Askofu mkuu Siegfried M. Jwara, Jimbo Kuu la Durban A. Kusini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Wilfrid Fox Napier, O.F.M., la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo, Baba Mtakatifu amemteuwa Askofu Siegfried Mandla Jwara, C.M.M. (Congregation of Mariannhill Missionaries) kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo kuu la Durban, nchini Afrika ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Siegfried Mandla Jwara, C.M.M. alizaliwa tarehe 1 Februari 1957 huko St. Nivard, nchini Afrika ya Kusini. Baada ya masomo na majiundo yake ya kipadre na kitawa, kunako mwaka 1986 akaweka nadhiri zake za daima.
Tarehe 14 Februari 1987 “Siku ya Wapendanao”, akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tarehe 30 Aprili 2016, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Vikarieti ya Ingwavuma, Afrika ya Kusini na kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 25 Juni 2016. Ilipogota tarehe 9 Juni 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini. Katika maisha yake kama Padre amewahi kuwa Mlezi wa Wanovisi, Gambera wa Seminari ya Merrivale na Mshauri wa Mkuu wa Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Mariannhill. Na kati ya mwaka 1998 hadi mwaka 2002 alichaguliwa kuwa ni Padre Mkuu wa Kanda na kurudia tena wadhifa huu kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2009.