Caritas Internationalis linasema, wanawake wameathirika vibaya zaidi kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Caritas Internationalis linasema, wanawake wameathirika vibaya zaidi kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. 

Caritas Internationalis: UVIKO-19: Wanawake Wameathirika Zaidi

Caritas Internationalis imejikita kusikiliza na kujibu changamoto za UVIKO-19 na kila siku inaona mchango mkubwa wa wanawake katika sekta za afya, elimu, uhamasishaji, mahusiano na jamii, uwajibikaji na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Janga la UVIKO-19 limekuwa na madhara hasi kwa wanawake: kimwili na kisaikolojia: mazingira ya familia, jamii na katika maeneo ya kazi!

Na Anastasia Evarist Lubangura, - Roma.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, “Caritas Internationalis” linasema kwamba, mgogoro wa afya ulimwenguni uliosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limeathiri bila kubagua watu, familia, jamii na mashirika ulimwenguni kote. Hata hivyo kumekuwa na athari ya pekee kwa maisha ya wanawake katika mazingira ya familia, jumuiya na jamii katika ujumla wake. Caritas Internationalis imejikita kusikiliza na kujibu changamoto za mgogoro huu wa afya katika zaidi ya nchi 160 duniani, na inashuhudia kila siku mchango mkubwa wa wanawake katika sekta za afya, elimu, uhamasishaji, muungano wa jamii, uwajibikaji wa pamoja na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.  Janga la UVIKO-19 limekuwa na madhara hasi kwa wanawake: kimwili na kisaikolojia. Madhara haya yanaweza kuangaliwa katika mazingira ya familia, jamii na katika maeneo ya kazi!

Takwimu zinaonesha kwamba, kumekuwepo na matukio mengi ya nyanyaso na ukatili yaliyotokea majumbani. Caritas nchini Afrika ya Kusini ikiangaliwa kama kituo pekee cha udhibiti cha serikali dhidi ya nyanyaso za wanawake, imetoa takwimu ya zaidi ya waathirika 120.000 katika kipindi cha wiki tatu za kwanza za watu kukaa karantini. Kwa wanawake waliokuwa mstari wa mbele kwenye huduma katika sekta ya afya, kadhalika katika huduma kwa wazee na wagonjwa, hatari ya maambukizi imekuwa kubwa mno na wengi wao hawakuwa na vifaa kinga kwa ajili ya kujilinda ipasavyo. Wanawake wengine ambao walikuwa tayari wameathirika na maradhi mengine waliathirika zaidi kwa sababu ya kuchelewa kupata tiba, katika nchi maskini ukosefu wa mahitaji msingi ya kiafya, kukosekana kwa msaada wa kitabibu wakati wa ujauzito na kipindi baada ya kujifugua umepelekea madhara yasiyoweza kurekebishwa.

Katika ngazi ya kisaikolojia, janga hilo limepelekea mmong’onyoko wa afya ya ubongo, kadhalika, katika baadhi ya mazingira, kuminywa kwa haki msingi za binadamu. Nchini India, mgogoro huu wa kiafya, kiuchumi na kijami umewaathiri wanawake kwa namna ya pekee, kukiwa na ongezeko la asilimia 30% ya unyanyasaji na vipigo majumbani. Kuzuia upataji wa matibabu na maelekezo sahihi kupelekea watu wengi kupoteza ajira, upungufu wa mapato ya familia na ongezeko la hali mbaya ya maisha. Katika ngazi ya kazi, sababu nyingi zenye uhusiano na janga la UVIKO-19 zimepelekea madhara zaidi katika ushiriki wa wanawake katika ulimwengu wa kazi na zaidi sana katika uwezekano wa kupata nafasi ya uongozi. Kumekuwepo na ongezeko la ukosefu wa ajira na kufukuzwa kazi au kazi za muda, maarufu kama “part-time”, ongezeko la shughuli za wanawake katika mazingira ya nyumbani na katika sekta ya elimu kwa watoto, bila kusahau mwendelezo na kukua kwa tofauti ya mishahara kati ya wanaume na wanawake.

Mfano, nchini Nigeria, kutokana na kufungwa kwa shughuli nyingi, ufukuzaji wa watu kazini na upunguzaji wa mishahara, vimekuwa na madhara makubwa kwa wanawake na hata katika ulinganifu wa weledi. Ushahidi muhimu unatoka pia Bangladesh, ambapo rejea inajikita zaidi katika maisha ya wakimbizi wa Rohingya, ambao tayari wako katika mazingira duni. Hawa wamekumbwa na madhara ya kukaa karantini ilyochukua muda mrefu, katika ngazi ya maisha ya familia na jamii, halikadhalika katika kazi. Hata hivyo, ni vyema kukumbuka pia umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika kipindi hiki cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 katika kutoa mchango wao muhimu katika nyanja za ujenzi wa mahusiano, huduma, mshikamano, uhamasishajim, ulinzi na utetezi. Katika kila kona ya dunia, makundi ya wanawake wamejikusanya kwa dhumuni la uhamasishaji na utoaji wa taarifa katika jamii.

Huko Afrika ya Kusini, Idara ya afya na ustawi wa jamii na Shirika la Caritas mahalia wameshirikiana kuajiri wahudumu 270 wa afya kwa lengo la kutoa taarifa msingi kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 kwa watu na familia, hususani wale walio katika mazingira magumu na yasiyofikika kwa urahisi. Nchini India, katika mazingira ya vijijini na miji midogo, wanawake “wafanyakazi katika idara ya afya” wamekuwa viunganishi madhubuti baina ya jamii na mfumo wa afya ya jamii, wakitenda bila kujibakiza kwa kutoa taarifa, kuwategemeza na kuwahudumia watu, kutembelea familia, kutafuta mawalisiano, kufanya uchunguzi na kutaarifu maambukizi katika vituo vya afya. Nchini Equador, asilimia 80% ya wafanyakazi wa Caritas waliojishughulisha na watu dhaifu zaidi inaundwa na wanawake.

Katika muktadha wa machafuko ya kisiasa na kivita kama ule wa Siria, Caritas limeunda huko Aleppo idara nyingi za habari na uhamasishaji zikipokea majibu chanya hata kule ambapo hakukuwa na maji tiririka, wala umeme, na kutunza afya ilkuwa ni changamoto kubwa katika ulinzi wa familia. Katika kipindi cha mwezi wa Aprili, 2020 Shirika la Caritas nchini Ufilipin, kwa kuamini kwamba namna pekee ya kupamabana na madhara ya UVIKO-19 ingekuwa ni ushirikiano, ukarimu na huruma, imeanzisha vituo vya ukarimu na mshikamano wa utu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko, mara nyingi amesisitiza kuwa “Janga la UVIKO-19” limewaweka watu wote njia panda na majaribuni na kwa hali zote, lakini kitu amabacho kingekuwa kibaya zaidi katika janga hili, ni hatari ya kulifumbia macho na kutokupata somo litokanalo na janga hilo”. Janga limeweka wazi madhaifu na uonevu yanayojeruhi jamii yetu yote, lakini limetupa mwanga kwaajili ya maisha yajayo: usawa, utamaduni wa kukutana, utambuzi wa mchango pekee wa kila mmoja na utajiri katika utofauti, upyaishaji. Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, “Caritas Internationalis” linasema kwamba, wanao utume wa kuendelea kufanya kazi pamoja, na kuhimiza wajibu wa kuwa ni sauti ya wale wasiokua na sauti duniani!

UVIKO-19
28 July 2021, 16:05