Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na  Fungamanisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki 2021. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Fungamanisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki 2021. 

Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki!

Tarehe 3 Januari 2021, Kanisa Katoliki na Fungamanisho la Makanisa ya Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yamefanya kumbukumbu endelevu ya miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Makanisa haya yanapenda kutangaza nia ya kufanya hija ya pamoja kutoka kwenye kinzani na mipasuko, kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo! Neema ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Fungamanisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki toleo la mwaka 2021: “Joint Declaration on the Doctrine of Justification” (JDDJ). Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo, ili wote wawe wamoja chini ya mchungaji mmoja. Tarehe 3 Januari 2021, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yamefanya kumbukumbu endelevu ya miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Makanisa haya yanapenda kutangaza nia ya kufanya hija ya pamoja kutoka kwenye kinzani na mipasuko, kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Toleo la Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki kwa lugha ya Kiitalia lililotolewa mwaka 2021 ndilo kwa sasa limebeba mabadiliko haya ambayo yametiwa saini na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Dr Martin Junge, Katibu mkuu wa Fungamanisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani.

Kwa pamoja wanakiri kwamba, si rahisi kuweza kufutilia mbali historia ya utengano wa Makanisa, lakini kwa sasa historia hii inaweza kuingizwa na hivyo kuwa ni sehemu ya mchakato wa historia ya upatanisho. Kardinali Kurt Koch, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Tamko hili ni muhimu sana katika mchakato wa upatanisho kati ya Wakatoliki na Waluteri kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki. Ikumbukwe kwamba, tofauti kubwa zilizojitokeza miongoni mwa waamini kunako karne ya kumi na sita, kulipelekea Kanisa kujikuta limegawanyika kati ya Waluteri na Wakatoliki. Kunako mwaka 1999, Waluteri na Wakatoliki wakafanikiwa kukiri na hatimaye, kutoa Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki: “Joint Declaration on the Doctrine of Justification of 1999”.

Waamini wa Makanisa haya mawili walikiri na kusema kwamba: “Kwa neema tu, katika imani kwa tendo la wokovu la Kristo, wala si kutokana na stahili yetu yoyote, tunakubaliwa na Mungu na kupewa Roho Mtakatifu, anayefanya upya mioyo yetu na kututayarisha na kutuita kwa ajili ya matendo mema” (TP 15).  “Twakiri kwa pamoja kwamba Mungu husamehe dhambi kwa neema, na wakati huo huo huwaokoa binadamu na mamlaka ya dhambi yenye kuwatia utumwani (...)” (TP 22). Kuhesabiwa haki ni msamaha wa dhambi, tena ni [mtu] kufanywa mwenye haki; [tendo] ambalo kwa njia yake, Mungu “huwajalia [binadamu] kipawa cha maisha mapya katika Kristo” (TP 22). “Basi, tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu” (Rum 5:1). Twaitwa “wana wa Mungu na ndivyo tulivyo!” (1Yn 3:1). Tunafanywa upya kwa kweli na kwa ndani kwa tendo la Roho Mtakatifu, hali tukiendelea kutegemea siku zote kazi yake ndani yetu. “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya” (2Kor 5:17). Kadiri ya maana hiyo, Waliohesabiwa haki hawaendelei kuwa wenye dhambi.

Kardinali Kurt Koch, anaendelea kufafanua kwamba, Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki, limesomwa na kufakariwa kwa kina na Makanisa mengine duniani ambayo kunako mwaka 2019 yameridhia kuhusu Tamko hili na marekebisho yake msingi kuchapishwa katika Toleo la Mwaka 2021 katika lugha ya Kiitalia. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa upatanisho wa kiekumene. Tarehe 3 Januari 2021 ilikuwa ni kumbukumbu ya Miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Papa Leo wa X. Hili ni tukio lililoacha kurasa chungu sana katika maisha na utume wa Kanisa na huo ukawa ni mwanzo wa mgawanyiko wa Kanisa kati ya Waluteri na Wakatoliki.

Kwa namna ya pekee kabisa, tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lakini hasa tangu kuundwa kwa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, kumekuwepo na jitihada za makusudi za kutaka kuivalia njuga changamoto hii ya kiekumene. Lengo limekuwa ni kuiangalia changamoto hii, mintarafu: Historia ya Kanisa wakati ule, Taalimungu iliyokuwa inavuma; Sheria na Kanuni za Kanisa zilizopelekea hata Papa Leo wa X akaamua kumtenga Martin Luther. Dhamana hii nyeti kwa muda wa miaka kadhaa, iliwekwa mikononi mwa mabingwa wa majadiliano ya kiekumene ili waweze kuifanyia kazi. Kumbe, Toleo la Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki kwa lugha ya Kiitalia lililotolewa mwaka 2021 na kutiwa saini na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Dr Martin Junge, Katibu mkuu wa Fungamanisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani unajikita katika mwelekeo huu.

Kwa pamoja wanakiri kwamba, si rahisi kuweza kufutilia mbali historia ya utengano wa Makanisa, lakini kwa sasa historia hii inaweza kuingizwa na hivyo kuwa ni sehemu ya mchakato wa hija ya majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo Yesu, huku wakiongozwa na Injili Takatifu. Kardinali Kurt Koch anakaza kusema, Kuna matukio mbalimbali yanayoadhimishwa katika Kipindi cha Miaka 10 kuanzia mwaka 2021 na kilele chake ni hapo mwaka 2030, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kutokea “Ungamo la Augusta”: “Confessio Augustana.” Ungamo hili lina nguvu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Waluteri na Wakatoliki. Hili ni tukio la matumaini ya majadiliano ya kiekumene kwa siku za mbeleni!

Makanisa yanataka kuanza huku yakiwa yameshikamana, ili kuendelea kujizatiti katika mambo yale yanayo waunganisha zaidi, ili kufanya kazi kwa pamoja, kwa kushinda kiburi na hali ya kutoaminiana. Hija ya majadiliano ya kiekumene inajielekeza zaidi katika mchakato wa upatanisho, kwa kutambua na kukiri machungu ya historia ya utengano kati ya Makanisa. Sasa ni wakati wa kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, mchakato uliokuwa na nguvu ya pekee kunako mwaka 1999, kwani waamini wanahesabiwa haki kwa neema tu, katika imani kwa tendo la wokovu la Kristo wala si kutokana na stahili yao yoyote, wanakubaliwa na Mwenyezi Mungu na hivyo kupewa Roho Mtakatifu, anayefanya upya nyoyo zao na kuwatayarisha pamoja na kuwaita kwa ajili ya matendo mema.

Tamko la Kiekumene

 

15 March 2021, 08:13