiyo maana kuna uhusiano wa karibu kabisa kati ya toba, wongofu wa ndani, karama za Roho Mtakatifu na utume wanaopaswa kuutekeleza kwa niaba ya Mama Kanisa. Mapadre wanawaalika kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, huku wakiendelea kuijenga na kuiimarisha kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya toba na huruma. Huduma kwa Familia ya Mungu, ipewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Mapadre, wakitambua kwamba, hata wao, Mwenyezi Mungu anawasubiri kuona wakifanya hija ya toba na wongofu wa ndani kwa unyenyekevu na moyo mkuu. Kama binadamu wana utajiri mkubwa lakini pia wanayo mapungufu yao yanayoweza kuwa ni kikwazo katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, kumbe, toba na wongofu wa ndani ni jambo la msingi, linalowawezesha kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, tayari kuwaimarisha ndugu zao katika imani.

Mapadre wakumbuke kwamba, utume wao ni mtakatifu, lakini umewekwa kwenye chombo cha udongo kinachohitaji uangalifu mkubwa, ili kutekeleza na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa unyenyekevu, huku wakitafakari kazi ya Mungu inayowaalika, inayowapatia nafasi ya kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani; kwani neema ya Mungu inaganga, inaponya na kutakatifuza. Huu ni mwaliko wa kumtangaza Mwenyezi Mungu ambaye wamemtafakari, wakamwona na kumwadhimisha; huyu ndiye Neno wa Mungu aliyejifanya mtu! Kwa kutambua ukuu wa Kristo Yesu kama Bwana na Mkombozi wa dunia; aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu; Kuhani mkuu wa Agano Jipya na la Milele. Ushuhuda wa maisha yao, uwe ni mfano bora wa kuigwa na wale wanaowazunguka na kamwe wasiwe ni sababu ya kashfa na kuanguka kwa Wakristo. Wawe ni viongozi wenye msimamo imara na dira makini ya kufuatwa. Daima waendelee kujifunza kutoka katika shule ya Mama Bikira Maria, aliyefanikiwa kusikiliza kwa makini, akafanya uamuzi wa busara na kutenda kwa hekima kadiri ya Mpango wa Mungu katika maisha yake.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Paolo Borgia, Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, amefungua maadhimisho ya Kongamano la Kwanza Kitaifa kwa Ajili ya Makleri nchini Pwani ya Pembe, kwa kurejea katika Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, aliyejisadaka bila kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya ya Familia Takatifu ya Nazareti. Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana.

Kongamano Mapadre
10 July 2021, 15:58