Tarehe 30 Julai 2021 Vatican na Ufalme wa Monaco wanafanya kumbukizi la miaka 40 tangu watiliane saini ifikati ya makubaliano kuhusu uteuzi wa Askofu mkuu. Tarehe 30 Julai 2021 Vatican na Ufalme wa Monaco wanafanya kumbukizi la miaka 40 tangu watiliane saini ifikati ya makubaliano kuhusu uteuzi wa Askofu mkuu. 

Kumbukizi la Miaka 40: Itifaki ya Makubaliano: Vatican na Monaco

Kumbukizi la miaka 40 tangu Vatican na Ufalme wa Monaco walipotiliana saini itifaki ya makubaliano kuhusu uteuzi wa Askofu mkuu, hapo tarehe 30 Julai 1981. Mtakatifu Yohane Paulo II akalipandisha hadhi Jimbo la Minaco na kuwa ni Jimbo kuu hapo tarehe 25 Julai 1981. Kardinali Parolin ameadhimisha Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la B. Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 alisema kwamba, “Siasa safi ni huduma ya amani”. Alikazia Injili ya amani kama sehemu ya utume wa Kanisa; Changamoto za siasa safi; Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya siasa inayohudumia haki msingi za binadamu na amani. Alipembua vilema vya wanasiasa; umuhimu wa siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani. Alisisitiza kwamba, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wa amani. Baba Mtakatifu anasema Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani kwa watu wa Mataifa wanaoogelea katika dimbwi la vita, kinzani na mipasuko ya kila aina. Amani inapaswa kukita mizizi yake katika maisha ya mtu binafsi bila kubaguliwa, amani katika familia na jamii katika ujumla wake sanjari na kulinda pamoja na kutunza mazingira nyumba ya wote. Amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu.

Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini ikitumiwa vibaya inaweza kuwa ni chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia Jumamosi tarehe 17 hadi Jumatatu tarehe 19 Julai 2021 anafanya hija ya kitume kwenye Ufalme wa Monaco. Hii ni sehemu ya kumbukizi la miaka 40 tangu Vatican na Ufalme wa Monaco walipotiliana saini itifaki ya makubaliano kuhusu uteuzi wa Askofu mkuu, hapo tarehe 30 Julai 1981. Mtakatifu Yohane Paulo II akalipandisha hadhi Jimbo la Monaco na kuwa ni Jimbo kuu hapo tarehe 25 Julai 1981. Pamoja na mambo mengine, Jumapili asubuhi, tarehe 18 Julai 2021, Kardinali Parolin ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa wachungaji wema, wanaosimama kidete kuwalinda, kuwachunga na kuwalisha kondoo wa Kristo Yesu, tayari kuwafunua huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mwenyezi Mungu anashirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza mpango wa kazi ya ukombozi na maisha kwa ajili ya watu wake. Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, ni ushuhuda amini wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu, kwa kuwapeleka faragha wafuasi wake, alitaka kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kama ilivyo kwa Kanisa kwa wakati huu. Yaani kwa njia ya uinjilishaji wa kina na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Ni jukumu la waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga na kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta zinazowatenganisha, ili wote wawe wamoja kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani inayofumbatwa katika huduma kwa jirani kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Hii ni huduma ya kiroho na kimwili. Waamini wajitahidi kulinda na kudumisha mazingira bora kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, alipokutana na kuzungumza na Wabunge kutoka katika Bunge la Ufalme wa Monaco kunako mwaka 2019 aliwashukuru na kuwapongeza kwa kuendeleza mapokeo ya kutunza mazingira nyumba ya wote mintarafu kazi kubwa inayotekelezwa na Mfuko wa Albert wa II wa Ufalme wa Monaco. Leo hii, changamoto kubwa ni athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo inatishia usalama na amani ya watu wanaoishi katika mwambao wa bahari sehemu mbalimbali za dunia. Wabunge hawa, wamekuwa wakishirikiana na Makanisa pamoja na wadau mbali mbali ili kutoa msaada kwa familia maskini hususan katika sekta ya elimu, afya na uchumi. Baba Mtakatifu alikaza kusema, changamoto mamboleo, zinawataka watu kufikiri na kutenda katika mwanga na mwelekeo mpya utakaosaidia kukuza na kudumisha amani na utulivu kati ya watu pamoja na kuzingatia hatima ya maisha ya binadamu. Kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maendeleo ya mwanadamu, kanuni maadili na utu wema vinapaswa kupewa msukumo wa pekee, kwani inaonekana kana kwamba, sayansi inahatarisha maendeleo yaliyokwisha kupatikana. Amani ni tunu inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Parolin
18 July 2021, 15:16