2021.04.10 Kardinali  Edward I. Cassidy 2021.04.10 Kardinali Edward I. Cassidy 

Ameaga dunia Kardinali Edward Cassidy na maisha yake katika huduma ya Vatican

Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo na baada ya utume wa ubalozi katika nchi mbali mbali za dunia kama mwanadiplomasia,Kardinali Edwad Cassidy ameaga dunia leo hii,huko Newcastle Australia akiwa na umri wa miaka 96.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican.

Kardinali Edward Cassidy, Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Kikristo ameaga dunia tarehe 10 Aprili 2021 huko Newcastle nchini australiana akiwa na umri wa miaka 96. Alizaliwa huko Sydney mnamo tarehe 5 Julai 1924, na kujiunga na Seminari ya Mtakatifu Colomba Springwood mnamo 1943. Kuanzia mwaka uliofuata, alikwenda Chuo cha Mtakatifu Patrick huko Manly, ambapo alimaliza masomo yake. Baadaye aliepewa daraja la ukuhani mnamo tarehe 23 Julai 1949 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu  Maria. Tangu 1950 hadi 1952 alitoa huduma yake kama msaidizi wa Parokia ya Yenda katika Jimbo la Wagga Wagga. Tangu 1952 alisomea Sheria ya Kanoni  ya kanisa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, Roma, na kupata digrii yake mnamo 1955. Tangu 1953 alihudhuria pia Chuo cha Kipapa cha Kanisa kilichopo katika Uwanja wa Minerva Roma na, mwishoni mwa kozi hiyo, alipata diploma, baadaye kujiunga na huduma ya kidiplomasia ya Vatican. Tarehe ya mazishi bado haijapangwa.

Utume wa Kidiplomasia ulimwenguni

Kazi yake ya kwanza ilikuwa katika ubalozi  wa kitume wa vatican nchini India (1955-1962). Baadaye alitumia miaka mitano, tangu 1962 hadi 1967, katika Ubalozi wa kitume  huko Dublin, Ireland , miaka miwili huko El Salvador (1967-1969) na mwaka mmoja huko Argentina. Aliwekwa wakfu kwa kiaskofu mnamo tarehe 5 Novemba 1970. Mnamo 1972 alipewa wadhifa wa kwanza wa Kitume huko Bangladesh, nchi ambayo ilikuwa imepata uhuru siku za karibuni,na  Mwakilishi wa Kitume huko Birmania. Mnamo tarehe 25 Machi 1979 aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kitume wa Afrika Kusini na kama Balozi wa Kitume nchini Lesotho. Mnamo tarehe 23 Machi 1988 aliteuliwa kuwa Naibu wa Katibu wa Nchi kwa ajili ya Mambo ya ndani kwa ujumla. Mnamo 1989 aliteuliwa kuwa rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Kikristo. Hii ni nafasi aliyoshikilia hadi mnamo tarehe 3 Machi 2001. Aliteuliwa  kuwa Kardinali katika Baraza la Makardinali mmnamo tarehe 28 Juni 1991 na Mtakatifu Yohane Paulo II.

10 April 2021, 14:06