Kauli ya Idara ya Toba ya Kitume kuhusu umuhimu wa Jukwaa la Ndani la Kutovunjwa kwa Siri ya Maungamano lililotolewa tarehe 21 Juni 2019, Mjini Vatican. Kauli ya Idara ya Toba ya Kitume kuhusu umuhimu wa Jukwaa la Ndani la Kutovunjwa kwa Siri ya Maungamano lililotolewa tarehe 21 Juni 2019, Mjini Vatican. 

Idara Ya Toba ya Kitume Kutovunjwa Kwa Siri ya Maungamo

Idara ya Toba ya Kitume inapenda kuthibitisha umuhimu na kuchochea uelewa sahihi katika mawasiliano ya Kanisa na ya jamii; dhana zinaonekana kuwa ngeni kwa mtazamo wa wengi na wakati mwingine kwa mifumo yenyewe sheria za kiraia: muhuri wa sakramenti, siri katika jukwaa la ndani nje ya Sakramenti, siri za kitaalam, vigezo na mipaka sahihi katika mawasiliano mengine yote.

Idara ya Toba ya Kitume, - Vatican.

"Kwa umwilisho wake Mwana wa Mungu ameungana kwa namna fulani na kila mtu";[1] kwa ishara zake na kwa maneno yake, ameuangaza ndani yake mwenyewe utu wenye hadhi kuu na usionajisika, kwa kufa na kufufuka kwake ameurejesha utu ulioanguka, akashinda giza la dhambi na kifo; kwa wale wamwaminio amefungua uhusiano na Baba yake; kwa kumimina Roho Mtakatifu ameliweka wakfu Kanisa, jumuiya ya waamini, ambayo hakika ni mwili wake, na amelishirikisha katika mamlaka yake ya kinabii, ya kifalme na ya kikuhani, ili liwe mwendelezo wa uwepo, na wa kazi yake ulimwenguni, kwa kuwatangazia ukweli watu wa nyakati zote, na kuwaongoza katika fahari ya nuru yake, kwa kuruhusu maisha yao yaguswe kweli na kupewa sura mpya. Katika nyakati hizi za historia ya binadamu vurugu nyingi, kukua kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia hakuonekani kurandana na maendeleo halisi ya kimaadili na kijamii, badala yake huendana na mapinduzi ya kiutamaduni na kimaadali ambayo, kwa kumsahau Mungu – kama si kupingana naye kabisa – hukosa uwezo wa kutambua na kuheshimu tunu-msingi za uwepo wa binadamu katika nyanja na ngazi zote, ikiwa ni pamoja na maisha halisi ya Kanisa. "Kama maendeleo ya kiufundi hayaendi sambamba na maendeleo ya binadamu katika malezi ya kimaadili, katika makuzi ya ndani ya mtu ..., basi hayo si maendeleo hata kidogo, bali ni tishio kwa mwanadamu na kwa dunia".[2]

Pia katika uwanja wa mawasiliano binafsi na kwa njia ya vyombo vya habari "njia za kiufundi" hukua kupita kiasi, lakini si upendo kwa ajili ya ukweli, dhamira ya kuutafuta, wala dhana ya uwajibikaji mbele ya Mungu na mbele ya watu; hofu na ukinzani kati ya njia (za mawasiliano) na maadili huwa dhahiri.Kujikuza kwa mawasiliano huonekana kupingana na ukweli, na matokeo ya hilo, huwa kinyume na Mungu na binadamu; kinyume na Yesu Kristo, Mungu aliyejifanya mtu, na kinyume na Kanisa ambalo ni uwepo wake katika historia na katika uhalisia. Katika miongo ya hivi karibuni kumekuwa na “tamaa” fulani ya habari, karibu bila kujali kama ni za kuaminika na kama ni wakati mwafaka, kiasi kwamba "dunia ya mawasiliano" imekuwa na mwonekano wa "kuchukua nafasi" ya uhalisia, kwa kushurutisha mtazamo na kwa kudhibiti ulelewa pia. Kwa bahati mbaya, muundo wenyewe wa Kanisa, ambalo linaishi katika ulimwengu na wakati mwingine kukumbatia vigezo vyake, hauna kinga dhidi ya tabia hii, ambayo yaweza kubeba dalili hahatarishi za ugonjwa. Mara kwa mara, hata miongoni mwa waumini, jitihada za pekee hutumika katika kutafiti "habari" - au "kashfa" za kweli na halisi – zenye uwezo wa kusisimua hisia au hoja mahususi katika jamii, kwa nia na malengo ambayo hakika hayaendani na maumbile ya kimungu-na-kibinadamu ya Kanisa. Yote haya husababisha uharibifu mkubwa katika utangazaji wa Injili kwa kila kiumbe, na katika mahitaji ya utume. Inabidi kutambua kwa unyenyekevu kwamba wakati mwingine, hata madaraja ya wakleri, hadi ngazi ya juu zaidi katika hairakia, hayana kinga dhidi ya tabia hii.

Mara nyingi mno, kama ilivyo hali halisi ya sasa, kwa kutumia maoni ya umma kama mahakama kuu, taarifa za kila aina hutolewa kuhusu nyanja binafsi na za siri sana, zenye kugusa kwa lazima maisha ya Kanisa, ambazo husababisha — au aghalabu huchochea maamuzi ya ovyo, yenye kuchafua majina ya wengine isivyo halali na kujeruhi sifa zao kwa namna isiyoponyeka, ikiwa ni pamoja na kukiuka haki ya faragha abayo kila mtu anatakiwa kuwa nayo na kuilinda (rej. Kanuni ya 220 CIC). Katika hali hii, ni wakati mwafaka kurejea maneno ya Mt. Paulo kwa Wagalatia: «Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo. Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe." Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!» (Gal 5:13-15). Katika muktadha huu, yaonekana kuwepo "chuki” yenye utata wa namna fulani, dhidi ya Kanisa Katoliki, ambayo uwepo wake hujionesha kiutamaduni na kujithibitisha kijamii, kwa upande mmoja, katika mivutano inayoweza kujitokeza baina ya uongozi-hairakia wenyewe, na kwa upande mwingine, huibuliwa katika kashfa nzito za hivi karibuni juu ya unyanyasaji uliotekelezwa na baadhi maklero.

Chuki hii yenye usahaulifu kwa asili ya kweli ya Kanisa, kwa historia yake makini na kwa matunda yake halisi na nufaishi ambayo daima limekuwa nayo na linaendelea kuwa nayo katika maisha ya watu, wakati mwingine hubadilika kuwa "madai" yasiyokuwa na uhalali wowote, kwamba Kanisa lenyewe, katika mambo kadha wa kadha, linapaswa kupatanisha mfumo wake wa kisheria na mifumo ya kiraia ya Mataifa ambapo linakutwa, kama dhamana pekee "ya kujihakikishia usahihi na ya uhalali". Kwa kuzingatia yote hayo, Idara ya Toba ya Kitume imeona ni vema kuingilia kati, kwa njia ya kauli hii, ili kuthibitisha umuhimu na kuchochea uelewa sahihi wa dhana hizi, za kawaida katika mawasiliano ya Kanisa na ya jamii, ambazo leo zinaonekana kuwa ngeni kwa mtazamo wa wengi na wakati mwingine kwa mifumo yenyewe sheria za kiraia: muhuri wa sakramenti, siri katika jukwaa la ndani nje ya Sakramenti, siri za kitaalam, vigezo na mipaka sahihi katika mawasiliano mengine yote.

1. Muhuri wa Sakramenti. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia Sakramenti ya Upatanisho, alitaka kuthibitisha ulazima na kutokupenyeka kwa muhuri wa Sakramenti: "Upatanisho wenyewe ni tunu ambayo hekima ya Kanisa imeilinda siku zote kwa nguvu zote za kimaadili na kisheria, kwa muhuri wa sakramenti. Ingawa si mara zote hueleweka kwa mitazamo ya kisasa, ni ya lazima kwa ajili ya utakatifu wa Sakramenti na kwa ajili ya uhuru wa dhamiri ya mwungama, ambaye sharti awe na uhakika, wakati wowote, kuwa mazungumzo katika sakramenti hubaki kuwa siri ya maungamo, baina ya dhamiri yake iliyojifunua kwa ajili ya neema, na Mungu, sharti kwa upatanisho wa Padre. Muhuri wa sakramenti ni lazima na hakuna mamlaka ya kibinadamu yenye uwezo juu yake, wala madai yoyote dhidi yake"[3] Siri ya maungamo isiyovunjwa ina chimbuko la moja kwa moja katika sheria ya kimungu iliyofunuliwa na imejikita katika asili halisi ya sakramenti ya Kitubio, kiasi kwamba hitilafu yoyote haikubaliki katika nyanja za kanisa, wala, hata kidogo, katika nyanja za kiraia. Kimsingi, ni kana kwamba maadhimisho ya sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa: Mwana wa Mungu alijifanya mtu ili kutuokoa na aliamua kulihusisha Kanisa kama "chombo cha lazima" katika kazi hii ya wokovu, na ndani yake, wale aliowachagua, akawaita na kuwaweka wawe wahudumu wake.

Ili kuelezea ukweli huu, daima Kanisa limefundisha kwamba mapadri, katika maadhimisho ya Sakramenti, hutenda “in persona Christi capitis”, yaani, hatika nafsi ya Kristo aliye Kichwa: «Kristo huturuhusu sisi kutumia “Mimi”, twanena katika “Mimi” ya Kristo, Kristo “anatuvuta ndani mwake” na kuturuhusu kuungana. Hutuunganisha na 'Mimi' yake. [...] Ni muungano huu na 'Mimi' yake ambao huthibitishwa katika maneno ya wakfu. Pia katika “Nakuondolea dhambi” kwa sababu hakuna yeyote kati yetu anayeweza kusamehe dhambi - ni “Mimi” ya Kristo, ya Mungu, ambayo ndiyo pekee ina uwezo wa kuondolea dhambi». [4] Kila mwenye kutubu ambaye kwa unyenyekevu huenda kwa Padre kuungama dhambi zake hushuhudia kwa namna hiyo, siri kubwa ya Umwilisho na asili ya kimungu ya Kanisa na ukuhani wa huduma, ambavyo kwavyo Kristo Mfufuka huja kukutana na watu, kwa njia ya sakramenti - yaani hakika – hugusa maisha yao na kuwaokoa. Kwa sababu hii, ulinzi wa muhuri wa sakramenti ambao hutekelezwa na Padre, ikibidi usque ad sanguinis effusionem, yaani hadi kumwaga damu, huonesha si tu tendo la “uaminifu” makini kwa mwumgama, lakini zaidi sana: ushuhuda muhimu – “ushuhuda wa damu” – ambao hutolewa moja kwa moja kwa upekee na umoja wa Kristo na Kanisa wenye kuleta wokovu. [5]

Suala la muhuri kwa sasa hufafanuliwa na kuongozwa na kanuni 983-984 na 1388, §1 za CIC (Sheria za Kanisa), na kanuni 1456 ya CCEO (Sheria ya Kanuni ya Makanisa ya Mashariki), pamoja na Katekisimu ya Kanisa Katoliki na. 1467, ambapo kwa uwazi kabisa, tunasoma kwamba Kanisa "latamka", kwa mujibu wa mamlaka yake, badala ya kusema “latangaza" – yaani, huthibitisha kama kanuni isiyohafifishwa, yenye chimbuko madhubuti katika utakatifu wa sakramenti iliyoasisiwa na Kristo – "kwamba kila Padre anayesikiliza maungamo anawajibika kushika siri kamili, chini ya adhabu kali sana, kuhusu dhambi ambazo wenye kutubu wameungama kwake”. Mwungamishi haruhusiwi kamwe, kwa sababu yoyote ile, "kumsaliti kwa namna yoyote mwenye kutubu, iwe kwa maneno au kwa njia yoyote ile" (CIC kan. 983, §1), vilevile "ni marufuku kabisa mwungamishi kutumia ujuzi alioupata katika maungamo kumdhuru mwenye kutubu hata kama ni kwa kuepuka kila hatari ya kuweka mambo wazi (CIC kan. 984, §1). Fundisho hilo lilisaidia pia kubainisha kwa kina yaliyomo ndani ya muhuri wa sakramenti, ambayo ni pamoja na "dhambi zote za mwenye kutubu na za watu wengine, zilizofahamika katika maungamo ya mfanya toba, ziwe za mauti au ndogo, ziwe zimetendwa wazi au sirini, kama zilivyobainishwa kwa ajili ya maondoleo, na hivyo kujulikana kwa mwungamishi kwa mujibu wa ujuzi ndani ya sakramenti”. [6] Kwa hiyo, muhuri wa Sakramenti, unahusu kila kitu ambacho mwenye kutubu amekiri, hata ikiwa mwumgamishi hakumfanyia maondoleo: kama toba yake ni batili au kwa sababu fulani maondoleo hayakufanyika, lazima muhuri usitiriwe kwa hali yoyote.

Kwa hakika, Padre hufahamu dhambi za mwumgama “non ut homo, sed ut Deus - sio kama mwanadamu, bali kama Mungu", [7] kiasi kwamba "hajui" alichoambiwa wakati wa maungamo, kwa sababu kiusahihi, hakusikiliza kama mtu, bali kwa jina la Mungu. Kwa hivyo mwungamishi anaweza pia "kuapa" bila wasiwasi wowote katika dhamiri yake, "kutojua" kile anachojua tu kama mhudumu wa Mungu. Kwa mujibu wa udhati wake wa kipekee, muhuri wa sakramenti huweza kumfunga mwungamishi hata "kwa ndani", kiasi kwamba hupigwa marufuku kukumbuka maungamo kwa hiari yake, na hulazimika kudidimiza kumbukumbu yoyote isiyokuwa ya hiari. Usiri unaotokana na muhuri huwafunga pia wale ambao, kwa njia yoyote, wamepata kujua dhambi wakati wa maungamo: "mkalimani, kama yupo, na wengine wote ambao kwa njia yoyote wana ufahamu wa dhambi kutoka kwenye maungamo hutakiwa pia kusitiri usiri” (CIC kan. 983, §2).

Katazo kamili lililowekwa na muhuri wa Sakramenti ni kali kiasi cha kumzuia Padre kuzungumzia nje ya Sakramenti, yaliyomo kwenye maungamo hata kwa mwungama mwenyewe, bila “kibali (bora hata kisiombwe) maalum" cha mwenye kutubu. [8] Kwa hiyo, muhuri huzidi mipaka ya utashi wa mwenye kutubu, ambaye, mara tu Sakramenti inapoadhimishwa, hana mamlaka ya kumlegezea mwungamishi jukumu la usiri, kwa sababu jukumu hili hutoka kwa Mungu moja kwa moja. Kinga ya muhuri wa sakramenti na utakatifu wa maungamo haiwezi kamwe kujenga aina yoyote ya ushirika katika maovu. Badala yake huwakilisha tiba ya kweli ya uovu unaotishia mwanadamu na ulimwengu wote; hujenga uwezo halisi wa kujisalimisha kwa upendo wa Mungu, wa kujiruhusu kuongoka na kubadilishwa na upendo huu, kwa kujifunza kuafikiana nao katika maisha halisi ya mtu. Katika uwepo wa dhambi zinazohusisha makosa ya jinai, hairuhusiwi kamwe kumtwika mwenye kutubu, kama sharti la maondoleo, jukumu la kujisalimisha mwenyewe kwa vyombo vya kiraia vya utoaji haki, kwa mujibu wa kanuni ya asili, inayofumbatwa katika kila mfumo, ambayo kwayo "nemo tenetur se detegere".

Wakati huo huo, hata hivyo, toba ya dhati, pamoja na nia thabiti ya kufanya marekebisho na kutokurudia uovu uliotendwa ni sehemu ya lazima katika "muundo" wenyewe wa Sakramenti ya Upatanisho, kama sharti la uhalali wake. Iwapo kuna mwungama ambaye amekuwa mwathirika wa uovu wa watu wengine, litakuwa jambo la ukarimu kama mwungamishi atamwelekeza kuhusu haki zake na pia juu ya vyombo vya kisheria anavyoweza kuvitembelea ili kuripoti uhalisia wa mambo katika jukwaa la kiraia au la kikanisa, ili kutetea haki. Tendo lolote la kisiasa au hatua ya kisheria inayolenga "kukiuka" hali isiyonajisika ya muhuri wa sakramenti litakuwa kosa lisilokubalika dhidi ya libertas Ecclesiae, yaani dhidi ya uhuru wa Kanisa, ambao uhalali wake hautoki kwa Taifa lolote, bali kwa Mungu; litakuwa pia ukiukwaji wa uhuru wa dini, ambao kisheria ni msingi wa uhuru mwingine wowote, ikiwa ni pamoja na uhuru wa dhamiri wa raia binafsi, iwe ni wenye kutubu au waungamishi pia. Kuvunja muhuri kutakuwa sawasawa na kumdhuru mnyonge aliye ndani ya mdhambi.

2. Jukwaa la ndani nje ya Sakramenti na maongozi wa kiroho. Jukwaa la ndani katika uwanja wa sheria-na-maadili hujumuisha pia kile kinachoitwa "jukwaa la ndani nje ya sakramenti", ambacho japo ni nje ya Sakramenti ya Kitubio, hubaki kimefungwa daima. Ndani yake pia, Kanisa hufanya utume wake kwa mamlaka yake ya kuokoa: sio kwa kusamehe dhambi, bali kwa kugawa neema, kuvunja mapingamizi ya kisheria (kama vile vikwazo) na kushughulikia yote yahusuyo utakaso wa roho, na hivyo, uwanja halisi wa faragha na wa binafsi kwa kila mwamini. Kwa namna ya pekee, maongozi ya kiroho ambayo kwayo mwamini binafsi huaminisha njia yake ya uongofu na utakaso kwa Padre fulani, kwa mtu wa wakfu au kwa mkristu-mlei, ni sehemu ya jukwaa la ndani nje sakramenti. Kuhani hufanya huduma hii kwa nguvu ya utume wake wa kumwakilisha Kristo, ambao amekabidhiwa katika Sakramenti ya Dalaja Takatifu na huifanya katika ushirika wa kihairakia wa Kanisa, kwa njia ya kile kinachoitwa tria munera: kazi ya kufundisha, kutakatifuza na kutawala. Waamini walei hufanya huduma hii kwa nguvu ya ukuhani wa Ubatizo na kwa kipaji cha Roho Mtakatifu. Katika maongozi ya kiroho, mwamini hufunua kwa uhuru siri ya dhamiri yake kwa kiongozi wa kiroho, ili aelekezwe na kusaidiwa katika kusikiliza na kutimiza mapenzi ya Mungu. Kwa hivyo, mazingira haya mahususi hudai pia usiri maalum ad extra, ambao kwa asili hufungamana na maudhui ya mazungumzo ya kiroho, pia hutokana na haki ya kila mtu kuhusu faragha yake (rej. CIC kan. 220).

Ingawa tu “kwa ufanano" na kile kifanyikacho katika Sakramenti ya Kitubio, kiongozi wa kiroho hupata kuifahamu dhamiri ya mwamini kwa mujibu wa uhusiano wake maalum na Kristo, ambao hutokana na utakatifu wa maisha, na kama ni Padre, hutokana na Sakramenti yenyewe ya Daraja Takatifu aliyoipokea. 5 Katika ushuhuda wa usiri maalum unaotakiwa katika maongozi ya kiroho, budi kutanabahi katazo lililowekwa na sheria, dhidi ya kudai maoni, si ya mwungamishi tu, bali pia ya kiongozi wa kiroho, wakati wa mchakato wa kumpokea mtu katika Daraja Takatifu au, kinyume chake, kwa ajili ya kuwaondoa seminarini watarajiwa wa upadre (rej. CIC kan. 240, §2; CCEO kan. 339, §2). Kwa njia hiyo hiyo, maelekezo ya “Sanctorum Mater” ya mwaka 2007, kuhusu utekelezaji wa uchunguzi wa kijimbo au kieparkia katika mchakato wa kutangaza Watakatifu, hukataza kupokea ushuhuda sio tu wa waungamishi katika kulinda muhuri wa sakramenti, bali pia ule wa viongozi wa kiroho wa Mtumishi wa Mungu, ikiwa ni pamoja na chochote kile walichokifahamu katika jukwaa la dhamiri, nje ya Sakramenti ya maungamo. [9]

Usiri huu muhimu utakuwa "wa msingi" zaidi kwa kiongozi wa kiroho, jinsi atakavyojifunza zaidi kutambua na "kuchukuliwa" katika fumbo la uhuru wa waamini ambao kupitia kwake humrudia Kristo; kiongozi wa kiroho hana budi kuelewa kwa namna ya pekee utume wake na maisha yake mwenyewe mbele za Mungu, katika huduma ya utukufu Wake (Mungu), kwa manufaa ya mtu, ya Kanisa, na kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima.

3. Siri na mipaka mingine ya msingi katika mawasiliano. Tofauti na jukwaa la ndani katika sakramenti na nje ya sakramenti, zipo siri nyingine ambazo huaminishwa chini ya kifungo cha muhuri, ikiwa pamoja na kile kiitwacho “siri za kitaalam” zinazohusu aina fulani za watu, iwe katika jamii za kiraia au katika nyanja za Kanisa kwa ujumla, kwa mujibu wa ofisi maalum wanazohudumu kwa ajili ya watu binafsi au kwa ajili ya jamii. Siri za namna hiyo, kwa mujibu wa sheria ya asili, lazima zihifadhiwe kila wakati "isipokuwa" – inatamka Katekisimu ya Kanisa Katoliki n. 2491 – "kwa masuala ya pekee ambamo kushika siri kungesababisha madhara makubwa sana kwa yule aliyeiaminisha, kwa yule aliyeipokea au kwa mtu wa tatu. Na pale ambapo madhara yale makubwa sana yaweza kuzuiwa tu kwa kuutoa ukweli”. Aina maalum ya usiri ni ile "siri ya kipapa", ambayo humfunga mtu kwa nguvu ya kiapo kinachohusiana na utekelezaji wa huduma fulani kwa ajili ya Kiti cha Kitume. Ikiwa kiapo cha usiri humfunga daima coram Deo yule aliyeapa, kiapo kinachohusu "siri ya kipapa" kina “lengo” lake kuu, yaani manufaa ya umma ya Kanisa na salus animarum (wokovu wa roho za watu). Inaeleweka kwamba lengo hili, na mahitaji yenyewe ya salus animarum, ikihusisha pia kwa misingi hiyo, matumizi ya habari ambazo haziko chini ya muhuri, vyaweza na havina budi kutafsiriwa kwa usahihi na Kiti cha Kitume pekee, katika nafsi ya Baba Mtakatifu, ambaye Kristo Bwana alimsimika na kumweka awe chanzo kinachoonekana na msingi wa umoja wa imani na ushirika wa Kanisa zima. [10]

Kuhusu nyanja nyingine za mawasiliano, yawe ya umma au ya binafsi pia, katika aina zote na sura zake mbalimbali, hekima ya Kanisa daima huhimiza kama kigezo cha msingi "kanuni ya dhahabu" iliyotangazwa na Bwana na iliyomo katika Injili ya Luka: "Watendeeni wengine kama mnavyotaka wawatendee ninyi” (Lk 6:31). Kwa njia hii, katika ushirikishaji wa ukweli na vilevile katika ukimya unaoambatana nao, ikiwa mwenye kuutafuta hana haki ya kuujua, yampasa kuyapatanisha maisha yake na amri ya upendo wa kidugu, akitanguliza manufaa na usalama wa wengine, heshima kwa maisha binafsi na maslahi ya pamoja. [11] Katika jukumu maalum la kupeana ukweli, linaloamriwa na upendo wa kidugu, mtu hawezi akakosa kuongelea suala la "marekebishano ya kidugu" katika ngazi zake mbalimbali, kama tulivyofunzwa na Bwana. Hubaki kuwa uwanja wa rejea, inapobidi na kwa kuzingatia uwezekano na mahitaji halisi ya mazingira: "Ndugu yako akikukosea, mwendee ukamwonye mkiwa ninyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako. Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe. Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa, na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watoza ushuru” (Mt 18: 15-17). Katika kipindi cha "ukuzaji" wa mawasiliano, ambamo habari zote "hukaangwa" na pamoja nazo kwa

Kuhusu nyanja nyingine za mawasiliano, yawe ya umma au ya binafsi pia, katika aina zote na sura zake mbalimbali, hekima ya Kanisa daima huhimiza kama kigezo cha msingi "kanuni ya dhahabu" iliyotangazwa na Bwana na iliyomo katika Injili ya Luka: "Watendeeni wengine kama mnavyotaka wawatendee ninyi” (Lk 6:31). Kwa njia hii, katika ushirikishaji wa ukweli na vilevile katika ukimya unaoambatana nao, ikiwa mwenye kuutafuta hana haki ya kuujua, yampasa kuyapatanisha maisha yake na amri ya upendo wa kidugu, akitanguliza manufaa na usalama wa wengine, heshima kwa maisha binafsi na maslahi ya pamoja. [11] Katika jukumu maalum la kupeana ukweli, linaloamriwa na upendo wa kidugu, mtu hawezi akakosa kuongelea suala la "marekebishano ya kidugu" katika ngazi zake mbalimbali, kama tulivyofunzwa na Bwana. Hubaki kuwa uwanja wa rejea, inapobidi na kwa kuzingatia uwezekano na mahitaji halisi ya mazingira: "Ndugu yako akikukosea, mwendee ukamwonye mkiwa ninyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako. Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe. Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa, na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watoza ushuru” (Mt 18: 15-17).

Katika kipindi cha "ukuzaji" wa mawasiliano, ambamo habari zote "hukaangwa" na pamoja nazo kwa bahati mbaya, mara nyingi sehemu ya maisha ya watu hukaangwa pia, ni lazima kujifunza upya nguvu ya neno, nguvu yake ya kujenga, lakini pia uwezo wake wa kubomoa; lazima tuwe macho kusudi isitokee kamwe muhuri wa sakramenti ukavunjwa na mtu yeyote, na usiri wa lazima unaofungamana na utekelezaji wa huduma za kikanisa ulindwe kwa udi na uvumba, kwa kutanguliza ukweli na manufaa ya watu kama kitu pekee mbele ya upeo wa macho. Tuombe kwa Roho Mtakatifu, kwa ajili ya Kanisa zima, upendo dhabiti wa ukweli katika kila eneo na hali zote za maisha; uwezo wa kuulinda kikamilifu katika utangazaji wa Injili kwa kila kiumbe, utayari wa kufa kishahidi ili kulinda kutokukiukwa kwa muhuri wa sakramenti, pamoja na busara na hekima ambavyo ni muhimu ili kuepuka matumizi yoyote mabaya na ya kimakosa, ya habari zinazohusu maisha ya watu binafsi, ya jamii na ya Kanisa, yanayoweza kugeuka makosa dhidi ya utu na dhidi ya Ukweli wenyewe, ambao daima ni Kristo mwnyewe, Bwana na Kichwa cha Kanisa.

Katika kusitiri kwa umakini muhuri wa Sakramenti na busara mahususi inayofungamana na jukwaa la ndani nje ya Sakramenti na matendo mengine ya huduma, kuna muungano maalum unaong’aa kaatika Kanisa, baina ya mlengo wa kipetrino na ule wa kimariana. Pamoja na Petro, bi harusi wa Kristo hulinda huduma ya kitaasisi ya "mamlaka ya funguo" hadi mwisho wa nyakati; kama Maria Mtakatifu sana, Kanisa husitiri "vitu hivi vyote moyoni mwake" (Lk. 2: 51b), likijua kuwa ndani yake huzunguka ile nuru inayomwangaza kila mtu na ambayo lazima ihifadhiwe, itetewe na ilindwe, katika uwanja mtakatifu kati ya dhamiri binafsi na Mungu. Baba Mtakatifu Francisko, amepitisha Ilani hii tarehe 21 Juni, 2019, na kuagiza kuchapishwe.

Imetolewa Roma, kwenye makao ya Idara ya Toba ya Kitume, tarehe 29 Juni, Mwaka wa Bwana 2019, Katika sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume.

Mauro Card. Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume

Mons. Krzysztof Nykiel, Hakimu wa Toba ya Kitume

Imetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili na Padre Florence Kamugisha Ngaiza (Jimbo Katoliki la

Bukoba – Tanzania)

14 March 2021, 14:33