Kardinali Pietro Parolin amemwandikia barua Kardinali Maung Bo, akimwomba kuhakikisha kwamba, Kanisa linajihusisha kikamilifu katika mchakato wa haki, amani na maridhiano ya kitaifa nchini Myanmar. Kardinali Pietro Parolin amemwandikia barua Kardinali Maung Bo, akimwomba kuhakikisha kwamba, Kanisa linajihusisha kikamilifu katika mchakato wa haki, amani na maridhiano ya kitaifa nchini Myanmar. 

Mapinduzi ya Kijeshi Myanmar: Kanisa Lisaidie Kudumisha Amani

Kanisa lisaidie mchakato wa kuwakutanisha viongozi wakuu wanaohusika na mgogoro huu wa kisiasa, ili kujadiliana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wasaidie kuwapatia wananchi na hasa vijana matumaini; walinde na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu! Amani ni jambo linalowezeka, ikiwa kama masilahi ya kitaifa yatapewa kipaumbele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kulaani na kushutumu mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Myanmar tarehe 1 Februari 2021 na tangu wakati huo kumekuwepo na maandamano makubwa kupinga mapinduzi ambao kwa sasa yamekuwa ni kichocheo kikubwa cha mauaji na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Wito umetolewa na Jumuiya ya Kimataifa wa kurejeshwa tena utawala wa kidemokrasia sanjari na kuachiliwa huru Aung San Suu Kyi kiongozi mkuu wa Chama cha “National League for Democracy, NLD., na wanasiasa wenzake wanaoshikiliwa kizuizini. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika barua aliyomwandikia Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Myanmar, anamsihi ili awakilishe ujumbe wa udugu wa amani na mshikamano, wasi wasi na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Parolin anamsihi Kardinali Maung Bo kuhakikisha kwamba, anasaidia mchakato wa kuwakutanisha viongozi wakuu wanaohusika na mgogoro huu wa kisiasa, ili kujadiliana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wasaidie kuwapatia wananchi na hasa vijana matumaini; walinde na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu! Amani ni jambo linalowezeka, ikiwa kama masilahi ya kitaifa yatapewa kipaumbele cha kwanza. Jumuiya ya waamini inapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa. Ni wakati wa kuanza kujikita katika demokrasia na utawala bora zaidi.

Wakati huo huo huo, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amependa tena kutoa wito kwa viongozi wanaohusika, kuanza kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na matumizi makubwa ya mtutu wa bunduki, hali inayoendelea kusababisha uvunjifu wa amani na ukosefu ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kuingilia kati na kuiokoa Myanmar inayoanza kuzama katika machafuko na maafa makubwa. Vijana nchini Myanmar wapewe tena nafasi ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, mahali ambapo chuki na uhasama havina nafasi tena na badala yake, watu wajikite katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa na msamaha wa kweli.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa demokrasia ulioanza kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni nchini Myanmar, utapyaishwa tena kwa kuwaachia huru wanasiasa waliofungwa gerezani au kuwekwa kizuizini. Amiri Jeshi mkuuu Min Aung Hlaing kwa sasa ndiye anayeongoza nchi ya Myanmar na kwamba, baada ya hali ya hatari kupita, Serikali ya Kijeshi itaitisha uchaguzi huru na wa haki kwa wananchi wa Myanmar.

Parolin Myanmar

 

16 March 2021, 16:10