Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni chombo madhubuti katika kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano, amani na haki jamii Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni chombo madhubuti katika kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano, amani na haki jamii  

Waraka wa Kitume: Fratelli tutti: Chombo Cha Majadiliano ya Kidini

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni chombo madhubuti katika kukuza na kudumisha mchakato wa utamaduni wa majadiliano, amani, haki jamii na udugu wa kibinadamu. Waraka unaonesha umuhimu wa dini kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni chombo madhubuti katika kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano, amani, haki jamii na udugu wa kibinadamu. Sura ya Tatu ya Waraka huu ni kuhusu mwono wa ulimwengu wazi, sehemu hii inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mwishoni wa Waraka huu wa kitume, Baba Mtakatifu anagusia mambo msingi yanayofumbatwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot hivi karibuni ameshiriki maadhimisho ya Waraka huu, tukio ambalo liliandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, kilichoko mjini Roma kwa kushirikiana na Ofisi ya Kudumu ya Vatican kwenye Umoja wa Mataifa katika ofisi zake ambazo ziko mjini Geneva.

Kimsingi, alijikita zaidi katika kufafanua maana ya udugu, majadiliano ya kidini na haki jamii. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kurejea kutoka katika hija yake ya Kitume nchini Morocco mwaka 2019 alisema, waamini wanapaswa kuwa ni wahudumu wa matumaini hapa duniani kwa kujenga na kuimarisha madaraja yanayowakutanisha watu. Lakini, jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Umuhimu wa dini kulinda, kutunza na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wajibu wa dini kudumisha, haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini wa dini mbalimbali washikamane na kutembea kwa pamoja kwa sababu tofauti zao msingi ni mpango wa Mungu, amana na utajiri unaopaswa kuendelezwa. Majadiliano ya kidini yageuzwe kuwa ni sehemu ya sala inayowaunganisha na kuwafanya kuwa wamoja. Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot anasema kwamba, sura ya Nane inakita maudhui yake katika dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anakazia majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Ni mwaliko wa kuheshimu na kuzingatia ukweli, utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kuondokana na vitendo vyote vinavyohatarisha mahusiano haya. Majadiliano ya kidini yasaidie kukusanya uzoefu, mang’amuzi na hekima za kidini. Kumbe, huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mwono sahihi wa maisha ya kiroho, uaminifu na mapenzi mema kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; umoja na mshikamano wa jirani. Waamini wachangie katika ustawi wa maendeleo yao, kwa kushirikisha tunu msingi za maisha ya kiroho ili kulinda na kuendeleza: haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Majadiliano ya kidini yasadie kukoleza utulivu kwa kujaliana na kuheshimiana, kwa kuendeleza pia mshikamano wa upendo.

Lengo ni kuondokana na kirusi cha: uchoyo na ubinafsi. Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, inawezekana kudumishwa na wote. Imani inawawezeshe waamini kukomaa zaidi kwa kutoka katika maridhiano na kuanza kujikita katika utulivu, unaowawezesha waamini wote kuishi kama ndugu wamoja, huku wakishirikiana. Utamaduni wa majadiliano ya kidini ni njia muafaka ya kunogesha ushirikiano wa kidugu, kwa kuendelea kufahamiana. Ni kwa njia hii, haki, amani na maridhiano vinaweza kutawala katika akili na nyoyo za watu. Ni hamu ya Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba Kanisa linatoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika huduma kwa maskini, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni katika mwanga wa Injili; utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.

Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot anamsema, Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini mchango wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani, kama sehemu ya mchakato wa kufahamiana sanjari na kutambua tunu msingi za maisha ya kiroho wanazoweza kushirikisha kwa familia nzima ya binadamu. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini, kila kukicha! Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 21 Desemba 2020 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio Kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Lengo ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani.

Kilele cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Iraq kilikuwa ni Jumamosi tarehe 6 Machi 2021 kwa kukutana na viongozi wa dini mbalimbali kwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo eneo maarufu ambalo Mwenyezi Mungu alikutana na kufanya ahadi na Ibrahimu, Baba wa imani. Baba Mtakatifu na ujumbe wake, walisafiri kutoka Baghdad hadi mjini Najaf. Huu ni kati ya miji mitakatifu inayoheshimiwa sana na waamini wa dini ya Kiislam. Akiwa mjini hapo amekutana na kuzungumza na Ayatollah Ali Sistani, kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq kwa faragha. Wachunguzi wa mambo wanasema hii ni fursa ya kumwilisha kwa vitendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni changamoto pevu kwa waamini wa dini mbalimbali duniani na wala si vita!

Majadiliano ya Kidini
04 May 2021, 15:31